Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes (48), amekataa kukisoma wala kukipokea kama zawadi kitabu cha maisha ya Askofu Mkuu wa kwanza wa dayosisi hiyo na Kanisa Anglikana nchini, John Sepeku.
Kitabu hicho chenye kurasa 287 kilichoandikwa na Jaji Mkuu mstaafu, hayati Augustino Ramadhani, kilichochapishwa mwaka 2017 kikiwa kinaeleza maisha ya hayati John Sepeku.
Askofu Sosthenes alikikataa kitabu hicho alipopewa na wakili wa upande wa madai katika kesi ya mgogoro wa ardhi inayomkabili yeye na wenzake katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.
Kesi hiyo namba 378/2023, imefunguliwa na Bernado Sepeku, mtoto wa Askofu Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Sosthenes na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Bernado ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yao anapinga uamuzi wa dayosisi hiyo chini ya uongozi wa Askofu Sosthenes kuwanyang’anya zawadi ya shamba alilopewa baba yao, na kumgawia mwekezaji kampuni ya Xinrong.
Anaiomba mahakama iamuru alipwe fidia ya Sh3.72 bilioni anayodai ni thamani ya shamba hilo kwa sasa na Sh493.65 milioni kama fidia ya hasara ya mazao yaliyoharibiwa katika shamba hilo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi hiyo zilizoko mahakamani, Desemba 8, 1978, Kamati ya Kudumu ya Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao ilipendekeza kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya ardhi ekari 20 na nyumba katika kutambua utumishi wake.
Sinodi ya dayosisi hiyo katika kikao cha Machi 8 na 9, 1980 iliridhia pendekezo hilo na iliazimia kumpatia Askofu Sepeku, shamba la ekari 20 lililoko Buza, wilayani Temeke na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Hata hivyo, uongozi wa sasa wa dayosisi uliligawa shamba hilo kwa mwekezaji, kampuni ya Xinrong, ambaye alifyeka mazao kisha akajenga kiwanda na nyumba yenye thamani ya Sh165 milioni.
Askofu Sosthenes ambaye ni shahidi wa tano wa utetezi, katika ushahidi wa maandishi aliouwasilisha mahakamani, pamoja na mambo mengine anadai waliompa Askofu Sepeku zawadi hizo hawakuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.
Alisisitiza msimamo huo hata wakati akihojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa mdai, Deogratius Butawantemi, Gwamaka Sekela na Eric Amon.
Wakati akihojiwa na wakili Butawantemi, jana jioni Oktoba 13, 2025 alizikataa nyaraka za ofisi yake pamoja mawasiliano yaliyotolewa na watangulizi wake kuhusu uamuzi wa kumzawadia hayati Sepeku ekari 20 na nyumba.
Baada ya kukataa kuzitambua nyaraka hizo, wakili Butawantemi alimpatia kitabu hicho ili akisome mahali ambako wakili huyo alimuelekeza.
Wakili Butawantemi alimwelekeza Askofu Sostheness asomewe ukurasa wa 249 wa kitabu hicho unaoeleza zawadi aliyopewa Askofu Sepeku ilitolewa baada ya vikao mbalimbali kufanyika kikiwamo cha Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi kilichofanyika mwaka 1978.
Hata hivyo, shahidi huyo aligoma kusoma kitabu hicho mpaka Jaji Arafa Msafiri anayesikiliza kesi hiyo, alipoingilia kati akamwelekeza asome ukurasa huo, ndipo akasoma.
Sehemu ya mahojiano kati ya wakili Butawantemi na shahidi ilikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Unamfahamu Jaji Augustino Ramadhani?
Wakili: Unafahamu kuwa baada ya kustaafu alipandishwa na kuwa padri? Na unafahamu ni mwandishi wa kitabu cha maisha ya Askofu John Thomas Sepeku?
Wakili: Alishaandika kitabu kinaitwa ‘Maisha ya John Thomas Sepeku’ na ndio mtunzi wa kitabu hicho?
Wakili: Mheshimwa jaji, naomba nimuonyeshe shahidi kitabu kilichoandikwa na Jaji Mkuu mstaafu, hayati Augustino Ramadhan. Naomba ukishike.
Shahidi: Sawa nimekishika.
Wakili: Shahidi unapenda kusoma?
Wakili: Nitakupa hiki kitabu shahidi ili uende ukakisome baadaye.
Shahidi: Nimesema sipendi kusoma.
Kutokana na msimamo huo Jaji Msafiri aliingilia kati na kumtaka asome kitabu hicho sehemu aliyoelekezwa ndipo akasoma ukurasa huo na sehemu aliyoelekezwa, kisha wakili Butawantemi akaendelea kumuhoji.
Miongoni mwa vielelezo vya ushahidi wa upande wa wadai ni barua mbalimbali za mawasiliano baina ya familia ya hayati Sepeku na Ofisi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, yalifanywa na watoto wa Askofu Sepeku, ambao ni Julius, Titus na Bernardo.
Mawasiliano hayo yaliyofanywa kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 1992, 2006, 2009 na 2016, yakihusu kukumbushia kucheleweshwa kupewa hati ya shamba lenye ukubwa wa ekari 20 kwa ajili ya mchakato wa kupatiwa umiliki wa eneo hilo.
Hata hivyo, watangulizi wake ambao ni miongoni mwa mashahidi wa upande wa madai katika kesi hiyo maaskofu wastaafu na waliowahi kuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamimi, walieleza kuwapo mawasiliano baina ya familia hiyo na Dayosisi ya Dar es Salaam.
Mashahidi hao ni pamoja na maaskofu Dk Valentino Mokiwa, Basil Simbano na Christopher Mlangwa.
Mashahidi hao walikiri kutambua, kuona na kushiriki vikao vilivyoridhia na kupitisha pendekezo la kumpa zawadi Askofu Sepeku, wakisema Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam ina mamlaka ya kufanya hivyo.
Walifafanua kuwa Sinodi ni Mkutano Mtakatifu wa Juu unaowahusisha Askofu wa Dayosisi, mapadri na waumini kwa ajili ya kufanya uamuzi wa kanisa na kwamba, uamuzi wake hauwezi kupingwa popote wala kutenguliwa na mtu yeyote.
Hata hivyo, Askofu Sostheness katika ushahidi wake na wakati wa mahojiano alidai hafahamu na hakuna kumbukumbu zinazoonyesha familia hiyo ilikuwa inafanya mawasiliano na dayosisi.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano zaidi baina ya wakili na shahidi huyo:
Wakili: Kwa kuwa wewe ni Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, habari zinazohusu makabidhiano ya nyumba ya ofisi yako, hayana maendeleo?
Wakili: Unafahamu familia ya hayati Sepeku imekuwa na mawasiliano na ofisi yako kuhusu kupatiwa hati ya umiliki wa eneo hilo?
Wakili: Pengine ieleze mahakama kama ni kweli ofisi yako haina mawasiliano na familia ya Sepeku?
Shahidi: Haina mawasiliano.
Wakili: Basi eneo ulilopangisha huyo mwekezaji, unafahamu lilikuwa na nyumba na mazao?
Shahidi: Sifahamu kwa sababu sijalima hapo.
Wakili: Shahidi unafahamu kuwa suala la Askofu Sepeku kupewa ardhi halikiwa suala la siri.
Wakili: Unafahamu maaskofu wote waliokutangulia waliheshimu uamuzi wa Sinodi ya mwaka 1980?
Kesi hiyo imeahirishwa mpaka Oktoba 15, 2025 itakapoendelea kwa shahidi kuulizwa maswali na wakili wake, Dennis Malamba.