Camara ashtua akiiweka mtegoni Simba

HII inaweza isiwe taarifa njema kwa mashabiki wa Simba, kwani kipa namba moja wa kikosi hicho, Moussa Camara amezua hofu baada ya kuonekana hajapona na kushindwa kucheza mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji, Oktoba 9, 2025.

Camara ambaye huu ni msimu wake wa pili ndani ya Simba, tangu atue kikosi hapo amekuwa hana mpinzani katika nafasi hiyo hata kwenye timu ya Taifa.

Kipa huyo ni miongoni mwa mastaa wa Simba walioitwa na timu za Taifa, kwa ajili ya michuano ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 na anaitumikia Guinea iliyo Kundi G na pointi 14, huku leo Oktoba 14, 2025 ikikabiliana na Botswana.

Katika mechi dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Oktoba 9, Camara alikuwa benchi wakati Guinea ikiibuka na ushindi wa mabao 1-2 ugenini.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa: “Huenda Camara hataweza kucheza mechi ijayo dhidi ya Botswana (leo Jumanne usiku), kwani hali yake bado haijatengamaa sawasawa.”

Camara alipata majeraha kwenye mechi ya pili hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, kwani toka mchezo huu uliomalizika kwa sare 1-1 hajaonekana uwanjani.

CAMA 01

Taarifa za ndani kutoka Simba zililiambia Mwanaspoti: “Kipa Moussa Camara amezusha hofu baada ya kuonekana hajapona sawasawa na kushindwa kucheza mchezo dhidi ya Msumbiji na leo pia kuna hatihati kubwa atakosa mchezo dhidi ya Botswana unaochezwa nchini Guinea.

“Jambo linalowapasua vichwa viongozi na hata benchi la ufundi ni wasiwasi wa kukosekana kwake, kwani sidhani kama atakuwa tayari kabla ya mchezo dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini.”

Oktoba 19, 2025, Simba itakuwa Eswatini kukabiliana na Nsingizini Hotspurs, ikiwa ni mechi ya kwanza ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, marudiano ni Oktoba 26, 2025.

Ikumbukwe kuwa, katika nafasi anayocheza Camara, kuna Yakoub Suleiman na Hussein Abel na hata alipokosekana kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, langoni alisimama Yacoub, kipa namba moja wa Taifa Stars kwa sasa.

Msimu uliopita Camara alidaka mechi 28 za Ligi Kuu Bara akikusanya clean sheet 19 na kuwa kinara, huku pia akidaka mechi zote za Kombe la Shirikisho Afrika wakati Simba ikicheza hadi fainali na kupoteza dhidi ya RS Berkane.

CAMA 02

Wakati huohuo, mechi mbili za kirafiki ilizocheza Simba dhidi ya Al Hilal, zimetajwa kama sehemu ya kuiboresha timu hiyo, huku wakongwe wakionya jambo.

Oktoba 9, 2025, Simba iliifunga Al Hilal mabao 2-1, katika mechi ya kwanza ya kirafiki iliyochezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo. Wafungaji wa Simba ni Jean Charles Ahoua na Jonathan Sowah. Baada ya hapo, Oktoba 12, 2025, Simba ikafungwa 4-1 na Al Hilal, mechi ikichezwa Uwanja wa Gymkhana, Dar. Bao la Simba lilifungwa na Elie Mpanzu. Yale ya Al Hilal wafungaji ni Adama Coulibaly, Hajj Madiki na Sunday Adetunji aliyetupia mawili.

Kutokana na matokeo hayo, beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Amir Maftah amesema benchi la ufundi la timu hiyo, limepata kipimo kizuri kabla ya kucheza dhidi ya Nsingizini Hotspurs.

“Kucheza na Al Hilal ambayo pia inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika hilo linaisaidia Simba kusahihisha makosa kabla ya mechi yao ya Jumapili itakayopigwa ugenini dhidi ya Nsingizini, eneo la kwanza ninaloliona linatakiwa kufanyiwa marekebisho ni mabeki, maana mechi mbili wamerehusu mabao matano.

“Natambua kuna wachezaji wapo katika timu zao za taifa, lakini haijalishi wanatakiwa wachezaji wote wawe na uwiano wa kiwango, kupitia mechi hizo makocha watajua kipi wakifanye,” amesema Maftah.

Aliyekuwa beki wa Yanga na Taifa Stars, Oscar Joshua, amesema: “Mechi za kirafiki zinawasaidia makocha na wachezaji kujua kikosi kina ubora na mapungufu gani, hivyo Simba itakuwa na wakati mzuri wa kujipanga zaidi kabla ya mechi yake ya CAF.”

CAMA 03

Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni amesema: “Mechi za kirafiki zinawasaidia makocha kutambua kikosi chake ni cha aina gani pia, kwa Pantev atapata wakati mzuri wa kumfahamu kila mchezaji ana uwezo gani.

“Safu ya mbele inafunga, ndiyo maana Sowah, Mpanzu na Ahoua wote wamemuonyesha kocha wana uwezo wa kutumia nafasi, kikubwa waangalie namna ya timu kuwa imara katika kujilinda.”

Msimu uliopita, Sowah akiwa Singida Black Stars alikosajiliwa dirisha dogo alifunga mabao 13 huku Ahoua alikuwa kinara wa mabao 16 na asisti tisa katika Ligi Kuu Bara, ilhali Mpanzu alifunga mabao manne na asisti sita.”