HUDUMA ZA FORODHA ZIMEZIDI KUIMARIKA

 

::::::::::

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema huduma za Forodha katika Bandari ya Dar es Salaam zimeendelea kuimarika ikiwemo upakuaji na usafirishaji wa sheshena mbalimbali kwa wakati. 

Ameyasema hayo leo tarehe 14.10.2025 alipofanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam upande wa Forodha kwa lengo la kuangalia mwenendo wa utoaji wa huduma kwa shehena zinazopitia kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Akiwa bandarini hapo Kamishna Mkuu Mwenda ameshuhudia shughuli za upakiaji na upakuaji wa mizigo zikiendelea kufanyika na kueleza kuwa TRA upande wa Forodha itaendelea kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa walipakodi. 

“Nimekuja hapa Bandarini kwa lengo la kuona shughuli mnazofanya na nimeziona zikiendelea vizuri, tuongeze ubora katika utoaji wa huduma zetu, hiyo itaongeza zaidi imani na ulipaji wa kodi kwa hiari kwa walipakodi tunaowahudumia” amesema Kamishna Mkuu Mwenda. 

Amesema kipaumbele cha TRA ni kutoa huduma bora na kwa wakati kwa walipakodi ili kuongeza ari ya uhiari katika kulipa kodi kwa wakati kwa maendeleo ya Taifa. 

Kamishna Mkuu Mwenda amewapongeza watumishi wa TRA upande wa Forodha kwa kujituma na kuwezesha kuvuka malengo ya makusanyo ya kodi kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 na kuwataka kuongeza juhudi zaidi na kuzingatia maadili. 

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Forodha Naibu Kamishna Bw. Felix Tinkasmile amesema ziara ya Kamishna Mkuu Bandarini itaongeza chachu ya uwajibikaji sambamba na makusanyo ya Kodi. 





= = = = = =