KLABU ya Yanga, leo Oktoba 13, 2025 imemtambulisha Patrick Mabedi kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo chini ya Mjerumani, Romain Folz.
Mabedi ametua Yanga kuchukua nafasi ya Manu Rodriguez, aliyewasilisha barua ya kuomba kuvunja mkataba wake kufuatia kupata changamoto ya kiafya.
Patrick Mabedi amezaliwa Novemba 5, 1973, mwaka huu anatimiza miaka 52. Huyu ni kocha wa soka raia wa Malawi na mchezaji wa zamani aliyekuwa akicheza kama beki wa kati. Pia amewahi kuitumikia timu hiyo ya taifa akiwa mchezaji na kocha. Anajulikana kwa majina ya utani Bosti au The General.

Katika maisha ya kucheza soka, amepita timu za Big Bullets ya Malawi (1997–1998), Kaizer Chiefs (1998–2006) na Moroka Swallows (2006–2008) zote za Afrika Kusini. Kisha akastaafu kucheza soka Julai 01, 2008.
Ndani ya Kaizer Chiefs, chini ya kocha Ted Dumitru, Mabedi na Fabian McCarthy waliunda safu imara ya ulinzi iliyoisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa ligi msimu wa 2003-2004 baada ya miaka 12, kwa mtindo wa kuvutia, wakiwa na tofauti ya pointi sita dhidi ya Ajax Cape Town waliomaliza nafasi ya pili, na wakiwa wamepoteza michezo mitatu pekee msimu mzima.
Mabedi alianza kazi yake ya ukocha kama mkuu wa kitengo cha vijana cha Moroka Swallows nchini Afrika Kusini kuanzia Septemba 30, 2011 hadi Juni 30, 2015, na baadaye akateuliwa kuwa kocha wa muda timu ya wakubwa msimu wa 2014–2015. Kazi yake ilianza Machi 17, 2015 hadi Machi 25, 2015, kisha alipotua Muhsin Ertuğral, yeye akawa msaidizi wake.
Nafasi ya kocha msaidizi ndani ya Swallows iliendelea kuanzia Machi 26, 2015 hadi Juni 30, 2015.
Msimu uliofuata, aliondoka Swallows na kujiunga na Mpumalanga Black Aces, ambapo alifanya kazi kama kocha msaidizi wa Ramadhan Nsanzurwimo kuanzia Julai 01, 2015 hadi Agosti 07, 2016. Timu hiyo ilimaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu ya Afrik Kusini, ikiwa pointi 24 nyuma ya mabingwa Mamelodi Sundowns.
Kuanzia Agosti 08, 2016 hadi Septemba 18, 2016, alihudumu kwa muda mfupi kama kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Malawi kabla ya kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa Cape Town All Stars, timu aliyoiwezesha kumaliza katika nafasi ya tisa kwenye Ligi Daraja la Kwanza ya Taifa (National First Division) msimu wa 2016–2017. Ilikuwa kuanzia Septemba 19, 2016 hadi Juni 12, 2017.
Mnamo Juni 13, 2017, Mabedi aliteuliwa kuwa kocha msaidizi wa Kaizer Chiefs chini ya Giovanni Solinas. Aprili 23, 2018, alipandishwa cheo na kuwa kocha wa muda (caretaker coach) hadi mwisho wa msimu, Juni 30, 2018.

Julai 01, 2018 hadi Desemba 7, 2018, alikuwa kocha msaidizi wa Kaizer Chiefs chini ya Lionel Soccoia. Wawili hao wakaondoka pamoja na Julai 01, 2019 wakatua Black Leopards, hawakudumu sana, ajira yao ilifika mwisho Septemba 17, 2019.
Kuanzia hapo, akaondoka Afrika Kusini alipodumu kwa muda mrefu na kurejea nchini kwao Malawi, akakabidhiwa kikosi cha timu ya taifa hilo akianza kama kocha wa muda kuanzia Aprili 26, 2023 hadi Oktoba 22, 2023, ndipo akawa kocha mkuu rasmi hadi anatambulishwa ndani ya Yanga. Mkataba wake na Malawi ulikuwa unafikia tamati Desemba 31, 2025.
Mabedi alianza kupata Leseni C nchini kwao Malawi, kisha Leseni B na A ya CAF. Akaenda Ujerumani kuongeza ujuzi, akafanikiwa kupata Leseni ya UEFA B kisha A kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Ujerumani (DEUTSCHER FUSSBALL-BUND).
Sifa hizo zinamfanya kuwa na uwezo wa kukaa katika benchi la ufundi la timu yoyote ya Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu Bara kama kocha mkuu kwani amekidhi kigezo cha kanuni ya 77:3 (1,2,3).