Kauli ya Nyerere, ikulu ni mahali patakatifu, yawafikirisha wasomi

Wakati ikitimia miaka 26 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere afariki dunia, moja ya kauli zinazokumbukwa katika hotuba zake alizowahi kuzitoa ni kwamba: “Ikulu ni mahali patakatifu.”

Mwalimu Nyerere alitoa kauli hiyo wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995 huku akikemea vitendo vya rushwa alivyosema vilishamiri kwa viongozi waliokuwa wakitaka kuingia ikulu.

Katika hotuba hiyo, Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba, mtu anayetaka uongozi wa nchi, lazima ajiepushe na kukemea vitendo vya rushwa na awe na uwezo wa kuwaambia ndugu na marafiki zake kwa kauli watakayoisikiliza.

“Kiongozi uwe na uwezo wa kuwaambia jamaa zako, na rafiki zako, kwa kauli ambayo wataiheshimu na wala hawatarudia tena, ikulu ni mahali patakatifu…mimi sikuchaguliwa na wananchi kuja kupageuza kuwa pango la walanguzi.

“Ukishawaambia hivyo ndugu zako, marafiki zako, mtu mwingine wala hakusogelei, nafsi yake haimtumi kukusogelea,” alisema Mwalimu Nyerere katika hotuba hiyo wakati viongozi mbalimbali wakitangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi huo.

Sasa, Taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, tayari wagombea 17 wanaowakilisha vyama vyao, wanaendelea na kampeni za uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini wakinadi ilani za vyama vyao na kutoa ahadi kwa Watanzania.

Mwangwi wa kauli ya Mwalimu Nyerere kwamba, “ikulu ni mahala patakatifu…si pango la walanguzi,” bado unasikika kama kilio cha kimaadili kinachoikumbusha Tanzania kuheshimu misingi ya utawala bora na kupiga vita rushwa hasa wakati wa uchaguzi.

Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kisiasa na kijamii, waliozumgumza na Mwananchi, wanaeleza kukubaliana na falsafa ya Mwalimu Nyerere kwa sababu vitendo vya rushwa vinashamiri zaidi wakati wa uchaguzi hasa kwa watu wanaosaka uongozi wa nchi.

Mwanahistoria na mwandishi maarufu wa vitabu nchini, Dk Mohammed Said anaeleza kuwa, Mwalimu Nyerere alikuwa mfano bora wa kiongozi asiyeongozwa na tamaa za mali wala madaraka.

“Ni vigumu leo kupata viongozi wa aina ya Nyerere. Wengi wametawaliwa na tamaa ya fedha, wakisahau kuwa mamlaka ni dhamana, si fursa ya kujitajirisha,” anasema Dk Said.

Anasimulia kisa cha uadilifu wa Mwalimu Nyerere wakati alipoletewa barua na benki moja ya Uswisi, ikimshauri ahamishie fedha zake huko kwa usalama zaidi.

“Akionekana kuchukizwa na kitendo kile, Mwalimu alimwonesha barua hiyo Waziri wa  Fedha, Amir Jamal na akaagiza haraka ichapishwe ukurasa wa mbele wa gazeti la Serikali (Daily News) ili kuwapa ujumbe wazungu hao kwamba yeye hakuwa kiongozi wa kupapasa pesa,” anasema Dk Said.

Dk Said anakumbusha mfano mwingine wa uadilifu kwa marehemu Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Pili wa Zanzibar.

“Alipopokea bahasha ya dola kutoka kwa Rais wa Libya, Muhammar Gaddafi kwa ajili ya matibabu nchini Marekani alikokwenda kutibiwa, aliporejea Zanzibar, aliikabidhi Hazina ya Serikali badala ya kuitumia binafsi. Huu ndio uongozi wa kupigiwa mfano ambao Mwalimu alitaka uendelee,” anasisitiza.

Dk Said anasema, Mwalimu Nyerere hakusema maneno hayo kama kejeli, bali kama waraka wa maadili wa kizazi kwa kizazi na akisisitiza kuwa, Ikulu si mahali pa tamaa, bali ni alama ya heshima ya Taifa.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Profesa Mohamed Makame anaona kauli hii ilizaliwa kutokana na mabadiliko ya mfumo wa kisiasa baada ya kuingia kwa vyama vingi mwaka 1992.

“Wakati wa chama kimoja, viongozi walichaguliwa kwa heshima na maadili. Lakini demokrasia ya vyama vingi ilileta ushindani, na watu wakaona urais kama tiketi ya biashara,” anasema Profesa Makame.

Anabainisha kuwa, mwaka 1995, Mwalimu Nyerere aliona wimbi la wanasiasa wanaotafuta madaraka kwa gharama yoyote, akatamka kwa busara kuwa: “Ikulu ni mahala patakatifu, si pango la walanguzi.”

“Kauli hii ni onyo lililodumu hadi leo,” anaeleza Profesa Makame, akiongeza kuwa: “Ni wito kwa wananchi kutochagua watu kwa misingi ya pesa au ushawishi wa muda, bali kwa heshima, utu na dhamira njema.”

Anafafanua kuwa, ikulu ni taasisi ya kutumikia Watanzania wote, si jukwaa la kunufaisha mitandao ya kisiasa. “Watanzania lazima wajihadhari na wanasiasa wanaoona uongozi kama njia ya biashara.”

Mchambuzi mwingine wa masuala ya kijamii kutoka Mtwara, Azikiwe Borauf anatafsiri kauli ya Nyerere kwa namna ya kipekee: “Ikulu ni sawa na nyumba ya ibada.”

 “Mwalimu alihamisha dhana ya utakatifu kutoka kwenye dini hadi kwenye uongozi.

“Kwamba kiongozi anayeingia ikulu anapaswa kujitathmini kama mtu anayejiandaa kwenda kusali. Je, ana udhu wa uadilifu au anaingia akiwa mchafu wa maadili?”

Anamnukuu kiongozi wa zamani, Paul Kimiti, aliyekataa kugombea urais licha ya kushawishiwa na Mwalimu Nyerere, akisema, “hawezi kubeba mzigo mzito kama huo.”

“Mwalimu alimpongeza Kimiti kwa kusema ni mtu muadilifu. Je, leo kuna viongozi wangapi wanaweza kujitathmini hivyo kabla ya kukimbilia kugombea urais?” anauliza Borauf.

Anasema Nyerere aliona mapema dalili za kuibuka mitandao ya watu wanaowekeza fedha nyingi ili “kumnunua mgombea. “Uongozi si biashara, bali ni huduma. Ukifanya uwekezaji ili kufika ikulu, utalazimika kulipa kwa kuchukua mali za umma,” anatahadharisha Borauf.

Urais ni dhamana, si cheo

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), Nassor Ali anaeleza kuwa, Mwalimu Nyerere alitumia neno patakatifu, kuashiria usafi wa dhamira.

“Mwalimu alikuwa akiwaoneshea kidole wanasiasa waliokuwa wakianza kampeni wakiwa na mizigo ya tuhuma na makandokando ya kimaadili,” anasema Ali.

Kwa mujibu wake, Nyerere alitaka Watanzania waelewe kwamba uongozi ni ibada, si starehe.

 “Ikulu si pa kwenda kupata raha, bali ni jukwaa la kuwatumikia wananchi. Kwa anayeona urais kama cheo cha kujitukuza, huyo hafai hata kuanza kampeni,” anasisitiza.

Ali anaongeza kuwa falsafa hii bado ina umuhimu mkubwa leo, hasa wakati ambao siasa zimegeuka jukwaa la fedha na propaganda.

“Watanzania wanapaswa kumchagua kiongozi mwenye moyo wa huduma, si mwenye tamaa ya madaraka,” anashauri.

Mchambuzi wa siasa, Abdulkareem Atiki anaona kauli hii kama dira ya kudumisha uchaguzi wa haki na heshima.

“Kwa vyombo vya uchaguzi kama INEC (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi), ni mwongozo wa kusimamia haki bila upendeleo. Kwa wananchi, ni wito wa kuchagua viongozi wa maadili, si wa pesa au ukabila,” anasema Atiki.

Anatoa mifano ya kihistoria inayoonesha uhalisia wa falsafa ya Nyerere.

“Mwalimu mwenyewe aliongoza kwa uadilifu na kujitolea. Nelson Mandela aliweka msamaha na utu mbele ya kisasi. Hayati John Magufuli alisisitiza nidhamu na kupambana na rushwa, wote hawa walionyesha roho ya Ikulu kama mahali patakatifu.”

Atiki anafafanua kuwa utakatifu unaotajwa na Nyerere si wa kidini, bali wa kimaadili: “Ni usafi wa moyo, uwazi, unyenyekevu na kuheshimu Katiba.”

Anasisitiza kuwa, mamlaka siyo uwanja wa kuwatisha wananchi, bali ni nafasi ya kutengeneza imani na heshima. “Kiongozi wa kweli hutawala kwa heshima, si kwa woga,” anaongeza.