Mgombea urais AAFP aahidi Taifa Stars kushinda Afcon

Geita. Mgombea urais kupitia chama cha AAFP, Kunje Ngombale Mwiru ameahidi timu ya mpira wa miguu ya Taifa Stars kuleta kombe la Afrika (Afcon) endapo atachaguliwa kuwa rais wa Tanzania.

Kunje ameyasema hayo leo Oktoba 14, 2025 katika uwanja wa Satellite mjini Katoro alipokuwa akinadi sera zake za urais.

“Mkinichagua ndani ya miaka mitano nitaleta kombe la Afrika, haiwezekani timu inachaguliwa kisiasa na inaongozwa kisiasa, mkinichagua ndani ya miaka mitano naleta kombe kupitia goli la Mzalendo,” amesema Kunje.

Ameongeza kuwa timu ya Taifa haifanyi vizuri katika mashindano ya kimataifa kutokana na soka kutawaliwa na siasa katika uendeshaji pamoja na uteuzi wa kocha na wachezaji.

“Eti unafungwa tena nyumbani? Mechi muhimu? Eti wachezaji wa kupeanapeana, mchezaji anacheza kama hajala halafu mnachekacheka naye.

“Mimi nitahimiza michezo kupitia ‘goli la Mzalendo’ sitakuwa na goli la baba wala goli la kaka, timu inafungwa na watu wanacheka tu,” amesema mgombea huyo.

Mgombea urais kupitia chama cha AAFP, Kunje Ngombale Mwiru akinadi sera zake uwanja wa Satellite mjini Katoro,Geita Leo Oktoba 14,2025

Kuhusu uwepo wa maandamano siku ya uchaguzi mkuu, Kunje amesema wanaotishia kudhibiti watu watakaoandamana majukwaani, wanawaonea Watanzania kwa kuwa hawana hata Gobole.

Amesema ni hofu iliyowajaa watendaji ambao hawakutekeleza majukumu yao na wao ndiyo sababu ya wananchi kulalamika.

“Hawa wanaGeita hawana hata gobole, kama umewafanyia mazuri, hofu yako ni nini? Mashaka yako ni nini? Kiongozi mwingine anasema ungenipa nafasi ya naibu IGP ningewavunja miguu, nani ataleta maandamano? Hawafanyi kazi zao kila sehemu wananchi wanalalamika,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kunje amelipongeza Jeshi la Polisi nchini akisema wanafanya kazi nzuri katika kudumisha amani nchini bila kujali changamoto zinazowakabili.

Aidha, Kunje amesema kuwa miundombinu ya umeme haipo katika ubora hali inayotishia usalama wao, yakitokea majanga ya moto huku wananchi wengi wakiwa hawana bima za afya, hivyo akishinda urais nyaya za umeme zitapita chini ya ardhi kwenye mabomba.

“Hapa ukija upepo au kimbunga ni hatari, hizi nyaya zimekaa ovyo lakini kwao haiko hivyo, nimetembea nchi nyingi, haya mambo huko hakuna na yakitokea maafa wananchi hata bima ya afya hawana, nawaahidi mkinichagua bima ni bure mambo ya majaribio kwangu hapana,” amesema Kunje.

Kuhusu uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, Kunje amewahimiza wapigakura kumchagua na kutokana na kampeni alizopiga nchi nzima, ana uhakika wa kushinda uchaguzi ujao huku akiwataka wananchi kuendelea na shughuli zao baada ya kupiga kura akisema atazilinda mwenyewe.