Mbeya. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo amewataka Watanzania kutoshiriki kwenye maandamano yaliyopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025, badala yake watumie sanduku la kura kuleta mageuzi.
Ametoa wito huo akilenga kudumisha amani na utulivu wa nchi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani pasipo kuzua taharuki.
Gombo amebainisha hayo leo Jumanne Oktoba 14, 2025 mkoani Mbeya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Gombo amewataka wananchi kutumia njia mbadala ya kupiga kura ili kuleta mabadiliko badala ya kutumia maandamano ambayo ni chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani nchini.
“Watu waliopanga kufanya maandamano hawana nia njema, lakini mwafaka ni kupiga kura na kuichagua CUF ambayo imebeba ajenda ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli na taifa kwa ujumla,” amesema.
Amesema suluhisho la wananchi katika kufanya uamuzi wa Oktoba 29, 2025 ni kumpigia yeye kura nyingi za kutosha ili alete mabadiliko ya kweli katika nyanja mbalimbali na kutekeleza vipaumbele vyake.
Ametolea mfano Madagascar, ambayo imeingia kwenye machafuko baada ya wananchi kuipinga Serikali kwa njia ya maandamano kwa lengo la kuindoa madarakani, jambo ambalo si busara na limesababisha umwagaji damu, uharibifu na ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
Amesema akichaguliwa kuwa Rais, atamaliza changamoto ya migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na kuhakikisha miji yote mikubwa nchini inakuwa na miundombinu ya makazi yenye mpangilio ili iendane na hadhi ya majiji.

Mgombea Urais wa Chama cha Wananchi (CUF),Gombo Sambandito Gombo akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Oktoba 14,2025 Mkoa wa Mbeya.Picha na Hawa Mathias
“Majiji ambayo yatakuwa ni kipaumbele ni ya Mbeya, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Arusha, mimi nina taaluma ya mipango miji, hivyo nitaifumua miji hiyo na kupanga upya,” amesema.
Gombo amesema kwa kipindi kirefu wanaona changamoto hizo, amejipima na kujipanga kuondoa mpangilio mbovu wa miji kwa kuzingatia miundombinu muhimu, hususan ya barabara.
Wakati huohuo, amebainisha upungufu wa Sh1 milioni kwa ajili ya kuwalipa mawakala 100,000 wa chama hicho nchini, ili kurahisisha shughuli ya kuhesabu kura Oktoba 29, 2025.
Gombo ameomba Watanzania kuchangia fedha kupitia akaunti ya benki ya NMB yenye namba 52810030530 na majina Gombo Samandito Gombo.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu wakati wa mchakato wa uchaguzi kwa madai kuna maisha mengine baada ya uchaguzi.
“Kama kijana nahamasisha wenzangu, siku ya uchaguzi wajitokeze kupiga kura, lakini pia kushiriki kwenye mikutano ya kampeni kusikiliza sera za vyama vya siasa na kuja na majawabu ifikapo Oktoba mwaka huu,” amesema Mwanaisha Hussen.
Ameshauri Serikali kuendelea kudumisha kaulimbiu ya mbio za mwenge kwa kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu mwaka huu ili kudumisha amani na utulivu wa Tanzania.