Mpango: Misingi ya Nyerere isimamiwe kuepusha Taifa kusambaratika

Mbeya/Mikoani. Watanzania wameaswa kuenzi maisha na mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kusimamia misingi mikuu aliyoiacha ya kulinda uhuru wa Taifa, umoja, amani na kusimamia haki miongoni mwa jamii, vinginevyo ipo hatari ya Taifa kusambaratika.

Akizungumza leo Oktoba 14, 2025 katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa jijini Mbeya, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema bila kufanya mambo hayo kwa dhati ipo hatari ya Taifa kusambaratika.

Amesema Watanzania wanapaswa kusimamia na kujenga maadili mema katika jamii, hasa kwa vijana ambao ndio Taifa la leo na kesho.

Dk Mpango amesema ni lazima kukemea mmomonyoko wa maadili, ikiwamo rushwa na ufisadi ambavyo Baba wa Taifa alivichukia na kupiga vita kwa vitendo.

Akizungumzia kuhusu uwajibikaji, ametaka kila mwananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha na kuinua vipato vyao na kuchangia ujenzi wa Taifa.

“Niwahimize vijana kuchangamkia fursa zilizopo na zinazochipukia katika sekta mbalimbali ikiwamo Tehama, kilimo na michezo,” amesema.

“Kila mmoja atambue anao wajibu katika kuijenga nchi, Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe. Tutunze na kuhifadhi mazingira hasa kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti na kufanya usafi kama alivyokuwa Baba wa Taifa.”

Kuhusu mbio za Mwenge wa Uhuru, amesema Taifa limefanikiwa kuondoa ubaguzi, ukabila na kujenga umoja wa kitaifa, kuimarisha utawala bora, kupinga dhuluma, dharau, chuki, ufisadi na rushwa.

“Niwahimize vijana kuendelea kutumia ubunifu, maarifa na nguvu zenu. Serikali inawaamini na itawaunga mkono, kwani imewekeza ili kuwajengea uwezo kushiriki kiuchumi na fursa zinazojitokeza,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere inawakutanisha Watanzania na kuwakumbusha misingi ya umoja, upendo na utu.

Amesema kupitia mbio hizo, ujumbe muhimu kuhusu maendeleo, uwajibikaji, uadilifu na uzalendo unaendelea kusambazwa nchini, akieleza Serikali imeendelea kuyatenda maono hayo kwa vitendo kwa kuimairisha uchumi wa Taifa.

“Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume walituachia urithi mkubwa wa uadilifu, uwajibikaji na uongozi wa kujituma kwa ajili ya watu, hivyo ni jukumu letu kuenzi urithi wetu kwa kushiriki uchaguzi kwa amani,” amesema na kuongeza:

“Vilevile kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi, ndivyo tunapaswa kudumisha heshima na hadhi ya Taifa letu kama mfano wa demokrasia yenye amani Afrika.”

Waiziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema mbio za Mwenge wa Uhuru zimetoa elimu kwa wananchi kujua umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi mkuu.

“Katika siku 195, Mwenge umekagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi zaidi ya 3,182 yenye thamani ya Sh2.9 trilioni, ikiwamo ya sekta za elimu, afya, maji na barabara,” amesema.

Amesema kati ya watu 62,257 waliopimwa 335 sawa na asilimia 0.6 walibainika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ambao walipewa ushauri na kuanza tiba.

Kuhusu mapambano dhidi ya vimelea vya malaria, amesema watu 28,928 walifanyiwa uchunguzi wa vipimo kati ya hao 831 sawa na asilimia 3.1 walibainika kuwa na vimelea.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2025, Ismail Ally Ussi  amesema wameridhishwa na miradi iliyotekelezwa na iliyokamilika hususani katika sekta za elimu, afya, maji na mingine, hivyo kuboresha huduma kwa wananchi.

Awali, Dk Mpango na viongozi wengine walishiriki adhimisho la misa kumuombea Mwalimu Nyerere katika Kanisa Katoliki Mwanjelwa, ikiwa ni kumbukizi ya miaka 26 ya kifo chake.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya, Gervas Nyaisonga, amesema Nyerere alikuwa mtu mwenye mwenendo wa huruma, upendo na uaminifu, hali hiyo hufanya mtu kuwa mtakatifu bila kujali itikadi zake za kidini.

Amesema mchakato wa kufikia utakatifu ni kupewa hadhi ya utumishi kwa kuzingatia hisia hasa katika jimbo lake la utumishi, mwenye fadhila kuu, kisha kutangazwa mtu kuwa mwenye heri.

“Hatua ya mwisho ni kuwa mtakatifu ambaye amehakikishiwa na kanisa kwamba yuko mbinguni, hivyo, mchakato wa Nyerere kutangazwa upo hatua ya kwanza na hatua hii itachukua muda mrefu,” amesema.

 “Mchakato unaendelea na tutatangaza akifikia hatua ya kuwa mtakatifu. Anahisiwa kuwa hivyo kutokana na alivyothibitisha, alikuwa mfuata maadili, haki, mnyenyekevu na mwaminifu.”

Nyaisonga amesema Mwalimu Nyerere aliacha urithi wa elimu na kufanya lugha ya Kiswahili kutumika kimataifa na alionesha uadilifu katika utumishi bila kuweka masilahi binafsi.

Amesema hata baada ya kustaafu alikuwa akitoa maoni yake bila kusita kwa mustakabali wa nchi.

Mgombea wa nafasi ya makamu wa Rais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema chama kitaendelea kupambana dhidi ya maadui watatu aliowatangaza Mwalimu Nyerere ambao ni ujinga, maradhi na umaskini kwa nguvu zote.
Mwalimu Nyerere aliyeongoza kupigania Uhuru wa Tanganyika sasa Tanzania uliopatikana Desemba 9, 1961, aling’atuka madarakani akiwa Rais mwaka 1985 na alifariki dunia Oktoba 14, 1999, London, nchini Uingereza alikokwenda kwa matibabu.

Dk Nchimbi akihutubia mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Kindiko, Wilaya ya Mkalama, Jimbo la Iramba Magharibi, mkoani Singida, amesema Mwalimu Nyerere ataendelea kukumbukwa daima.
Amesema ilani ya uchaguzi mkuu ya chama hicho ya mwaka 2025/2030, imebainisha jinsi inavyokwenda kuendelea kutafuta suluhu ya maadui hao watatu aliowasema Mwalimu Nyerere, Desemba 9, 1961.
Dk Nchimbi amesema ujenzi wa shule, hospitali, mikopo ya asilimia 10 na kuboresha sekta za kilimo na ufungaji ni miongoni mwa mambo yatakayotokomeza maadui hao.

“Leo tutafanya kosa kubwa sana kama tukiacha misingi ya umoja, mshikamano na amani kwa nchi yetu, huku tukidai tunamuenzi Baba wa Taifa,” amesema.

Dk Nchimbi amesema katika kipindi chake Mwalimu Nyerere, jambo kubwa alilosimamia kuliko yote ilikuwa kuhakikisha nchi inajitegemea

“Kwa hiyo niwaambieni wana Mkalama, tutafanya kosa kubwa sana kama tutamsahau Baba wa Taifa. Alifanya kazi kubwa kubwa na ya kizalendo,” amesema.
 

Mgombea urais  wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi waa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amesema namna nchi inavyoendeshwa sasa siyo kwa umoja na mshikamano aliouacha Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake.

Akihutubia mkutano wa kampeni eneo la soko la matunda wilayani Nachingwea, mkoani Lindi, amesema kipindi cha Nyerere katika kudumisha umoja na mshikamano hakukuwa na utoaji huduma za kubagua watu, lakini leo kuna shule na hospitali binafsi, huku huduma zikitofautiana kwa kiasi kikubwa.

“Enzi za mwalimu hakukuwa na shule za binafsi wala hospitali binafsi hali iliyofanya tusome na watoto wa mawaziri, lakini leo hii hata mtoto wa mkuu wa wilaya au mkoa hawezi kusoma shule zetu, hivyo kuchangia utoaji elimu kuwa mbaya,” amesema.

“Mkinipa ridhaa ya kuongoza nchi nakwenda kudumisha umoja na mshikamano kwa kuhakikisha huduma zote zinatolewa kwa usawa kwani hatuwezi kumuenzi Baba wa Taifa wakati umaskini unaongezeka, huduma za kijamii zinadorora, hii siyo nchi aliyotuachia na wala sivyo tunavyotakiwa kumkumbuka.”

Amesema wakati Mwalimu Nyerere anaimba wimbo wa umoja na mshikamano alikuwa akiendeleza nchi, ikiwamo uanzishwaji wa viwanda mkoani Tanga lakini leo vyote vimekufa.

Mgombea huyo amesema Mwalimu Nyerere hakuwa akiuza gesi wala kuanza kuchimba mafuta, lakini kulikuwa na ahueni ya maisha katika mikoa ya kusini ikiwamo kutegemea kilimo.

“Leo Lindi mna bahari, gesi, mafuta na korosho ambazo dunia inazichukulia kama dhahabu lakini mnatawaliwa na umaskini na kutoona maana ya kuwa na rasilimali hizo. Naomba chagueni Chaumma tuwaletee mabadiliko,” amesema.

Imeandikwa na Sadam Sadick na Hawa Mathias (Mbeya), Ibrahim Yamola (Singida) na Nasra Abdallah (Nachingwea)