Iringa. Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, inaendelea kutekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi(HEET), unaolenga kubadilisha mfumo wa elimu ya juu nchini ikilenga kutoa mchango wa moja kwa moja katika mageuzi ya kiuchumi.
Kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (MUCE), kimenufaika kwa kujenga miundombinu ya kisasa, kuanzisha kituo cha watu wenye mahitaji maalumu, dawati la masuala ya kijinsia na kuboresha teknolojia ya ujifunzaji kwa njia ya mtandao.
Hatua hizo zimeongeza usawa wa kijinsia, ujumuishaji wa wanafunzi wote na kuimarisha ubora wa elimu chuoni hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo leo Jumanne Oktoba 14, 2025, Rasi wa MUCE, Profesa Method Semiono amesema chuo hicho kimepata Sh18.6 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi sita ikiwamo ya uboreshaji wa mitalaa, ujenzi wa miundombinu, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na kuimarisha elimu jumuishi na usawa wa kijinsia.
Profesa Semiono amesema kupitia mradi huo, MUCE imefanya mapitio ya mitalaa mitano ya zamani na kuanzisha mipya 30.
Amezitaja programu saba za umahiri na mbili za uzamivu, akisema jambo hilo limepanua wigo wa elimu na kuongeza idadi ya wanafunzi hadi kufikia zaidi ya 10,000.
“Mradi huu wa miaka mitano (2021/2022–2025/2026) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha elimu ya juu. Kupitia HEET, MUCE kimekuwa mfano wa mabadiliko chanya katika sekta ya elimu nchini,” amesema Profesa Semiono.
Ameongeza kuwa uboreshaji wa mitalaa na mbinu za ufundishaji umezingatia mahitaji ya soko la ajira, kwa kuandaa wahitimu wenye ujuzi wa kisasa, uwezo wa kujiajiri na umahiri katika masuala kama elimu ya fedha na akili mnemba.
Katika upande wa miundombinu, amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh15 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi, jengo la sayansi, maabara ya fizikia yenye kituo cha hali ya hewa na jengo la midia anuwai na elimu maalumu.
“Tumepokea pia Sh15 bilioni nyingine kwa ajili ya ujenzi wa majengo mengine matatu na kufanya jumla ya fedha za maendeleo kufikia zaidi ya Sh30 bilioni,” amesema profesa huyo.
Akizungumzia ujenzi wa hosteli mpya, amesema utasaidia kupunguza changamoto ya malazi kwa wanafunzi.
Mkuu wa Kitengo cha Tehama chuoni hapo, Sebastian Majimoto amesema kupitia mradi wa HEET, chuo kimeanzisha studio ya kisasa ya kutengeneza maudhui ya kujifunzia kwa njia ya mtandao na kupata vifaa vya kuimarisha usalama wa mifumo.
“Hii inatupa uwezo wa kutoa elimu kwa njia ya kidijitali kwa wanafunzi walioko sehemu mbalimbali duniani,” amesema Majimoto.
Katika eneo la rasilimali watu, amesema watumishi 31 wa MUCE wamefadhiliwa kusoma shahada za uzamili na uzamivu katika vyuo vya kimataifa, huku wengine wakipatiwa mafunzo ya muda mfupi kuhusu ufundishaji wa kidijitali, masuala ya kijinsia na elimu jumuishi.
Mmoja wa wanufaika, Dk Baraka Luvanga amesema; “Nchi haiwezi kukua bila kuwekeza kwenye elimu ya juu. Kupitia HEET, nimepata fursa ya kusoma hadi ngazi ya uzamivu na sasa narudi kutoa mchango wangu kwa Taifa.”
Katika kukuza elimu jumuishi, MUCE limeanzisha Kitengo cha Mahitaji Maalum na dawati la masuala ya kijinsia vinavyosimamia huduma kwa wanafunzi wenye ulemavu wa uoni, usikivu na viungo.
Mkuu wa kitengo hicho, Joseph Paul amesema wanafunzi watapimwa ili kubaini mahitaji yao na kupatiwa vifaa maalumu kama kompyuta mpakato, kishkwambi au vifaa vya usaidizi wa usikivu.
Naye rais wa serikali ya wanafunzi wa MUCE, Musa Mgema ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa huo akisema utaboresha mazingira ya kujifunzia. “Hosteli hizi zitatupunguzia gharama na muda wa kutembea umbali mrefu kufika madarasani,” amesema.