Mwalimu Nyerere alivyolinda tunu za amani, umoja wa kitaifa

Dar es Salaam. Amani na umoja ni tunu zilizosimamiwa kwa nguvu kubwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiamini kwamba umoja ndiyo nguvu ya mnyonge na amani ndiyo nguzo ya maendeleo.

Leo ni miaka 26 tangu Nyerere alipofariki dunia, Oktoba 14, 1999, huku akiliacha Taifa likiwa na amani na umoja licha ya kupita katika vipindi tofauti vya viongozi wenye maono na mitindo tofauti ya uongozi.

Sasa Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu, Oktoba 29, 2025, huku nguzo kuu za amani na umoja zikitikiswa na watu wenye mitazamo tofauti kuhusu uchaguzi ujao, wakiamini muundo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na mazingira ya uchaguzi hayatoshi kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

Katika kipindi hiki cha kampeni na maandalizi ya uchaguzi, fikra na falsafa za Mwalimu Nyerere zinabaki kuwa dira ya Taifa, zikikumbusha Watanzania kuwa amani na umoja si zawadi bali ni matokeo ya misingi madhubuti ya kitaifa.

Uimara wa nyumba ni msingi wake, kwa hakika uimara wa Tanzania umetokana na misingi hiyo aliyoiweka tangu wakati wa kupigania uhuru na hata baada ya uhuru, huku akiweka misingi imara ya kulinda amani na umoja wa Watanzania.

Umoja wa kitaifa, siasa zisizo na ukabila wala udini, utawala wa sheria, maadili ya uongozi, elimu ya uraia, amani na utulivu, pamoja na dhana ya maslahi ya Taifa kwanza, ndizo nguzo kuu zilizoshikilia amani hata miaka 26 baada ya kifo chake.

Mwalimu Nyerere aliamini kuwa Taifa haliwezi kusimama bila umoja. Alikataa siasa za chuki na ubaguzi wa kidini au kikabila.

Katika hotuba yake ya mwaka 1965 alisema: “Sisi hatutaki siasa za kugawanya watu. Tunataka uchaguzi uwe chombo cha mshikamano, siyo chanzo cha chuki.”

Ujumbe huu bado unaishi. Wakati wa uchaguzi, wanasiasa na wananchi wanaendelea kuhimizwa kushikamana, kujadili hoja na si kufarakana. Umoja huo umeifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani barani Afrika.

Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Mwalimu alisisitiza: “Vyama vingi visitugawanye. Vyote vishindane kwa sera, lakini Taifa lisalie moja.” Msingi huo umeendelea kudhibiti sumu ya siasa za ukabila.

Mchambuzi wa siasa, Dk Paul Loisulie, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), anasema Nyerere alikuwa na upeo mpana wa kisiasa uliolenga umoja kuliko madaraka.

Anasema alitambua kuwa ukabila na udini ni sumu ya Taifa, ndiyo maana alijenga siasa za utambulisho wa uraia badala ya asili ya mtu.

“Hakuwa kiongozi wa maneno, alikuwa mtu wa vitendo. Alijenga misingi ya Taifa lenye utambulisho mmoja Watanzania. Hii ndiyo sababu mpaka leo hatuna migogoro ya kikabila kama nchi nyingine za Afrika,” anasema Dk Loisulie.

Anaongeza kuwa urithi huo wa siasa zisizo na ubaguzi umefanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa barani.

Kiswahili ni alama ya urithi wa Nyerere. Alikitumia kama silaha ya kuunganisha Taifa na kuvunja mipaka ya kikabila. Alipohutubia kongamano la Kiswahili la Kimataifa mwaka 1974, aliweka wazi nia yake ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa.

“Kiswahili ni lugha ya umoja, ni chombo cha kuunganisha na kuelimisha wananchi,” anasema mwanazuoni huyo.

Leo, Kiswahili kimekuwa lugha ya utambulisho wa Watanzania duniani kote na kimeendelea kuwa alama ya urithi wa Mwalimu Nyerere. Kwa kutumia lugha moja, Taifa limekuwa na utambulisho mmoja wa Waswahili wa Tanzania.

Kwa upande wa demokrasia ya watu na ushirikishwaji, Mwalimu Nyerere aliweka msingi wa Serikali ya wananchi kama chombo cha umoja na amani ya Taifa katika uchaguzi.

Katika hotuba yake ya mwaka 1961 alisema wazi: “Serikali ni ya watu na kwa ajili ya watu.” Alianzisha mifumo ya ushirikishwaji kuanzia vijijini hadi ngazi ya Taifa ili wananchi washiriki katika uamuzi unaowahusu.

Mwalimu Nyerere aliamini katika usawa wa wote mbele ya sheria. Alisisitiza kuwa hakuna aliye juu ya sheria, hata viongozi, katika muktadha wa kulinda amani ya nchi.

Dk Onesmo Kyauke, wakili na mchambuzi wa masuala ya uongozi, anasema Nyerere aliweka msingi wa utawala unaojali haki na uwajibikaji.

“Mwalimu Nyerere aliweka misingi ya kuheshimu taasisi, alijenga heshima kwa Mahakama na Bunge kama mihimili huru, na hata alipokuwa madarakani hakujiona kuwa juu ya sheria. Hili linaendelea kuwa somo kubwa kwa viongozi wa sasa,” anasema Dk Kyauke.

Anaongeza kuwa uongozi wa Nyerere uliimarisha imani ya wananchi kwa Serikali yao kwa sababu aliweka uwiano kati ya nguvu ya dola na haki za binadamu.

Maadili ya uongozi yalikuwa moyo wa falsafa ya Mwalimu Nyerere. Katika Azimio la Arusha alisema: “Viongozi ni watumishi wa wananchi; wanapaswa kuwa na maadili ya juu.”

Alipiga vita rushwa, ufisadi na tamaa ya madaraka bila kupepesa macho. Uadilifu wake ulifanya hata wapinzani wake wamheshimu.

Dk Loisulie anasema Nyerere aliongoza kwa mfano, hivyo kujenga misingi ya umoja na amani kwa Taifa.

“Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa kipekee ambaye hakuogopa kukemea uovu ili kulinda misingi ya uadilifu. Alitaka viongozi wawe mfano wa nidhamu na uwajibikaji,” anasema Dk Loisulie.

Mwanazuoni huyo anaongeza kuwa leo Taifa likikumbuka misingi hiyo, linapaswa kujitazama upya katika vita dhidi ya rushwa na tamaa ya madaraka, kwani hayo ndiyo yalikuwa maadui wa amani na umoja wa Taifa kwa mtazamo wa Mwalimu.

Msisitizo wa amani na utulivu

Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa “amani haina mbadala”. Aliamini kuwa amani ndiyo tunu kubwa ya Taifa ili liendelee.

Aliamini kuwa maendeleo hayawezekani bila amani. Kutokana na msingi huu, hata wakati mataifa mengine yakipita kwenye machafuko, Tanzania imeendelea kuwa salama kwa misingi hii.

Baba wa Taifa aliwahi kusema: “Taifa ambalo watu wake hawana amani, wakisikia mtu amegonga mlango wanahisi amekuja kuwakamata, hilo Taifa hauwezi kusema lina maendeleo.” Alisisitiza akionesha mtazamo wake kuhusu amani.

Hakuridhika na uhuru wa ndani pekee, aliamini kuwa uhuru wa Tanzania pekee, wakati mataifa jirani yakiteseka na unyonyaji na uonevu, hautoshi. Alisaidia ukombozi wa mataifa mengine, yakiwemo yale ya kusini mwa Afrika.

“Aliamini kuwa siasa bila amani ni sumu, hivyo alijenga taasisi zenye misingi ya majadiliano badala ya mapambano. Hata wakati wa tofauti za kisiasa, Mwalimu Nyerere aliamini katika mazungumzo kuliko migogoro,” anasema Dk Kyauke.

Anaongeza kuwa amani ndiyo msingi wa uwekezaji na maendeleo ya kijamii, akitoa wito kwa jamii na viongozi kuenzi fikra za Mwalimu ili kudumisha amani kwa maridhiano na misingi ya utawala bora.

Mwalimu Nyerere aliweka kipaumbele kwa elimu yenye maadili na maarifa ya uraia. Alisisitiza kuwa elimu inapaswa kuwakomboa wanaoipata na kutumika kama silaha ya kutatua matatizo ya jamii na kuunganisha Taifa.

Aliwahi kusema: “Elimu ni haki ya kila Mtanzania; inapaswa kuwa na manufaa kwa wote na haipaswi kuwa bidhaa ya kuuzwa.” Hii inaonesha kuwa Nyerere aliona elimu kama daraja la ukombozi.

Dk Kyauke anasema: “Mwalimu aliona elimu kama silaha ya kuleta haki na usawa. Hakuwa anazungumzia tu elimu ya darasani, bali elimu ya uelewa wa wajibu na haki. Alisisitiza elimu ya ukombozi na kujitegemea. Mwalimu alitaka wasomi wawe chachu ya maendeleo, si wanyonyaji wa jamii. Hili ndilo tunapaswa kulirudisha leo.”