Pemba. Changamoto ya upatikanaji wa mafao ya wastaafu kwa wakati, imeibua ajenda kwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT – Wazalendo, Othman Masoud Othman aliyewaahidi Wazanzibari kulivalia njuga suala hilo, ili haki ipatikane.
Othman Ametoa ahadi hiyo leo Jumanne Oktoba 14, 2025 akizungumza na wazee na wakazi wa jimbo la Kiwani Sokoni, Wilaya ya Mkoani visiwani Pemba, katika utaratibu wake wa kukutana na makundi ya watu, kabla ya kufanya mkutano wa hadhara katika mwendelezo wa kampeni zake za kusaka kura.
Katika kulivalia njuga suala hilo, Othman amesema akishika usukani wa kuiongoza Zanzibar Oktoba 29, Serikali atakayoiunda itapitia upya mfumo mzima wa mafao ya wastaafu Serikalini ili kuhakikisha wastaafu wanapewa heshima.
Amefafanua kuwa dhumuni la kushughulikia kero hiyo ni kuhakikisha pia wastaafu hao wanapata thamani na haki zao za msingi kwa mujibu wa mchango wao katika kuitumikia Zanzibar wakati wa utumishi wao.
“Hali ya wastaafu kwa sasa ni ya kusikitisha, wengi wao wametelekezwa, kudharauliwa na wanateseka licha ya kufanya kazi kwa uaminifu na bidii kubwa kwa miaka mingi,” amesema na kuongeza;
“Wastaafu wamefanya kazi kubwa kwa moyo wa uzalendo, lakini leo hawathaminiwi. Serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha kila mstaafu anapewa thamani anayostahili ili jasho lao linawanufaisha na familia zao,” amesema Othman.
Amefafanua kuwa mfumo wa sasa wa hifadhi ya jamii, hususan kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), umekuwa na usumbufu kwa wastaafu hao, badala ya kuwa suluhisho la maisha baada ya kustaafu.
“Kikotoo kinachotumika kuwalipa wastaafu hakiendani kabisa na hali halisi ya maisha. Niwaahidi tutapitia upya kanuni, mifumo ya kikotoo na utaratibu wa mafao kwa lengo la kurejesha imani kwa watumishi wa umma wanaokaribia kustaafu.
“Lazima haki, utu, na heshima ya mstaafu vilindwe kwa nguvu zote. Serikali ya ACT – Wazalendo itahakikisha wastaafu wanashirikishwa moja kwa moja katika uamuzi unaohusu maslahi yao ili kuwepo kwa mfumo wa malipo wa haraka utakaozingatia haki na thamani halisi ya mchango wa kila mtu,” amesema.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kanza wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo, amesema Serikali atakayoiongoza haitapenda kuona kuona mzee anahangaika kupata haki yake ya msingi, kwa sababu wastaafu ni nguzo muhimu ya Taifa lazima kuheshimiwe na kuenziwa.
Vuai Said Vuai ambaye ni mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) amesema; “nimelipwa nusu miaka na miaka mengine sijalipwa, naomba utusaidie mheshimiwa mgombea endapo ukishika madaraka tulipwe fedha zetu.”
Mkazi mwingine wa Kiwani, Ramadhan Makame Kombo amesema watumishi wakistaafu wanapatia wakati mgumu katika kupata mafao yao kwa wakati, licha ya kuitumikia Serikali.