Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema masuala yote aliyoahidi Wazanzibari ikiwemo ajira, majibu yatapatikana ndani ya muda mfupi kabla hawajamuuliza utekelezaji wake.
Ahadi nyingine ambazo Othman amekuwa akiziahidi katika mikutano yake ya kampeni visiwani humo ni pamoja na masilahi bora kwa wafanyakazi, uwezeshaji, katiba mpya, kurejesha heshima kwa wananchi na nchi.
“Hilo ni deni nalibeba, kama kiongozi, kama mgombea urais, Inshallah mtakuja kuniuliza, ila naamini kabla ya kuniuliza mtaona majibu kwanza. Mtatangulia kuyaona majibu kwanza…,” amesema Othman.
Othman ameeleza hayo leo Jumanne Oktoba 14, 2025 alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mwambe, Jimbo la Kiwani Mkoa wa Kusini Pemba katika mwendelezo wa kampeni za kusaka kura.
Amefafanua kuwa wajibu wa kiongozi ni kuwatumikia na kuwatimizia mahitaji yao ikiwemo haki, akisisitiza ahadi hizo amezibeba na akifanikiwa kushinda uchaguzi atakwenda kuzitimiza, kabla ya Wazanzibari hawajamuuliza.
Katika mkutano huo, Othman amewaahidi wananchi wa Kiwani wanaojishughulisha na ufugaji kuwa Serikali atakayoiunda itawawezesha ikiwemo kuwapa maarifa, mbegu bora na madaktari wa mifugo ili kufuga kwa tija.
“Hii ndio kazi ya Serikali, tukiweza kuyafanya haya hakuna mtu atakayeweza kuwa maskini.
Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa kwa sababu Zanzibar inahitaji mabadiliko ya kiuongozi ili kusonga mbele katika hatua za maendeleo.
Jussa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, amewataka Wazanzibari kuiga mfano wa mataifa mengi ya Afrika yaliyofanya mabadiliko ya viongozi wao kwa njia ya chaguzi.
“Ndugu zangu upepo unakuja, tukijaaliwa Oktoba 29 tunakwenda kuing’oa Serikali ya CCM na kumweka Othman Masoud Othman ili akainyooshe Zanzibar.
“Zanzibar inakwenda katika mkondo huo na mabadiliko ya uongozi katika uchaguzi wa Oktoba 29 yataanzia hapa Kiwani kisha maeneo mengi ili kuwapa fundisho,” amesema Jussa.