Polisi alivyouawa kwa kupigwa mshale nje ya lango la Ikulu

Nairobi. Ni tukio linaloibua maswali nchini Kenya, baada ya mshukiwa aliyekuwa amejihami kwa upinde na mshale, kumshambulia Ofisa wa Polisi, Ramadhan Mattanka nje ya lango la Ikulu jijini Nairobi na kusababisha kifo chake.

Maswali hayo yanaibuka kutokana na ukweli kuwa Ikulu ni moja kati ya maeneo yenye ulinzi mkali zaidi nchini Kenya, kama ilivyo katika nchi nyingi duniani. Mbali na hilo pia maeneo yote ya karibu na Ikulu huwa na Polisi waliojihami kwa silaha.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Polisi nchini Kenya (NPS) jana Oktoba 13,2025 kupitia akaunti yake ya X, mtuhumiwa  alimshambulia Ofisa huyo saa 2:10 asubuhi ya jana akiwa lango la Ikulu namba D.

State House

A section of State House Nairobi. There have been a number of security breaches at the president’s official residence over the years. 

Photo credit: Dennis Onsongo | Nation Media Group

Kulingana na taarifa  iliyotiwa saini na Msemaji wa NPS, Muchiri Nyaga, mshukiwa huyo ambaye baadaye alitambuliwa kuwa ni Kinyuka Kimunyi (56), alitiwa mbaroni na maofisa wengine wa Polisi waliokuwa na marehemu.

Inaelezwa Mattanka ambaye ni Konstebo wa Polisi alikuwa kitengo cha General Service Unit (GSU) na baada ya kushambuliwa kwa mshale aliwahishwa Hospitali ya Taifa ya Kenyata (KNH) lakini alipoteza maisha akipatiwa matibabu.

Nyaga alieleza kuwa mshukiwa huyo akiwa na upinde na mshale, aliwasogelea polisi waliokuwa eneo hilo kwa haraka na licha ya kutakiwa kujisalimisha, hakufanya hivyo na badala yake alimfuata Mattanka na kumchoma mshale.

“NPS inalaani kitendo hiki kiovu na inawapongeza maofisa wa Polisi waliokuwepo eneo hilo kwa kuchukua hatua ya haraka, ambayo ilizuia madhara zaidi. Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha shambulio hilo,”imeeleza taarifa  ya Polisi.

Gazeti la Taifa Leo linalomilikiwa na Kampuni ya Nation Media Group (NMG), limemnukuu  Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Uhalifu (DCIO) wa Kilimani, Mahat Hassan akisema kuwa Kimunyi alikuwa akitembea karibu na Ikulu.

Hapo ndipo Mattanka akamkaribia mshukiwa huyo na ndipo alipopigwa mshale lakini ripoti ya Kituo cha Polisi cha Kilimani ilieleza kuwa Kimunyi aliwaendea maofisa wanaolinda lango la kuingia Ikulu waliokuwa wakiyakagua magari mawili.

State house man killer

Kithuka Kimunyi, a man suspected of killing a GSU officer, is help on October 13, 2025 at Kilimani Police Station.

Photo credit: Billy Ogada | Nation Media Group

“Alitoa mshale na kumdunga kwenye kifua upande wa kushoto na kumwacha akitokwa na damu nyingi.Akafikishwa KNH ambako aliaga dunia eneo la kuwapokea wagonjwa mahututi,” ilieleza ripoti ya Ofisa wa GSU, Daniel Kemboi.

Gazeti la Daily Nation limeandika kuwa saa chache baada ya kifo cha Ofisa huyo wa Polisi, vyanzo mbalimbali vikiegemea kamera za CCTV, zinashawishi kuwa Ofisa huyo na muuaji wake walikuwa wakifahamiana vizuri.

Kulingana na taarifa ya gazeti hilo, kwa dakika takribani 17, wawili hao walionekana wakiwa katika mazungumzo kwenye eneo la ukaguzi lango namba D la Ikulu, ambalo ni maalumu kwa watumishi wa Ofisi ya Rais na wageni.

Vyombo vya uchunguzi vinachunguza ilikuwaje Kimunyi akasogelea karibu na lango hilo ambalo ni  watumishi wa Ikulu na wageni waalikwa ndiyo wanaruhusiwa kufika, na hii ndio inajenga nadharia pengine walikuwa wakifahamiana.

CCTV zinazochunguzwa na zinaweza zisionyeshe nini walichokuwa wakizungumza lakini nadharia zinashawishi kuwa pengine walikuwa wanafahamiana, na kuna kitu ambacho hakikwenda vizuri baina ya wawili hao kabla au wakati wakijadiliana.

State house man killer

Kithuka Kimunyi, a man suspected of killing a GSU officer, is help on October 13, 2025 at Kilimani Police Station.

Photo credit: Billy Ogada | Nation Media Group

Kulingana na gazeti hilo, nadharia hizo zinapata nguvu kwa kuwa katika uchunguzi wa awali wa simu ya marehemu, inaonyesha siku za nyuma waliwahi kuwasiliana na kukutana na Kimunyi nje ya lango ambalo marehemu alipangwa zamu.