Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji nchini imewaondoa raia wawili wa kigeni waliobainika kukiuka masharti ya viza zao za matembezi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 14, 2025 na Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle, wageni hao walioondolewa jana, Oktoba 13, 2025, ni Dk Brinkel Stefanie, raia wa Ujerumani mwenye hati ya kusafiria namba C475MMNGL na Catherine Janel Almquist Kinokfu, raia wa Marekani mwenye hati ya kusafiria namba A80321764.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, hatua ya kuwaondoa nchini imechukuliwa baada ya kubainika walikiuka masharti ya viza zao za matembezi, jambo lililo kinyume cha taratibu zilizowekwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 pamoja na kanuni zake.
Idara ya Uhamiaji imewataka raia wa kigeni wanaoingia na kuishi nchini kuhakikisha wanazingatia masharti yaliyoainishwa katika viza au vibali vyao vya ukaazi, ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza pindi wanapokiuka sheria.
“Tunatoa wito kwa raia wa kigeni kuzingatia matakwa ya viza zao kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu wowote,” amesema Mselle katika taarifa hiyo.
Idara ya Uhamiaji imesisitiza kuwa, itaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya wageni nchini na kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika kukiuka sheria za uhamiaji.
Lissu aliwataja mahakamani
Wakati Uhamiaji ikichukua hatua hiyo, wageni hao walitajwa kwa majina yao na Tundu Lissu, akieleza waliingia nchini kufuatilia mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Oktoba 6, 2025, kabla ya kuanza usikilizwaji wa kesi, Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliieleza Mahakama kuwa Agosti 30, 2025, Naibu Msajili, Livin Lyakinana alimwandikia barua kupitia kwa Mkuu wa Gereza aliyokabidhiwa Oktoba 2, 2025.
Alidai kuwa, barua hiyo ilimwelekeza awasilishe orodha ya watu 100 ambao angependa wahudhurie kesi hiyo na alielekeza majina hayo yamfikie Naibu Msajili Oktoba 3, 2025 kabla ya saa 12:00 jioni.
Lissu alidai kuwa, orodha hiyo ni ya mawakili, viongozi wa chama na ndugu zake na kwamba, aliorodhesha majina hayo na kuyawasilisha kwa muda uliotakiwa.
Hata hivyo, alidai siku hiyo kati ya watu aliowaandika kama ndugu zake walizuiwa kuingia na kwamba alimuona mwenyewe akizuiwa getini.
Alimtaja mtu huyo ambaye katika orodha ya ndugu zake jina lake ni la 12 kuwa Dk Brinkel Stefanie, ambaye ametoka Ujerumani kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.
Pia, alimtaja mwingine aliyedai kuzuiwa kuingia mahakamani ni Almquist Kinokf, kutoka Marekani.
Akijibu malalamiko ya Lissu, kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji Dunstan Ndunguru alisema Mahakama ilishatoa utaratibu wa uhudhuriaji wa kesi hiyo na kwamba watu hawazuiwi lakini wanapaswa kufuata utaratibu uliowekwa.
Hata hivyo, Jaji Ndunguru alisema watafuatilia malalamiko ya kuzuiwa kwa watu aliowaorodhesha.
Oktoba 7, 2025 Jaji Ndunguru alimweleza Lissu kuwa, wamemwelekeza Msajili kufuatilia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuhakiki majina ya watu walioorodheshwa kwenye orodha, wanaopaswa kuruhusiwa kuingia mahakamani kufuatilia kesi.
Oktoba 8, 2025, Lissu alikumbushia suala hilo, akidai Dk Stefanie amezuiwa na maofisa Uhamiaji, akiieleza Mahakama kuwa amemtaka asiondoke nchini bali aendelee kuwepo mpaka muafaka ujulikane.
Jaji Ndunguru alimjibu Lissu kuwa wamearifiwa kuna mtu anaitwa Heche analifuatilia, lakini akamuahidi Lissu kuwa, watalifuatilia zaidi ili kupata taarifa sahihi.
Siku iliyofuata, Oktoba 9, 2025, Jaji Ndunguru alimjulisha Lissu kuwa amefuatilia kwa Msajili ameelezwa kuna masuala ya kiuhamiaji ambayo maofisa Uhamiaji wanahitaji kujiridhisha.
Jaji Ndunguru alieleza alijulishwa kuna nyaraka ambazo mgeni wake huyo anatakiwa kuzipeleka Uhamiaji au mtu anaitwa Golugwa, kisha ataruhusiwa kuingia mahakamani.
Lissu alisema hao si wageni wa chama (Chadema) bali ni wageni wake, hivyo viongozi wa chama hawawezi kufuatilia suala lao kwa kuwa hawawajui.
Badala yake, Lissu alipendekeza ndugu zake ndio wafuatilie suala hilo Uhamiaji, akisisitiza kuwa, hawataondoka nchini bali wataendelea kusubiri mpaka mwisho. Pendekezo hilo Jaji Ndunguru alisema hawana tatizo nalo.