Rais wa Madagascar athibitisha kujificha baada ya jaribio la kupinduliwa

Dar es Salaam. Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina amesema alilazimika kuondoka nchini humo na kujificha katika eneo salama baada ya kile alichokiita jaribio la kumpindua lililopangwa na wanajeshi na wanasiasa.

Katika hotuba yake ya usiku wa jana, Oktoba 13, 2025, iliyorushwa kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook nchini humo, Rajoelina amekiri kuwa maisha yake yapo hatarini, akisisitiza kwamba hatang’atuka madarakani.

Katika hotuba hiyo, Rajoelina ambaye alichaguliwa tena mwaka 2023 katika uchaguzi uliosusiwa na upinzani, alijibu kwa kusema kulikuwa na kile alichokiita ‘jaribio haramu la kuchukua madaraka’ na akatangaza kuwa ameondoka nchini kwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, hakufafanua ni wapi alipojificha.

“Wamalagasy, familia yangu, njia pekee ya kutoka katika hali hii ni kuheshimu katiba ya nchi. Tukivuka mipaka hiyo, tutazama katika umaskini mkubwa na taifa letu litapoteza mwelekeo,” Rais huyo alisema akifutilia mbali wito wa kujiuzulu ulilotolewa na vuguvugu la maandamano la Gen Z.

Hata hivyo, duru za kimataifa zinaonyesha kuwa hali ya kurejea kwake bado ni tete kufuatia kikosi cha jeshi cha CAPSAT ambacho kilimsaidia kuingia madarakani mwaka 2009, sasa kimegeuka kuwa tishio kwake.

Inaelezwa kuwa, Kamanda wake, Kanali Michael Randrianirina, amesema jeshi limeamua kusimama upande wa wananchi, lakini amekanusha kuwa kinachoendelea nchini humo si mapinduzi ya kijeshi, akisema hatima ya nchi iko mikononi mwa wananchi.

Hayo yamejiri baada ya maandamano ya nchi nzima, yakiongozwa na vijana, yenye lengo la kumuondoa madarakani kufuatia jaribio lililofeli la Rajoelina kuwatuliza waandamanaji hao vijana ‘Gen Z Mada’,  hatua iliyomfanya baraza lote la mawaziri na kufanya makubaliano mengine bila mafanikio.

Hotuba yake ya jana kwa taifa ilicheleweshwa mara kadhaa huku kukiwa na machafuko ya maandamano yaliyoripotiwa na vyanzo vya kimataifa kusababisha vifo zaidi ya watu 20 na kujeruhi zaidi ya 100, huku serikali ikikanusha na kuthibitisha vifo 12 pekee.

Rais Rajoelina, jana, aliripotiwa kutoweka nchini humo huku taarifa zikisema aliondoka kwa ndege ya kijeshi na kupelekwa Ufaransa chini ya makubaliano na Rais wa taifa hilo, Emmanuel Macron.

Kwa wiki kadhaa, taifa hilo la kisiwa katika Bahari ya Hindi, limekumbwa na maandamano makubwa yanayoongozwa na vijana wa kizazi cha Gen Z, waliotajwa kuwa chanzo kikuu cha wimbi jipya la upinzani.

Waandamanaji wamekuwa wakilalamikia kukatikakatika kwa maji na umeme, hali ngumu ya kiuchumi, gharama kubwa za maisha na tuhuma za ufisadi serikalini ambapo Jumamosi iliyopita, hali ilizidi kuwa tete baada ya kikosi maalumu cha jeshi, CAPSAT, kujiunga na waandamanaji na kutoa wito kwa rais kujiuzulu.

Katika hotuba yake ambayo ilicheleweshwa mara kadhaa baada ya wanajeshi kudaiwa kuteka kituo cha matangazo ya taifa, rais huyo amesema: “Baadhi ya marais wa Afrika walijitolea kutuma wanajeshi kuleta amani Madagascar. Nililikataa hilo kwa sababu halilingani na maadili yetu ya Kimalagasy. Kwa sababu hiyo, nililazimika kwenda katika eneo salama kulinda maisha yangu,” alisema Rajoelina katika hotuba yake.

Hii ni mara ya pili kwa Rajoelina kukabiliwa na shinikizo kubwa la kisiasa tangu aliposhika madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2009 kufuatia mapinduzi yaliyomuondoa madarakani mtangulizi wake, Marc Ravalomanana. Wengi nchini humo wanasema historia inajirudia.

Hadi sasa, hali ya usalama imebaki kuwa tete katika mji mkuu wa Antananarivo huku magari ya kivita yakiendelea kuzunguka maeneo nyeti ya serikali, huku wananchi wakihimizwa kubaki majumbani.

Inaelezwa kuwa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wameitaka serikali na jeshi kurejea kwenye wajibu wa kikatiba na kuhakikisha mgogoro unatatuliwa kwa njia ya mazungumzo.