Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thadeus Ruwa’ichi, amezungumzia uchaguzi wa haki, wa ukweli, wa uhuru na wa kuaminika, huku akieleza kusikitishwa na hali inayoendelea ya kupotea na kutekwa watu.
Askofu Ruwa’ichi, ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), amesema hayo leo Jumanne, Oktoba 14, 2025, katika adhimisho la misa takatifu ya Uwaka kutegemeza Masista wa Dada Wadogo wa Mtakatifu Fransisko wa Asizi, Visiga, Dar es Salaam.
Amesema kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, wanawaomba raia wote kuongozwa na dhamiri safi, iliyohai na yenye kuongozwa na ukweli halisi unaozingatia hofu ya Mungu, utu wa mtu, historia nzuri ya Taifa, umoja na mshikamano.
“Mpigakura na mpigiwa kura mnaalikwa kuheshimu dhamiri juu ya suala hili la uchaguzi mkuu, usirubuniwe kwa vitisho wala kwa rushwa, usirubuniwe kwa namna yoyote ile,” amesema.
Vilevile, ameiomba Serikali na wenye mawazo tofauti kuhusu masuala ya uchaguzi, waongozwe na utamaduni wa kuwa na mazungumzo katika kutekeleza haki msingi za kisiasa kadri ya Ibara ya 21 ya Katiba ya nchi, ambapo kila raia ana haki hizo.
“Wanasiasa kupitia vyama na Serikali, kaeni mzungumze. Wahakikishieni watu haki zao, nguvu ya wananchi iko kwenye hoja, siyo kwenye mabavu na hila. Serikali kupuuza wanaolalamika si afya wala tija kwa Taifa letu,” amesema na kuongeza:
“Wakati uliokubalika kuzungumza ni sasa na wala hamjachelewa. Hatuchelewi kujisahihisha wala kutenda mema. Naiomba Serikali iwasikilize raia wenye malalamiko ya haki zao za kisiasa. Unyenyekevu mbele ya raia hujengeka kwenye ukweli na uwazi.”
Amesema, “Kiongozi wa watu akiwa mnyenyekevu na mkweli anaaminika na watu wote. Tukumbuke kuwa historia ya uchaguzi katika nchi yetu, kuanzia mwaka 1962 mpaka 2015, zilithibitika na ziliaminika, na viongozi wakapatikana kutokana na chaguzi hizo hata kama zilikuwa na mapungufu yake.”
“Ninawatakieni uchaguzi wa haki, wa ukweli, wa uhuru na wa kuaminika mwaka huu wa 2025,” amesema.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema tukio la uchaguzi mkuu ni la kikatiba, kwani hapo ndipo wananchi hutegemewa kuwapa waliowachagua dhamana ya kutawala na kuongoza nchi.
Amesema Ibara ya 8 ya Katiba ya nchi inaweka wazi kuwa mamlaka ya nchi yamo chini ya wananchi, na Serikali huwajibika kwa wananchi ikiwa na wajibu wa kulea na kuleta ustawi wa watu wote bila ubaguzi.
“Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ambayo ninaiongoza, kwa kulitazama tukio la uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025, inasikitishwa na hali inayoendelea bila kusitishwa ya kupotea na kutekwa watu,” amesema na kuongeza:
“Utekaji huu unaonekana unaendeshwa kwa mpango wa kikundi maalumu kinachotekeleza uovu huu sehemu mbalimbali za nchi yetu.”
Amesema utekaji huo umesababisha kupotea kwa ulinzi wa haki ya uhai, ambayo ni haki ya msingi, akieleza: “Kwani hatusikii walioapa kulinda uhai wa Watanzania kulaani au kukomesha utekaji huu na kutoweka kwa watu.”
Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema ni takribani zaidi ya miaka miwili matukio hayo yamezidi kukithiri na kuwafanya Watanzania wajiulize iweje watekaji hao wawe na nguvu kuliko vyombo vya ulinzi wa watu na kuliko wale wenye mamlaka ya kuwaletea watu matumaini ya kuishi na ustawi wake.
“Dalili za kukomesha utekaji hazionekani, wala hatusikii kulaaniwa kwa matukio hayo. Ikumbukwe kuwa uhai wa kila mwanadamu unadhihirisha utukufu wa Mungu,” amesema.
Amesema mwanadamu ni kiumbe wa pekee ambaye hakuna mwenye haki au mamlaka ya kumuondolea uhai wake, akieleza kuwa kazi ya Serikali ni kulinda uhai wa kila mwanadamu.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania, kila mtu ana haki msingi ya uhai wake na kuhakikishiwa kuwa haki hii inalindwa kwa gharama zozote zile,” amesema na kuongeza kuwa wanaitaka Serikali kuwahakikishia raia na watu wote usalama wa haki ya uhai kwa kila mtu bila ubaguzi wowote.
“Uchaguzi mkuu una maana tu watu wanapopata viongozi wenye kulinda na wenye kutetea uhai. Wagombea wa vyama na vyama vyao, kwa mujibu wa Ibara ya 3 na 5, walipaswa kuonesha uwezo na moyo wa kuwashinda wauaji na watekaji,” amesema.
Mwenyekiti huyo amesema sheria zipo zinazoonesha jinsi ya kushughulikia wahalifu, akahoji kwa nini waliopotea na kutekwa hawapatikani mahabusu.
“Tunaitaka Serikali izingatie kanuni ya utawala wa sheria na kuheshimu kimatendo haki ya msingi ya kila mwanadamu.”