Dar es Salaam. Shilingi ya Tanzania imeibuka kuwa moja ya sarafu imara zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku wataalamu na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakieleza kwamba uthabiti wake unatokana na kupanda kwa bei ya dhahabu duniani pamoja na kuimarika kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
Bei ya dhahabu imepanda kufikia kiwango cha kihistoria, ikivuka Dola 4,000 kwa wakia moja (sawa na gramu 31.1) mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati wawekezaji duniani kote wakikimbilia katika bidhaa hiyo adimu kutokana na hali ya sintofahamu katika uchumi wa dunia na misukosuko ya kisiasa kimataifa.
Tangu mwanzo wa mwaka 2025, bei ya dhahabu imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 50, ongezeko ambalo wachambuzi wanalihusisha kwa sehemu na kurejea madarakani kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, mapema mwaka huu.
Thamani ya madini hayo iliongezeka kwa kasi Aprili, baada ya kurejea kwa mvutano wa kibiashara chini ya utawala wa Trump, na tena Agosti ilipanda zaidi baada ya Rais huyo kuikosoa hadharani Benki Kuu ya Marekani (Federal Reserve).
Vita vinavyoendelea Gaza na Ukraine navyo vimechochea zaidi hamasa ya wawekezaji kuelekeza fedha zao kwenye dhahabu kama kimbilio salama.
Hali hii imekuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania, ambayo ni mzalishaji wa saba kwa ukubwa wa dhahabu barani Afrika, baada ya Ghana, Afrika Kusini, Mali, Burkina Faso, Sudan na Guinea.
Taarifa za hivi karibuni za BoT zinaonesha kuwa mapato yatokanayo na mauzo ya dhahabu nje ya nchi yamevuka kiwango cha Dola bilioni 4 kwa mara ya kwanza katika historia, kwa mwaka ulioishia Agosti 2025.
Tanzania ilipata Dola bilioni 4.3 kutokana na mauzo ya dhahabu katika kipindi hicho, ikilinganishwa na Dola bilioni 3.2 mwaka uliotangulia, sawa na ongezeko la asilimia 37.5.
Hivyo, Shilingi ya Tanzania ilidhoofika kwa takribani asilimia sita dhidi ya Dola ya Marekani katika mwaka ulioishia Oktoba 13, 2025, ikilinganishwa na kushuka kwa asilimia 10 kwa shilingi ya Kenya katika kipindi hicho hicho. Shilingi ya Uganda ilipungua kwa takribani asilimia nne, jambo lililochangiwa zaidi na uwekezaji wa kigeni katika sekta ya mafuta nchini humo.
Kuhusu mwenendo huo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alisema bei na kiasi cha dhahabu kinachouzwa nje kimeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kwa mara ya kwanza, bei ya dhahabu imefikia Dola 4,063 kwa wakia moja, ikichochewa na ongezeko la mahitaji ya wawekezaji katika kipindi cha sintofahamu ya kiuchumi duniani.
“Kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu nje ya nchi kunasaidia kuongeza upatikanaji wa dola nchini Tanzania. Benki Kuu ya Tanzania inanunua dhahabu moja kwa moja kutoka kwa wachimbaji, ambao ama huuza kwa benki kuu au kuiuza nje, hivyo kusaidia kuongeza fedha za kigeni katika uchumi,” alisema Gavana Tutuba.
Alisema mahitaji ya bidhaa za kuagiza kutoka nje yamepungua kutokana na kuimarika kwa viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa kama vigae, vioo na samani, hivyo kupunguza utegemezi wa bidhaa za kigeni.
Tutuba pia alieleza athari chanya za sheria mpya inayowataka wananchi kufanya miamala yote ya ndani kwa kutumia shilingi ya Tanzania badala ya dola za Marekani.
“Sera hii imesaidia kuimarisha shilingi kwa sababu bidhaa na huduma za ndani sasa zinalipiwa kwa sarafu ya taifa, huku dola zikitumika tu katika biashara za nje,” alifafanua.
Mbali na dhahabu, sekta nyingine zimechangia katika kuimarika kwa sarafu. Sekta ya utalii, hasa Zanzibar na Arusha, imepata nafuu kubwa baada ya kuporomoka kutokana na janga la Uviko-19, huku mauzo ya mazao ya kilimo kama mahindi, maharage, mchele na karanga yakiendelea vizuri.
“Mauzo makubwa ya dhahabu, kupungua kwa uagizaji bidhaa kutoka nje, usimamizi makini wa sarafu, sheria zenye kuunga mkono uchumi na ongezeko la mauzo yasiyo ya jadi, yote yamechangia kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Tanzania,” alisema Gavana Tutuba.
Mchumi Christopher Makombe anakubaliana na Gavana, akisema nguvu ya shilingi inatokana na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni, usimamizi bora wa Serikali na misingi thabiti ya uchumi mpana.
“Mapato makubwa kutoka dhahabu, kilimo na utalii yameongeza upatikanaji wa dola.
“Wakati huohuo, kanuni zinazokataza matumizi ya dola katika miamala ya ndani zimewahamasisha watu na kampuni kubadilisha akiba zao kuwa shilingi, hivyo kupunguza shinikizo dhidi ya sarafu yetu,” anaongeza
Anaongeza kuwa maagizo ya Serikali yanayowataka wafanyabiashara wa dhahabu kuuza sehemu ya akiba yao kwa BoT yameongeza hifadhi ya fedha za kigeni na kuimarisha imani ya wawekezaji.
Kwa mtazamo mpana zaidi, Makombe anasema uthabiti wa uchumi wa Tanzania, unaooneshwa na mfumuko mdogo wa bei, ukuaji thabiti wa Pato la Taifa (GDP), na kupungua kwa nakisi ya mizania ya malipo ya nje, umeimarisha uimara wa shilingi.
“Mahitaji ya dola yamepungua baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa ya uagizaji bidhaa na kushuka kwa bei ya mafuta duniani, jambo lililopunguza gharama ya uagizaji na upungufu wa fedha za kigeni,” anaongeza.
Mchambuzi mwingine, Oscar Mkude, anabainisha kuwa ingawa shilingi ilikumbwa na kuyumba mwishoni mwa mwaka jana, hatua za BoT ziliisaidia kurejea katika hali ya utulivu.
“Awali ilikuwa vigumu kupata dola kupitia benki kutokana na kuwepo kwa soko la sambamba (parallel market), lakini kadri mapato kutoka utalii na dhahabu yalivyoongezeka katikati ya mwaka, upatikanaji wa fedha za kigeni uliboreka kwa kiasi kikubwa,” anasema.
Anaongeza kuwa misimu ya kilimo pia imechangia kuimarika kwa shilingi. Baada ya msimu wa mavuno, ongezeko la chakula nchini lilipunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje, huku sera ya BoT ya kuimarisha fedha mwanzoni mwa mwaka 2024 kwa kupandisha kiwango cha riba hadi asilimia 6 ikisaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha sarafu.
“Kupunguzwa kwa riba hadi asilimia 5.75 kulionesha mwelekeo wa sera laini zaidi,” anasema.
Mkude pia anaeleza kuwa sera ya BoT kuhusu akiba ya dhahabu, inayowataka wauzaji wa dhahabu kuweka asilimia 20 ya mapato yao katika benki kuu, inalenga kujenga akiba ya kimkakati.
“Kwa muda, BoT inapanga kukusanya dhahabu ya kutosha ili kuitumia kama mali ya fedha (monetary asset). Hii itaongeza uwezo wake wa kuingilia soko la fedha za kigeni endapo shilingi itaanza kudhoofika,” anasema.