Taifa Stars yachapwa tena, yamaliza dakika 540 bila ushindi

MABAO mawili yaliyofungwa Iran katika dakika 26 za kwanza, yametosha kuifanya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kushindwa kuambulia ushindi kwenye mechi sita mfululizo ilizocheza sawa na dakika 540.

Taifa Stars ambayo mara ya mwisho kupata ushindi ilikuwa Agosti 9, 2025 kwenye michuano ya CHAN 2024 hatua ya makundi ilipoichapa Madagascar mabao 2-1, leo Oktoba 14, 2025 imeambulia kipigo katika mechi ya kirafiki.

Kabla ya leo, Agosti 16, 2025, ilitoka 0-0 na Jamhuri ya Afrika ya Kati katika CHAN 2024, kisha Agosti 22, 2025 ikafungwa 1-0 na Morocco hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Septemba 5, 2025, Taifa Stars ilitoka 1-1 ugenini dhidi ya Congo, mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, kisha ikafungwa mara mbili mfululizo nyumbani mechi za kufuzu michuano hiyo kwa matokeo ya 1-0 dhidi ya Niger (Septemba 9, 2025) na Zambia (Oktoba 8, 2025). 

Katika mechi ya leo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Al-Rashid uliopo Dubai, United Arab Emirates, Iran imeshinda 2-0.

Amirhossein Hosseinzadeh alianza kuifungia Iran dakika ya 17 kwa penalti baada ya Ibrahim Bacca kufanya faulo eneo la hatari.

Dakika tisa baadae, Mohammad Mehdi Mohebi aliongeza bao la pili kwa Iran akimalizia vyema pasi ya Kasra Taheri.

Iran ilionekana kuwa hatari kila inapofika eneo la Stars hali iliyofanya kumaliza kipindi cha kwanza ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Katika kipindi cha pili kabla ya kuanza, Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu akiwatoa Charles M’mombwa, Feisal Salum na Israel Mwenda, wakaingia Abdul Suleiman Sopu, Morice Abraham na Lusajo Mwaikenda, huku kocha wa Iran, Amir Ghalenoei akimtoa mfungaji wa bao la pili, Mohammad Mehdi Mohebi na kuingia Alireza Jahanbakhsh.

Mabadiliko hayo na mengine kadhaa yaliyofanyika kipindi cha pili, hayakubadili ubao wa matokeo na mwisho wa mchezo Iran 2-0 Tanzania.

VIKOSI
TAIFA STARS: Yakoub Suleiman, Israel Mwenda, Pascal Msindo, Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto, Yahya Zayd, Tarryn Allarikhia, Novatus Dismas, Paul Peter, Charles M’mombwa na Feisal Salum

IRAN: Payam Niazmand, Danial Esmaeilifar, Shojae Khalilzadeh, Amin Hazbavi, Milad Mohammadi, Saman Ghoddos, Saeed Ezatolahi, Kasra Taheri, Amirhossein Hosseinzadeh, Mehdi Hashemnejad na Mohammad Mehdi Mohebi.