Tchiroma ajitangaza mshindi uchaguzi wa Rais Cameroon

Younde. Kufuatia uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 12, 2025, mgombea wa upinzani kutoka chama cha Front for National Rebirth (FNR), Issa Tchiroma  amejitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo, ingawa matokeo rasmi bado hayajatangazwa na Baraza la Katiba.

Mwanasiasa huyo amejitangaza kupitia   hotuba ya takriban dakika tano iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii leo Oktoba 14, 2025, Tchiroma, ambaye alikuwa msemaji wa serikali kwa zaidi ya miaka 20 na mshirika wa karibu wa Rais Paul Biya kwa muda mrefu.

Tchiroma amesema wananchi wamechagua mabadiliko, hivyo akimtaka kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 92 kukubali matokeo ya kweli ya kura.

“Watu wameamua na uamuzi wao lazima uheshimiwe,” amesema Tchiroma aliyasema hayo katika video iliyorekodiwa mjini kwake Garoua, kaskazini mwa Cameroon.

Hata hivyo, Serikali ya Cameroon imeonya kuwa matokeo yoyote hayatachukuliwa kuwa rasmi hadi Baraza la Katiba litakapoyatangaza. Kwa mujibu wa sheria, Baraza hilo lina hadi Oktoba 26, 2025 kutoa matokeo ya mwisho ya urais.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Paul Atanga Nji amewakumbusha wagombea kuwa kitendo cha kutangaza matokeo bila idhini ya Baraza la Katiba ni uhaini.

Tchiroma, ambaye aliwahi kuwa mshirika wa karibu wa Rais Biya na kushika nyadhifa kadhaa serikalini, alijiuzulu Juni 2025 na kujiunga na upinzani, hatua iliyoonekana kama changamoto kwa utawala wa Biya ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 43, akiwa ni kiongozi mzee zaidi duniani aliye madarakani.

Kampeni ya Tchiroma imevutia maelfu ya wafuasi hasa vijana na mashirika ya kiraia, pamoja na makundi kadhaa ya vyama vya upinzani vilivyoamua kumuunga mkono.

Wito kuheshimu demokrasia

Akizungumza kutoka mji wake wa nyumbani Garoua, Kaskazini mwa Cameroon, mbele ya bendera ya taifa, Tchiroma alizihimiza taasisi za serikali na jeshi kutambua matokeo ya kweli ya kura na kusimama upande wa wananchi.

“Msiache mtu yeyote awapotoshe kutoka jukumu lenu la kuwalinda watu,” amesema.

Ameongeza kuwa matokeo ya uchaguzi huu ni adhabu kwa utawala wa Biya na mwanzo wa enzi mpya kwa Cameroon.

Hadi kufikia jana jioni, Rais anayetetea kiti chake, Biya, mwenye umri wa miaka 92 na chama chake tawala, hawajatoa kauli yoyote rasmi kuhusu matamshi ya Tchiroma.

Wachambuzi wa siasa wanasema kitendo cha Tchiroma kujitangaza mshindi kinaweza kuchochea mivutano ya kisiasa katika taifa hilo la Afrika ya Kati lenye historia ya migawanyiko ya kisiasa na kikabila.

Imeandikwa na Mintamga Hunda