UCHAMBUZI WA MALOTO: Hizi zingekuwa agenda za Nyerere Uchaguzi Mkuu 2025

Kutoka Oktoba 14, 1999 hadi ilipofika jana, Oktoba 14, 2025, ilitimia miaka 26 bila Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Naikumbuka ile siku, mchana, aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa, alililiza taifa.

“Nasikitika kuwatangazia kwamba mpendwa wetu, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, amefariki dunia. Mwalimu ameaga dunia hii leo saa 4:30 asubuhi saa za Tanzania, katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, mjini London, ambako alikuwa amelazwa akipata matibabu ya kansa ya damu tangu Septemba 24, mwaka huu (1999),” alitangaza Rais Mkapa.

Ilikuwa siku nzito ajabu kwa Watanzania. Rais Mkapa, kulia kwake, akiwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Omar Ali Juma na kushoto akiwa Waziri Mkuu wakati huo, Fredrick Sumaye. Taifa lilizizima kwa majonzi.

Ni miaka 30 iliyotimia tangu Mwalimu Nyerere alipotoa hotuba ya kihistoria, kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, kuelekea Uchaguzi Mkuu 1995. Mwalimu aliwahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM, akiwataka wamchague mtu wa aina gani kwa ajili ya Watanzania.

Uchaguzi Mkuu 1995, ulikuwa wa mwisho Mwalimu Nyerere kuushuhudia na kuushiriki. Uchaguzi Mkuu 2025, ni wa sita kufanyika bila uwapo wa Mwalimu. Kipimo cha nini agenda za Mwalimu Nyerere Uchaguzi Mkuu 2025, kinapaswa kuwa Uchaguzi Mkuu 1995.

Je, mazingira ya mwaka 1995 yanaoana vipi na ya 2025? Ulinganifu au kukaribiana kwa mazingira ya kisiasa baina ya mwaka 1995 na 2025, kwa namna yoyote, ni karata inayotosha kubashiri na kupatia nini zingekuwa agenda za Mwalimu Uchaguzi Mkuu 2025, kama angebaki hai, na angekuwa na afya njema ya kimwili na kiakili.

Katika Mkutano Mkuu wa CCM 1995, hotuba ya Mwalimu Nyerere, iliipambanua agenda yake namba moja ya Uchaguzi Mkuu 1995 kuwa ilikuwa rushwa. Alitaka wana-CCM wamteue mgombea ambaye angekuwa na sifa za kukabiliana na rushwa.

“Mgombea mtakayemteua lazima tumtetee, wote tumtetee, lakini inatakiwa ukiulizwa swali, ‘huyu atatusaidia kupiga rushwa vita’, jibu litoke ndani ya roho yako, hapana hapa tu (mdomoni), kwamba ndiyo, anaweza,” alisema Mwalimu Nyerere.

Je, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, rushwa haipo Tanzania? Bila shaka ipo na pengine ni kubwa kuliko ilivyokuwa mwaka 1995. Nchi imekua, uchumi ni mkubwa, mapato ya Serikali ni makubwa, vyanzo vya fedha serikalini ni vingi. Ufafanuzi huo unatosheleza kutengeneza mtandao mpana wa rushwa, kuliko miaka 30 iliyopita.

Watanzania ni binadamu. Mifumo ya ukusanyaji mapato inasimamiwa na Watanzania, ambao hakuna malaika miongoni mwao. Mmomonyoko wa maadili ni mkubwa, uwepo wa watu waadilifu ni sawa na kuonekana kwa kakakuona. Rushwa ipo. Tena kubwa.

Mwalimu Nyerere angekuwa hai leo, mwenye afya njema ya akili na mwili, agenda yake ingekuwa rushwa. Angetaka kuona ilani za vyama vya siasa zimeweka mkazo suala la kupambana na rushwa. Angetamani wagombea wapaze sauti wakijinasibu kukabiliana na rushwa. Na kweli wafanane na maneno yao.

Agenda ya pili ni umaskini wa Watanzania. Mwaka 1995, Mwalimu Nyerere alitaka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, watambue kuwa Watanzania bado ni maskini, na wamteue mgombea ambaye angekuwa anatambua hali za maisha ya Watanzania.

Kutoka mwaka 1995 mpaka 2025, maendeleo ni makubwa. Hata hivyo, haina maana umaskini umeisha. Bado Watanzania wengi ni maskini. Mwalimu Nyerere alitaka Tanzania liwe taifa lisilo na matabaka ya kimaisha. Kwa maana hiyo, Uchaguzi Mkuu 2025, Mwalimu Nyerere angepigania uwezeshwaji zaidi kwa Watanzania maskini ili wapige hatua kimaisha.

Mwalimu Nyerere alitaka ifahamike kuwa Watanzania maskini ndiyo wenye nchi yao. Eneo la kupigania maisha ya Watanzania maskini alilichambua kuwa ni kwanza kujenga uchumi wa wananchi, kushughulikia elimu, afya, kilimo na viwanda.

Maana yake, Mwalimu Nyerere alitaka mkazo uwe kujenga huduma bora za kujamii, vilevile kuboresha njia za kiuchumi. Hili Mwalimu Nyerere angelipigia kelele hata Uchaguzi Mkuu 2025. Maisha ya Watanzania, ustawi wao, ni agenda muhimu. Tena namba mbili.

Udini ulikuwa agenda namba tatu ya Mwalimu Nyerere mwaka 1995. Ingekuwa hivyo mwaka 2025. Mwalimu Nyerere hakupenda udini kuwagawa Watanzania. Mwalimu, alitaka kila mmoja aabudu kwa imani yake, kisha Watanzania wabaki wamoja kupitia Utanzania wao.

Nakumbuka vuguvugu la G55, wabunge walioanzisha harakati za kudai Tanganyika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwalimu Nyerere hakukwepesha, aliwaambia kuwa ndani ya agenda yao kulikuwa na udini. Wakati huo, Rais alikuwa Ali Hassan Mwinyi.

Hivi sasa nchi ipo kwenye hatari kubwa ya udini. Mitandaoni kuna watu wanapambana kuitafuta Tanganyika. Inasikitisha kuwa kelele za Utanganyika huibuka pale ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anapotokea Zanzibar. Hili Mwalimu Nyerere asingelikalia kimya.

Ukabila ni agenda ambayo Mwalimu Nyerere asingeikalia kimya. Ukabila umeendelea kuwa tatizo Tanzania. Mwalimu aliukemea mwaka 1995, angeukaripia mwaka 2025. Mwalimu alichukia kila aina ya ubaguzi. Alitaka Watanzania wawe kitu kimoja. Hakutaka mgawanyiko wa aina yoyote, ukabila, udini, ukanda, wala Utanganyika na Uzanzibari.

Vema kuitambua na kuiheshimu misingi iliyoasisi taifa chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere. Kwamba pamoja mambo mengi, katika Kitabu cha Azimio la Arusha, sehemu ya madhumuni ya Tanu, kipengele (b), ni kuhusu msimamo wa nchi kwa haki za binadamu.

Mwalimu Nyerere aliwaongoza waasisi wa taifa hili kuishi misingi yake na kusimama kidete juu ya uvunjwaji wa haki za binadamu popote pale ulipokuwepo. Kwa hali hiyo, Mwalimu angeumizwa na matukio ya watu kupotea, angetaka Uchaguzi Mkuu 2025, ubebe agenda ya kutokomeza upotevu wa Watanzania bila maelezo.