Dar es Salaam. Hakuna ubishi kwamba, katika dunia ya leo, mabadiliko ya kiteknolojia yanakwenda kasi isiyodhibitika kuanzia roboti, Akili Ubnde (AI), mitandao ya 5G, hadi matumizi ya simu janja.
Elimu nayo haijaachwa nyuma. Sasa siyo tu suala la kujifunza, bali pia namna tunavyofundisha, tunavyopata rasilimali za kujifunzia na tunavyofanya tathmini; yote haya yakitegemea zaidi teknolojia.
Tanzania nayo imeanza safari yake ya kidigitali. Sekta ya elimu imewekwa kwenye shinikizo jipya; wanafunzi wanapaswa kumudu ujuzi wa kidigitali, walimu wanahitaji mbinu mpya, na shule zinapaswa kuwa na miundombinu imara ya Tehama. Lakini swali kubwa ni moja: je, shule zetu ziko tayari kwa mapinduzi haya?
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Watanzania wengi sasa wanatumia mtandao wa intaneti, ingawa kiwango halisi kinatofautiana kati ya mijini na vijijini.
Kwa mfano, hadi Machi 2025, idadi ya watu waliojisajilio kutumia intaneti walikuwa milioni 49.3.
Aidha, ripoti za taasisi ya utafiti ya EdTech Hub zinaonyesha kuwa ni takribani asilimia 13 pekee ya Watanzania walio na muunganisho binafsi wa intaneti.

Wakati huo huo, takwimu za elimumsingi (BEST-2021) zinaonyesha kuwa uwiano katika shule za msingi, ni wanafunzi 371 kwa kifaa kimoja cha Tehama kama kompyuta au kishkwambi, na katika shule za sekondari, wanafunzi 85 wanatumia kifaa kimoja.
Kwa hali hii, wachambuzi wa elimu wanasema bila uwekezaji mkubwa katika vifaa, walimu stadi, na sera madhubuti, elimu ya kidigitali inaweza kubaki ndoto nzuri tu kwenye makaratasi na kusiwe na ufanisi wa kutosha kivitendo.
Dk Paul Loisulie, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anasema safari ni ndefu, lakini tumeanza vizuri.
Anasema elimu ya kidigitali ni ufundishaji na ujifunzaji unaofanyika kupitia majukwaa ya kimtandao.
“Tangu kuzinduliwa kwa sera ya elimu ya mwaka 2014 (toleo la 2023) na Dira ya 2025, Serikali imefanya hatua kubwa sana ya kusomesha walimu, kugawa vifaa vya Tehama, kuanzisha masomo ya Tehama ngazi za msingi na sekondari, na kugawa vishikwambi kwa walimu wote,” alisema wakati alipozungumza na gazeti hili.
Hata hivyo, Dk Loisulie anakiri kuwa shule nyingi za umma bado ziko hatua za awali katika utekelezaji wa elimu hii…“Lakini safari moja huanzisha nyingine; ni mwanzo mzuri.’’
Kwa mtazamo wake msomi huyo, faida za elimu ya kidigitali ni pana zikiwemo kurahisisha mbinu za kujifunza, kuongeza upeo wa wanafunzi na walimu pamoja na kupunguza upungufu wa vitabu.
Aidha, changamoto kubwa anayoiona ni uhaba wa vifaa na miundombinu, hasa vijijini, japokuwa Serikali inaendelea kupeleka umeme kupitia miradi kama REA na kuandaa vyumba maalum vya Tehama.
“Umeme na intaneti bado ni changamoto, lakini shauku na dhamira ya wadau ni kubwa. Hiyo ndiyo nguzo ya mafanikio,” alisema Dk Loisulie.
Anasisitiza kuwa mafanikio ya elimu ya kidigitali hayawezi kupimwa tu kwa idadi ya kompyuta au projekta, bali kwa namna walimu na wanafunzi wanavyoweza kutumia teknolojia kutatua matatizo halisi.
Naye Jumanne Mpinga, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kiraia la Education Gauge for Growth Tanzania (EGG-Tanzania), anasema uzoefu unaonyesha kuwa ni chini ya asilimia tano ya shule nchini zikiwamo za Serikali na binafsi ndizo zenye vifaa vya kutosha vinavyowezesha ufundishaji wa Tehama.
“Serikali imejitahidi kuandaa miongozo na mitalaa, lakini vifaa bado ni tatizo. Hata hivyo, si kila suluhisho ni lazima ligharimu pesa nyingi, ubunifu unaweza kusaidia,” anasema.
Kupitia shirika lake, Mpinga yumo kwenye mchakato wa kubuni mfumo uitwao EGG Connect, ambao utaruhusu mwalimu mmoja kufundisha shule zaidi ya 100 kwa wakati mmoja kupitia teknolojia ya video na kamera.
“Mwalimu ataingia darasani na projekta, kompyuta na kamera tu. Wanafunzi katika shule zote wataweza kumuona na kumsikiliza moja kwa moja,” anasema.
Anasema mfumo huo utasaidia kukabiliana na uhaba wa walimu na vifaa, huku ukihakikisha wanafunzi wengi zaidi wanapata elimu bora.
Kuhusu changamoto za miundombinu, Mpinga anasema tatizo la umeme linapungua kutokana na upanuzi wa miradi ya REA.
“Vifaa vya Tehama havitumii umeme mwingi, hivyo tatizo kubwa sasa ni upatikanaji wa intaneti yenye kasi,” anasisitiza.
Aidha, anaonya kuwa walimu wengi bado hawajaandaliwa kukabiliana na teknolojia ya Akili Unde (AI), jambo linaloweza kuathiri ubora wa elimu nchini.
“Kama walimu hawatafahamu kutumia vema Akil Unde, wanafunzi watawapita kwa maarifa. Na hii ni hatari kwa mustakabali wa elimu yetu,” anaonya.
Mpinga anashauri Serikali kushirikiana na sekta binafsi na vyuo vya elimu ya juu kuandaa mafunzo maalum kwa walimu kuhusu matumizi ya Akili Unde, uchambuzi wa data, na usalama wa mtandao. “Mwalimu wa leo lazima awe sehemu ya mabadiliko, si mtazamaji,” anaongeza.
Kwa upande wake, Said Miraj Abdullah, mwalimu mstaafu na mchambuzi wa masuala ya kijamii, anasema shule nyingi nchini bado hazijawa tayari kwa mapinduzi ya kiteknolojia.
“Kuna haja ya mabadiliko makubwa katika sera, mafunzo ya walimu, na upatikanaji wa vifaa. Tukishindwa kufanya hivyo, tutapata wanafunzi wenye ujuzi mkubwa wa teknolojia kuliko walimu wao,” anasema.
Miraj anashauri Serikali kuandaa wakaguzi maalum wa kufuatilia namna walimu wanavyotekeleza mafunzo ya Tehama.
Pia anasisitiza umuhimu wa kuwa na miundombinu ya msingi kama umeme, kompyuta, vishikwambi, na maabara za Tehama katika kila shule.
“Tunahitaji walimu bora, vifaa vya kutosha, na mtandao unaofika kila kona ya nchi. Vinginevyo, pengo kati ya wanafunzi wa mijini na vijijini litaongezeka,” anaonya.
Anasema pamoja na changamoto hizo, elimu ya kidigitali inaleta fursa kubwa kutoka kuongeza ubora wa elimu hadi kuandaa vijana watakaoshindana kimataifa kwenye sekta za sayansi, biashara, na kilimo.
“Hiki ndicho kizazi cha ‘Google’ tukikosea kukiandaa, tutabaki nyuma kama taifa,” anasisitiza.

Ofisa Mitihani kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Mwanawetu Mmuni, anasema mitalaa ya sasa inatambua na kuunganisha dhana ya elimu ya kidijitali kwa kila ngazi ya elimu.
“Kwenye shule za awali, msingi, sekondari na hadi vyuoni, elimu ya kidijitali imehusishwa kwa kiwango kinacholingana na uwezo wa kila ngazi,” anasema.
Anabainisha kuwa Serikali kupitia mradi wa Digital Tanzania Project (DTP), inaendelea kuimarisha miundombinu na kuunganisha shule nyingi zaidi katika mfumo wa Tehama, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mtandao wa kasi unaoweza kusaidia walimu kufundisha kwa ubunifu.
“Kuweka somo la Tehama katika mtalaa ni hatua kubwa sana. Labda changamoto iwepo kwenye utekelezaji, hasa kutokana na tofauti ya uwezo kati ya shule za mijini na vijijini,” anasema Mmuni.
Anashauri kuwa ili kuimarisha elimu ya sayansi, Serikali inapaswa kuendelea kuhimiza ufundishaji wa masomo hayo kwa njia za kidijitali.
“Badala ya kufundisha kemia au biolojia kwa njia za kawaida, tuanze kutumia teknolojia video, maabara za mtandaoni, na mifumo ya kujifunza kwa vitendo,” anaeleza,
Kwa maoni yake, sera ya elimu toleo la 2023, imeshabeba kikamilifu suala la teknolojia.
Kinachohitajika sasa ni miongozo ya utekelezaji wa kina, usimamizi madhubuti, na bajeti mahsusi kwa ajili ya Tehama. Elimu ya kidijitali si anasa, ni uwekezaji wa Taifa,” anasisitiza.
Serikali imeendelea kuwekeza katika kueneza elimu ya kidijitali nchini, hasa kwa kuanzisha madarasa janja katika shule mbalimbali.
Mfano mzuri ni Shule ya Sekondari Kibaha mkoani Pwani, ambayo imepokea kompyuta 50 za kisasa, vishikwambi, na projekta katika kila darasa, pamoja na muunganisho wa mtandao wa kasi unaowawezesha walimu kufundisha kwa njia za kidigitali.
Shule hii ni sehemu ya mpango wa Serikali wa Digital Tanzania Project (DTP) ambao unalenga kuhakikisha kila shule ya sekondari nchini inapata miundombinu ya msingi ya Tehama.
Mbali na hilo, shule za vijijini zimeanza kuunganishwa katika mfumo huu wa kidigitali kupitia miradi ya REA na ufadhili wa Serikali wa vifaa vya Tehama.
Shule za sekondari Ruvuma na Mbeya zimepewa vyumba vya Tehama vyenye kompyuta, projekta na mtandao wa intaneti, jambo linalowezesha walimu kufundisha kwa ubunifu na wanafunzi kupata elimu bora bila kujali eneo wanaloishi.
Kupitia juhudi hizi, Serikali inalenga kupunguza pengo la elimu kati ya shule za mijini na vijijini, huku ikihakikisha elimu ya kidijitali inakuwa nyenzo ya kuandaa vijana kushindana kimataifa.
Mustakabali wa kidigitali ni sasa
Ni wazi kuwa Tanzania ipo kwenye njia sahihi, lakini bado safari ni ndefu. Kuna sera, dhamira na miradi mizuri, lakini utekelezaji unahitaji kasi na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, wazazi na walimu.
Teknolojia si chaguo tena kwa sasa, bali ni uhalisia wa dunia ya leo. Swali si kama tutaiweka darasani, bali lini na kwa maandalizi yapi.
Ni wakati wa kila mdau kuhakikisha elimu ya kidigitali inakuwa nyenzo ya usawa, si ubaguzi. Tukichukua hatua sasa, tutawajenga watoto wetu kuwa washindani wa dunia ya kesho. Ama tukisubiri, tutapoteza kizazi kizima.
Kwa maana mustakabali wa elimu ya Tanzania ni wa kidigitali si ndoto, tena, bali ni uhalisia unaosubiri kutekelezwa