WAKILI MNDEME AAHIDI MAENDELEO KWA WANANCHI WA TUNGI NA MJIMWENA KIGAMBONI

……………..

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigamboni kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Wakili Mwanaisha Mndeme, ameendelea na kampeni zake kwa kuzungumza moja kwa moja na wakazi wa Kata ya Mjimwena na Tungi, akielezea vipaumbele vya maendeleo ikiwa ni kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba.

Akiongozana na wagombea udiwani wa kata hizo kupitia chama cha ACT Wazalendo, Wakili Mndeme amezungumza na wakazi kuhusu umuhimu wa kuboresha miundombinu, huduma bora za afya, utoaji wa ajira, pamoja na mikopo ya asilimia 10% inayolengwa kwa makundi ya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.

Mndeme amesema kuwa vipaumbele hivi vitasaidia kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kata hizo, huku akisisitiza kuwa atahakikisha masuala haya yanazingatiwa endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Kampeni hii ya mtaa kwa mtaa ni sehemu ya juhudi za Wakili Mndeme za kuwafikia wakazi moja kwa moja na kuelewa changamoto zao kabla ya uchaguzi mkuu ujao.