Dar es Salaam. Wakati Tanzania inaadhimisha kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Watanzania wametakiwa kujifunza na kuyaishi maono ya kiongozi huyo hasa katika kusimamia uadilifu na uzalendo kwa Taifa lao.
Mwalimu Nyerere anajulikana si tu kama kiongozi wa kisiasa, bali kama mwasisi na mlezi wa amani, mshikamano na umoja wa wananchi katika taifa hili. Leo, Oktoba 14, 2025, ametimiza miaka 26 tangu alipofariki dunia mwaka 1999.
Kila mwaka, kiongozi huyo anakumbukwa kwa namna alivyojenga misingi ya amani na umoja na viongozi wanakumbushwa kuendeleza misingi hiyo aliyoiacha hasa katika siasa, maendeleo ya jamii na uhuru wa kiuchumi.
Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 14, 2025 kwenye kikao cha wafanyabiashara wa Jimbo la Kivule, Dar es Salaam, mchumi na mwanasiasa, Florian Karugaba amesema wanasiasa wa sasa wanapaswa kujifunza kutokana na misingi ya siasa safi na uongozi wa kizalendo ambao alianzisha Mwalimu Nyerere.
Amesema misingi hiyo ilikuwa ikisisitiza kujenga taasisi imara za chama na Serikali, badala ya kujikita kwenye siasa za majukwaa, makundi na ubinafsi.
Karubaga amesema Nyerere alianza kama mwanaharakati, akitetea haki za wafanyakazi, lakini alibadilika kuwa mwanasiasa wa kujenga taasisi zenye nguvu ambazo zingeliendeleza taifa kwa amani.
“Mwalimu Nyerere alikuwa mwanaharakati wa kweli, lakini alipogundua kuwa harakati pekee hazitoshi, aliamua kuingia kwenye siasa ili kujenga taasisi. Ndiyo maana alipigania uhuru kwa njia za amani, siyo kwa vurugu,” amesema Karugaba.
Amesema chama chochote kinachotaka kushika madaraka lazima kijenge muundo imara wa taasisi ambao unaweza kuongoza Taifa bila mtikisiko na si chama kinachotegemea ushawishi wa mtu mmoja au makundi.
Amesema ili kupambana na mfumo wenye mizizi, lazima ujenge taasisi imara zaidi. Ndani ya historia ya Tanzania, Mwalimu Nyerere aliitumia dhana ya Hegemonic Stability Theory kuunda TANU ambayo leo imerithi Chama cha Mapinduzi (CCM), kama taasisi imara yenye misingi ya kipekee.
“Kiongozi wa kweli anapaswa kuwa na dira, mpango na uwezo wa kujenga taasisi. Tukitaka Taifa liendelee, lazima tujifunze kutoka kwa Nyerere. Alileta mabadiliko bila kupigana na aliwaongoza wananchi kwa hoja, si kwa hasira,” amesema.
Hata hivyo, Karugaba amesema wanasiasa wanapaswa kuwekeza katika taaluma za siasa, kuendeleza sifa za chama kwa kujenga taasisi zenye misingi na kuwa na uwezo wa kutuliza wafuasi wakati wa mgogoro.
Naye, mchambuzi wa siasa na uchumi, Amos Haganya amesema Nyerere alikuwa mtunga sera na mfalsafa wa kisiasa aliyependelea mazungumzo na kutafuta amani badala ya vurugu, hivyo ni jukumu la viongozi wa ngazi zote kuendeleza hiyo tamaduni ya kuwatuliza wananchi wakati wa mizozo.
“Mwalimu hakuwahi kurudisha wananchi kusababisha vurugu badala yake aliwatuliza. Hii ndio njia tunayotakiwa kuifuata,” amesema Hangaya.
Amesema viongozi wa sasa wanatakiwa kujiepusha na tabia ya kushinikiza mwenzao kutoka katika chama na kujiunga na chama kingine, kwa sababu tabia hiyo inasababisha mgongano wa kijamii.
Kwa upande wake, dereva wa malori, Juma Murundi amesema ni muda muhimu wa kukumbuka misingi na falsafa alizoacha ambazo ziliweka Tanzania katika msingi wa umoja, amani na utu.
Murundi amesema Mwalimu Nyerere alikuwa na maadili yake katika siasa na uongozi, hasa alivyokuwa akipinga viongozi kujihusisha na biashara binafsi.
“Mwalimu alikuwa wazi ukitaka kuwa mwanasiasa, basi achana na biashara. Ukichagua siasa halafu ukawa na kampuni, unaweza kujipa tenda za Serikali. Hiyo ndiyo tofauti ya viongozi wa wakati ule na wa sasa,” amesema Murundi.
Amesema kuwa tofauti kubwa kati ya siasa za wakati wa Mwalimu Nyerere na siasa za sasa ni kwamba wakati ule, viongozi walikuwa watumishi wa wananchi, lakini sasa siasa imegeuzwa kuwa njia ya kujitafutia utajiri binafsi.
“Siku hizi unaona mwanasiasa akipata cheo, badala ya kuwahudumia wananchi, anaanza kujilimbikizia mali. Hiyo haikuwa falsafa ya Mwalimu. Yeye alitaka viongozi watumikie wananchi, si kujitumikia wao,” amesema Murundi.
Ameongeza kuwa falsafa ya Mwalimu ya kufanya kazi, kuheshimu utu na kuendeleza mshikamano bado ina thamani kubwa katika jamii ya sasa, hasa kwa vijana wanaotakiwa kutazama mbele kama alivyofanya Mwalimu.
“Mwalimu alikuwa anaona Taifa la kesho, si la leo tu, aliweka misingi ya umoja na kazi ambayo inatufanya leo tuwe na amani. Hivyo viongozi wa sasa wajifunze kumtumikia mwananchi, si familia zao pekee,” amesema Murundi.
Amesema Nyerere alifanikiwa kuliondoa taifa katika ukabila na kulijenga katika misingi ya utu na kazi.
“Mwalimu Nyerere alitufundisha kufanya kazi kwa bidii, na ndio maana leo tunayo amani na mshikamano. Hakuamini katika ukabila, bali alituunganisha kama Watanzania,” amesema Murundi.