Dodoma. Wazazi, walezi na ndugu wa karibu wametajwa kuwa chanzo kikuu cha matukio ya ubakaji, ulawiti na vitendo vya ukatili vinavyowakumba watoto huku wengi wakishindwa kueleza ukweli hata wanapobaini matukio hayo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne, Oktoba 14, 2025, na Meneja wa Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo jijini Dodoma, Darius Kalijongo wakati akizungumza na viongozi wa dini waliotembelea kituo hicho na kutoa misaada.
Viongozi hao wa dini kutoka jijini Dar es Salaam na Dodoma wameongozana na makundi mbalimbali ya taasisi zisizo za kiserikali katika kuadhimisha kumbukizi ya kifo cha Mwalimu, Julius Nyerere na wametumia fursa hiyo kutoa zawadi na kushiriki michezo na watoto hao.
Kalijongo amesema watoto wengi wanaolelewa katika kituo hicho wamefikishwa hapo kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo ukatili, umaskini, migogoro ya kifamilia na utelekezaji, huku baadhi yao wakiwa waathirika wa vitendo vya kikatili vilivyofanywa na ndugu wa karibu.
Ameongeza kuwa jamii inapaswa kujenga moyo wa uzalendo na upendo kwa kuwajali watoto wote bila kujali uhusiano wa damu, huku akihimiza wale wenye nafasi, kutembelea makao hayo mara kwa mara ili kuwatia moyo watoto na kuwapa faraja.
“Kituo hiki kinapokea watoto waliotelekezwa, wenye utapiamlo, waliofiwa na wazazi pande zote, wanaoishi mitaani, waliokinzana na sheria au waliofanyiwa ukatili. Tunawachukua kama hatua ya mwisho baada ya juhudi za jamii kushindikana. Tunawaomba majirani na makundi mbalimbali kuwatembelea watoto hawa mara nyingi,” amesema Kalijongo.
Kwa upande wake, Mchungaji Benedina Nyoni wa Kanisa la Calvary Assemblies of God (CAG) la jijini Dar es Salaam, amesema watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, hivyo wanapaswa kupewa kipaumbele katika malezi, ulinzi na upendo.
Amesema iwapo kundi hilo litaachwa bila malezi bora, Taifa la kesho litakuwa dhaifu kwani litazalisha kizazi kisicho na maadili wala uwezo wa kujenga nchi.
“Kanisa letu na mengine tumeendelea kushirikiana katika kuwalea watoto katika vituo kama vile kituo cha rekebishi cha Upanga, Dar es Salaam, na tumeona matokeo chanya kwani baadhi yao wamekua watu mashuhuri na wachangiaji wazuri kwa jamii,” amesema Mchungaji Nyoni.
Aidha, mmoja wa watoto wanaolelewa kituoni hapo, Pendo John (siyo jina lake halisi), ameeleza kuwa watoto wengi wanaishi katika mazingira magumu na changamoto nyingi kabla ya kufikishwa kwenye vituo hivyo.
Pendo amesema baadhi ya hadithi za wenzake ni za kusikitisha kiasi kwamba wengi wao hawatamani tena kurudi katika familia zao kutokana na mateso na vitendo vya kinyama walivyofanyiwa na watu wa karibu vikiwamo vya ubakaji na ulawiti.