Dk Tindwa ataja sababu za Samia kuchaguliwa kiti cha urais

Kilwa. Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Dk Chakou Tindwa amesema uzoefu wa uongozi alionao mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa sababu kuu zinazomfanya astahili kuendelea kuiongoza nchi kwa miaka mingine mitano.

Akizungumza leo Jumatano Oktoba 15, 2025 katika mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kwa ajili ya kujadili masuala muhimu kuelekea uchaguzi mkuu, Dk Tindwa amesema Watanzania wanapaswa kumpa tena ridhaa ya kuongoza kutokana na uthubutu, uzoefu na uadilifu wake katika uongozi wa taifa.

“Rais Samia anastahili kupewa tena nafasi ya kuongoza kwa sababu ana uzoefu mkubwa. Amewahi kuwa mbunge, waziri na makamu wa rais, hivyo ana uelewa mpana wa uongozi wa nchi,” amesema.

Amesema kwa upande wa mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi, ameanza kuongoza tangu akiwa kijana, “jambo linaloonyesha kuwa chama chetu kina viongozi wabobezi watakaoliendeleza taifa.”

Ameongeza kuwa serikali inayoongozwa na Samia imekuwa ya vitendo, ikitekeleza miradi mikubwa ya kimkakati iliyobuniwa kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

“Kwa sasa dawa zinapatikana hospitalini, miundombinu inaboreshwa na miradi mikubwa kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, reli ya kisasa (SGR) na Daraja la Kigongo–Busisi, yote imekamilishwa au inaendelea kukamilika kwa kasi kubwa,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mafia, Amina Khatibu amesema umoja huo umejipanga kuhakikisha Samia anachaguliwa tena ili aendelee kutekeleza miradi yenye manufaa kwa vijana na taifa kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mafia, Mohamed Hassan Faki amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Samia, wilaya hiyo imepiga hatua kubwa za kimaendeleo kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali.

“Tangu Rais Samia aingie madarakani, zaidi ya Sh60 bilioni zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara, madarasa, miradi ya maji na kuboresha huduma za afya,” amesema Faki.

Kupitia mkutano huo, Dk Tindwa amewaomba wananchi wa Mafia na mkoa mzima wa Pwani kumpigia kura mgombea huyo wa CCM kwa nafasi ya urais, Juma Kipanga kwa ubunge wa Mafia, pamoja na wagombea wote wa udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi.