MCHEZAJI wa zamani wa Simba, William Lucian ‘Gallas’ amesema kama kuna kitu alichofanikiwa beki wa timu hiyo, Shomari Kapombe ni moyo mgumu wa kukwepa mishale na kuweka nguvu katika kazi yake inayowafanya mashabiki waendelee kumpa heshima.
Ameifafanua kauli yake hiyo ni namna baadhi ya mashabiki wanaomuona Kapombe ni mzee, lakini bado ameendelea kuonyesha umuhimu wake wa kucheza kikosi cha kwanza na bado ni msaada kwa timu.
“Mara kadha zilikuwepo stori za Kapombe kutaka kuachwa na Simba huku baadhi mitandaoni wakimwita mzee, wakati huohuo kuna wachezaji wa kigeni ambao wana umri mkubwa kuliko wake ila wanapewa heshima, hilo kwangu linafanya nimpe maua yake,” amesema Gallas.
“Kapombe bado ana ufundi wake mkubwa mguuni ambao binafsi najifunza vitu vingi kutoka kwake ambavyo navifanyia kazi ninapokuwa nacheza mechi.”

Mbali na hilo, alizungumzia ugumu wa kukaa nje ya kazi kwa muda mrefu, akikiri wazi kinachombeba ni kujuana na watu wanaompa sapoti ya hapa na pale.
“Timu ya mwisho niliyokuwa nimeichezea ni Tabora United ambayo kwa sasa inaitwa TRA kipindi ilipokuwa Daraja la Kwanza, msimu huu kuna timu nilitakiwa nijiunge nayo, ila kuna vitu havikukaa sawa, hivyo nipo nafanya mazoezi na natarajia dirisha dogo nitaanza kucheza,” amesema.

Gallas ambaye alipitia kituo cha kulelea vipaji cha Moro Youth Academy, mwaka 2016 alikumbana na adhabu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya sheria na hadhi za wachezaji ya kufungiwa kwa mwaka mmoja baada ya kuonekana kuwa na matatizo kwenye mkataba wake kwa kosa la kusaini kwenye klabu mbili tofauti kwa msimu mmoja. Nyota huyo ilibainika alisaini katika timu za Ndanda na Mwadui.