Mbeya. Mgombea Urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo amesema iwapo atapata ridhaa ya kuwa rais, ataunda tume ya kuchunguza kundi linalojiita ‘Wasiojulikana’ na kukomesha vitendo vya utekaji na mauaji.
Akizungumza leo Jumatano Oktoba 15, 2025 katika mkutano wake wa kampeni jjini hapa, Gombo amesema hawezi kukubali maisha hayo akieleza kuwa anaenda kushughulikia katiba mpya na kwamba mwisho wa CCM ni mwaka huu.
Amesema CUF haipo tayari kuwa ya kwanza kumwaga damu, badala yake wanahitaji kuingia madarakani kwa amani, akieleza kuwa mwaka huu chama hicho kimejipanga akiomba wananchi kumuunga mkono ili kufikia malengo.

“Msiwe wanyonge, muda wa kuamua ni sasa, tumechoka na wale wanaojiita wasiojulikana, hatusikii mamlaka wakizungumza hili, sasa natoa rai kwa vyombo vya dora nchini vitende haki, Watanzania wapige kura kwa amani,” amesema Gombo.
Amesema haki haiwezi kupatikana kama watawala hawatendi haki, hivyo wananchi wakichague CUF chama kinacho amini katika haki.
Ameongeza kuwa Tanzania si nchi masikini bali imejaa rushwa, hivyo CUF kikiingia madarakani kitadhibiti mianya yote ya rushwa na kitatoa huduma za afya na elimu bure kwa kuwa fedha zipo.
“Kama hamtaamua kuiondoa CCM mwaka huu, mtaiondoa kwa damu zenu, twende tukapige kura kwa wingi na bahati nzuri mimi niliwahi kuwa mtumishi, hivyo najua namna fedha zinavyopatikana na zinakokwenda,” amesema mgombea huyo.
Akizungumzia huduma ya umeme, amesema kila mwananchi akimaliza ujenzi wa nyumba yake, nguzo ya umeme itamfikia.
“Ajira zipo, tutoa za kutosha kuanzia hospitalini, shuleni na hata za Jeshi la Polisi,” amesema.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Yusuph Mbungiro ameionya INEC itende haki katika uchaguzi huo, vinginevyo hawataiamini tena.
Amesema tayari wameanza kubaini kasoro akisema; “Tunaionya kutopendelea upande mmoja haswa CCM, katika mfano wa fomu ya wagombea amewekwa mgombea Urais chama hicho sehemu ya kwanza jambo linalotuweka shakani na kuhisi kuwapo upendeleo.”
Amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura na iwapo itathibitika wagombea wao wameshinda INEC iwatangaze kwa haki.
Mgombea Ubunge wa Uyole, Ibrahim Mwakwama amesema amejipanga kuwatumikia wananchi kwa kujenga miundombinu na viwanda kwa manufaa ya Uyole na si maslahi binafsi.
“Maendeleo hayawezi kuja bila amani, nikiingia bungeni wiki moja tu nitaita mkutano wa dharula wananchi kujadiliana masuala ya amani, hatuwezi kuishi kwa hofu muda wote, watu wanapotezwa, kutekwa, kuuawa,” amesema Mwakwama.