Unguja. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed amesema chama hicho kimejengwa juu ya misingi mitatu ikiwemo haki, maridhiano na ustawi wa jamii hivyo kina kila sababu ya wananchi kukichagua kwa masilahi ya nchi.
Hayo ameyasema leo Jumatano Oktoba 15, 2025 wakati akizungumza na mawakala wa chama hicho watakaosimamia uchaguzi mkuu ujao, Kiembesamaki, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema chama hicho kina uthubutu wa kuzungumza wakati wengine wakiwa wamenyamaza na kina sera zinazojibu changamoto za Wazanzibari, hivyo amewataka wananchi kukichagua kwani kina lengo la kuijenga Zanzibar yenye utu, heshima na fursa kwa wote.
Mgombea Urais kupitia chama Cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed akizungumza na mawakala wa chama hicho, Kiembesamaki Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Picha na Zuleikha Fatawi
“Mawakala nendeni mkafanye kazi yenu kwa uadilifu na nidhamu ili kura zisiibiwe wala kupotea, tafuteni sauti za mabadiliko kwani kura ni haki, amani na maisha bora ya kila Mzanzibari,” amesema.
Vilevile, amesema endapo akichaguliwa atahakikisha walimu wote wa madrasa wanalipwa mshahara wa staha wa Sh300,000 kila mwezi na kusajiliwa katika mfumo rasmi kwa lengo la kupatiwa stahiki zao.
Amesema fedha hizo zitapatikana kupitia bajeti ya elimu ya jamii na misaada itakayotolewa kwa ajili ya dini.
“Zanzibar ina walimu 3,000 wa madrasa na ADC inaamini kuwa elimu hiyo ni nguzo ya maadili ya Taifa itahakikisha inawainua walimu kwa hadhi inayostahiki,” amesema.

Mawakala wa Chama cha Alliance for Democratic Changes (ADC) wakimsikiliza Mgombea Urais wa Chama hicho, Hamad Rashid Mohamed. Picha na Zuleikha Fatawi
Amesema chama hicho kinatambua mchango wa walimu wa madrasa katika malezi ya watoto na vijana na wameshajitoa miaka mingi hivyo ni wakati wao kwa sasa kupatiwa malipo kwa kazi hiyo.
Amesema kazi ya utumishi ni ngumu kwa maana hiyo amejitoa kuwatumikia Wazanzibari bila kuweka ubaguzi, migogoro na yote yatakayosababisha machafuko.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake ADC, Nadhera Haji amesema anafurahishwa kuona wanawake wanapewa fursa kwani wapo tayari kulinda kura za chama hicho kwa amani.

Mawakala wa Chama cha Alliance for Democratic Changes (ADC) wakimsikiliza Mgombea Urais wa Chama hicho, Hamad Rashid Mohamed. Picha na Zuleikha Fatawi
Pia amewataka wazazi kuzungumza na vijana wao kuacha kutumika vibaya kwa wanasiasa na wanapomaliza kupiga kura watulie majumbani kwao.
Mbali na hilo amewaomba wananchi na wanachama kumchagua kiongozi wa ADC kutokana na kuwa uadilifu na juhudi mbalimbali anazozichukua kwa wananchi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Mtumwa Faidh Sadik amewataka wananchi kabla ya kutoka nyumbani kwao wanapaswa kusali kwa ajili ya kumuomba Mungu ajaalie uchaguzi wa utulivu na amani.
Hata hivyo amesema kwa wakala wowote atakayepata kura nyingi katika usimamizi wa Oktoba 29, atapatiwa zawadi maalumu ikiwa ni sehemu ya shukurani kutoka kwa chama hicho.