Heche, Mnyika na wenzao wapewa siku sita kujibu madai ya kudharau mahakama

Dar es Salaam. Mahakama Kuu imewaamuru viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika pamoja na makada wengine kuwasilisha majibu dhidi ya shauri la madai ya kuidharau mahakama ndani ya siku sita.

Amri hiyo imetolewa na Jaji Awamu Mbagwa, leo Jumatano, Oktoba 15, wakati shauri hilo lilipotajwa kwa mara ya kwanza.

Shauri hilo la madai mchanganyiko namba 25480 la mwaka 2025 linatokana na kesi ya kikatiba inayoikabili Chadema kuhusu mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama, baina ya Tanzania Bara na Zanzibar inayosikilizwa mahakamani hapo.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema (Zanzibar) na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

‎Walalamikiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho, Mnyika.

Wakati kesi hiyo ikiwa haijaanza kusikilizwa madai ya msingi, walalamikaji wamefungua shauri la madai dhidi ya viongozi hao wa Chadema, Heche, Mnyika na wenzao wakiwataka wajieleze ni kwa nini wasifungwe kama wafungwa wa madai kwa kudharau amri ya mahakama hiyo.

‎Mbali ya Heche ambaye ni mjibu maombi wa kwanza katika shauri hilo, wengine ni Mnyika, Rose Mayemba, Brenda Rupia, Hilda Newton, Twaha Mwaipaya na Gervas Lyenda. Wamo pia Wadhamini wa Chadema.

Kwa pamoja wanadaiwa kuidharau mahakama kwa kukiuka amri ya zuio dhidi ya wadaiwa katika kesi ya msingi ya kikatiba, ambayo kwayo wamezuiwa kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka itakapomalizika.

Wajibu maombi waliokuwapo mahakamani leo Oktoba 15, 2025 ni Mnyika, Bodi ya Wadhamimi wa Chadema iliyowakilishwa na Azaveli Lwaitama na Mnyika, ambao kwa pamoja wamewakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu.

Wakili wa waombaji Shabani Marijani akishirikiana na Alvan Fidelis, ameieleza mahakama kuwa wajibu maombi wote walitumiwa hati ya wito wa kufika mahakamani kwa njia ya baruapepe kupitia wakili wao, Dk Rugemeleza Nshala.

Hata hivyo, Wakili Mpoki amesema wajibu maombi wengine hawajapewa taarifa ndiyo maana hawakufika mahakamani.

Amesema taarifa iliyotumwa kwa baruapepe kwa Dk Nshala inawahusu wajibu maombi wanne waliofika mahakamani kwa kuwa ndio wanaowakilishwa na Dk Nshala.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Mbagwa ameelekeza wajibu maombi wengine wapewe taarifa na wito wa kufika mahakamani mara moja.

Vilevile ameelekeza wajibu maombi wawe wamewasilisha mahakamani majibu yao ifikapo Oktoba 21, 2025, huku akipanga kusikiliza shauri hilo Oktoba 22, 2025.

Pia, ameelekeza mawakili wa wajibu maombi wawasilishe mahakamani na kwa wajibu maombi flash disk yenye picha mjongeo (video) zinazowaonyesha washtakiwa wakikiuka amri ya mahakama.

Awali, waombaji ambao ni walalamikaji katika kesi ya msingi walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakiiomba mahakama itoe amri kuwazuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

‎Juni 10, 2025 mahakama katika uamuzi mdogo ilikubali hoja za walalamikaji ikatoa amri za zuio kama walivyoomba.

Hata hivyo, ‎waombaji katika shauri la kukiuka amri ya mahakama wanadai wajibu maombi wamekuwa wakiikiuka amri hiyo.

Shauri hilo ‎limefunguliwa chini ya hati ya dharura inayothibitishwa na mmoja wa mawakili wa waombaji, Mulamuzi Byabusha. 

‎Byabusha anadai kati ya Juni 10 na Septemba 2025, wajibu maombi wamekuwa wakikaidi waziwazi na mara kwa mara amri hiyo halali.

Anadai wamekuwa wakiendesha na kushiriki shughuli za kisiasa, ikiwemo mikutano ya ndani ya Chadema, mikutano na wanahabari na hotuba kwa umma juu ya masuala ya kisiasa.

Vilevile, anadai katika nyakati tofauti, wamewahamasisha viongozi wengine, mawakala na wanachama wa Chadema kuendelea kufanya shughuli za kisiasa za chama, kinyume cha amri hiyo halali.

Katika kiapo cha pamoja cha waombaji/walalamikaji wamebainisha tarehe mbalimbali ambazo wajibu maombi hao mmoja mmoja au kwa pamoja wamekuwa wakifanya shughuli hizo za kisiasa. Hivyo, wanaiomba mahakama iamuru wajibu maombi wakamatwe na kuwekwa kizuizini kama wafungwa wa madai kwa kukaidi kwa makusudi amri halali ya mahakama.

Katika kesi ya msingi walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo wa rasilimali usio sawa baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, na ubaguzi katika masuala mbalimbali.

Kutokana na hilo, wanaomba mahakama itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A (1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.

Mbali ya hilo, wanaiomba mahakama itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.

Vilevile, wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya mahakama yatakapotekelezwa na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika pamoja na gharama za kesi.

Kesi ya msingi imepangwa kusikilizwa Oktoba 30, 2025 kwa hatua ya pingamizi lililowekwa na walalamikiwa kuhusu mamlaka ya mahakama kwenye kesi yenye madai ya kikatiba kusikilizwa na jaji mmoja badala ya jopo.