Hukumu kesi ya zawadi kwa Askofu Sepeku Novemba 27

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, imepanga Novemba 27, 2025 kutoa hukumu ya kesi ya ardhi iliyofunguliwa na Bernardo, mtoto wa Askofu John Sepeku.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Oktoba 15, 2025 na Jaji Arafa Msafiri, baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wake wa mashahidi watano.

“Baada ya upande wa utetezi kumaliza kutoa ushahidi, mahakama hii inapanga Novemba 27, 2025 kutoa hukumu katika kesi hii,” amesema jaji na kuongeza:

“Hivyo, mawakili wa pande zote mbili mnatakiwa kuwasilisha majumuisho yenu kwa njia ya maandishi Oktoba 28, 2025.”

Kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023 imefunguliwa na Bernardo Sepeku, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Bernardo ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yake anapinga uamuzi wa dayosisi hiyo chini ya uongozi wa Askofu Sosthenes kuwanyang’anya zawadi ya shamba alilopewa baba yao na kumpatia mwekezaji Kampuni ya Xinrong.

Hivyo, anaiomba Mahakama iamuru alipwe fidia ya Sh3.72 bilioni anayodai ndio thamani ya shamba hilo kwa sasa, na Sh493.65 milioni kama fidia ya hasara ya mazao yaliyoharibiwa katika shamba hilo.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi hiyo zilizoko mahakamani, Desemba 8, 1978, Kamati ya Kudumu  ya Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao chake ilipendekeza kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya Ardhi eka 20 na Nyumba, katika kutambua utumishi wake.

Sinodi ya Dayosisi hiyo katika kikao chake cha Machi 8 na 9 ,1980 iliridhia pendekezo hilo na iliazimia na kumpatia Askofu Sepeku, shamba la eka 20 lililoko Buza Wilayani Temeke, na Nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Hata hivyo baadaye uongozi wa sasa wa Dayosisi uliligawa shamba hilo kwa mwekezaji, kampuni hiyo ya Xinrong, ambaye alifyeka mazao mbalimbali waliyokuwa wameyalima na familia ya Sepeku na kisha akajenga kiwanda na nyumba yenye thamani ya Sh165 milioni

Askofu Sosthenes ambaye ni shahidi wa tano wa utetezi, katika ushahidi wake wa maandishi aliowasilishwa mahakamani, pamoja na mambo mengine anadai kuwa waliompa Askofu Sepeku zawadi hizo hawakuwa na mamlaka kufanya hivyo.

Sosthenes alisisitiza hayo hata wakati akihojiwa maswali ya dodoso na jopo la mawakili wa mdai, Deogratius Butawantemi, kutoka kampuni ya uwakili ya Diakonus Attorneys, Gwamaka Sekela na Eric Amon.

Hata hivyo, kabla ya kupangwa kwa tarehe hiyo ya hukumu, wakili wa utetezi, Dennis Malamba alimuongoza shahidi huyo kujibu hoja za kusawazisha zilizotokana na maswali aliyohojiwa na mawakili wa mdai.

Na sehemu ya mahojiano hayo baina wakili Malamba na shahidi huyo ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Uliulizwa Sepeku amepata hasara ya vitu vingi, wewe unasemaje kuhusu hiyo hasara?

Shahidi: Siitambui hasara hiyo kwa sababu eneo lipo chini ya Bodi ya wadhamini.

Wakili: Uliulizwa na wakili Deogratias Butawantemi kuwa familia ya Sepeku imekuwa na mawasiliano na wewe na ukaonyeshwa hizo barua na kwa nini huzifahamu?

Shahidi: Kimsingi kuwa hakukuwa na uhalali na watangulizi wangu kutekeleza mamlaka hayo.

Wakili: Shahidi uliulizwa kuhusu kiasi cha fedha ambacho uliahidi baraza la Kata?

Shahidi: lile lilikuwa ni shauri katika mediation na kama halikupata muafaka kwa wakati ule, basi halikuwa na uhalisia wa kuzungumzwa.

Wakili: Uliulizwa Dayosisi ya Dar es Salaam ina katiba yake?

Shahidi: Haina katiba, inatumia katiba ya Kanisa la Anglikana Tanzania.

Wakili: Shahidi uliletewa kitabu kilichoandikwa na Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhani na ukaambiwa usome ukurasa wa 249 unaelezea shamba na nyumba iliyopo Buguruni Kichwele,  hebu tuambie kama kanisa inakitambuaje?

Shahidi: Kitabu kile hakitambuliki na kanisa.

Wakili: Pia wakili wa mdai, alikuuliza familia ya Sepeku imekuwa na mawasiliano na ofisi yako, hebu ieleze mahakama nini ambacho kipo?

Shahidi: Kimsingi, maoni na mapendekezo waliyokaa kikao cha sinodi yalikuwa ni mapendekezo ya kutoa zawadi hiyo na sio kikao cha kutoa uamuzi.

Wakili: Kuhusu kutolewa kwa eneo la Temeke kwa mwekezaji, taratibu zilikuaje?

Shahidi: Tulizingatia taratibu za kimaandishi na kufanikiwa kutoa eneo na tulimpa mwekezaji

Wakili: Katika ule mkataba, fedha hizo ziliingia kwenye akaunti gani?

Shahidi: Fedha ziliingizwa kwenye akaunti ya bodi ya wadhamini.

Awali, Shahidi huyo alihojiwa maswali ya dodoso na wakili wa mdai, Gwamaka Sekela na sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo.

Wakili: Baba askofu bwana asifiwe

Wakili: Ni kweli wewe ni mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana?

Wakili: Bodi ya Wadhamini huwa inakutana mara ngapi kwa mwaka?

Shahidi: Si chini ya mara mbili au tatu.

Wakili: Umekuwa askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam kwa muda gani sasa?

Shahidi: Miaka saba na miezi saba

Wakili: Kwa kipindi ukiwa mjumbe wa bodi ya Wadhamini, umeshawahi kuuza au kutoa mali za kanisa?

Shahidi: Ndio nimeshawahi.

Wakili: Unakumbuka ni kitu gani ulitoa na pengine ilikuwa mwaka gani?

Shahidi: Manispaa ya Temeke iliomba eneo la ekari tano na Bodi ya Wadhamini kwa kuzingatia kanuni na katiba ilitoa.

Wakili: Iambie mahakama, utaratibu uliotumika ni upi kutoa eneo hilo.

Shahidi: Manispaa ya Temeke iliiandikia barua Bodi ya Wadhamini na kuipeleka makao makuu Dodoma na kulikuwa na maazimio na waliandika barua kwenda  Rita.

Wakili: Je, maamuzi hayo yanaweza kupingwa na mkutano wa Sinodi?

Shahidi: Hayawezi kupingwa.

Wakili: Vipi bodi ya wadhamini wanaweza kupinga maamuzi ya sinodi?

Shahidi: Ndio bodi inaweza kupinga.

Wakili: Baba askofu, utaratibu ukikosewa ndani ya kanisa wa kutoa zawadi inawezekana kurekebisha utaratibu?

Wakili: Kwa mara ya kwanza kusikia askofu Sepeku amepewa shamba ilikuwa lini?

Shahidi: Mwaka 2020 nadhani.

Wakili: Na wakati huo ulishakuwa askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam?

Shahidi: Toka askofu Sepetu astaafu, wamepita maaskofu wangapi hadi wewe kuchukua nafasi hiyo?

Shahidi: Maaskofu watano.

Wakili: Kwa hiyo, kwa lugha nyingine upo hapa mahakamani kupambana na mtangulizi wako? Sema ndio au hapana

Shahidi: Sidhani kama napambana nao.