Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa kongamano la kwanza la kikanda kuhusu ufugaji nyuki Afrika Masharikilitakalofanyika jijini Arusha kuanzia Desemba 11 hadi 12, 2025.
Kongamano hilo lijulikanalo kama Bees East Africa Symposium 2025 (BEASY 2025)litabebwa na kaulimbiu “Kutumia nguvu ya uchavushaji kwa usalama wa chakula, bayoanuwai na maisha endelevu,” likitarajiwa kuwakutanisha wataalamu, wafugaji wa nyuki, watafiti, wakulima, mashirika ya kimataifa, wafanyabiashara na wadau wa mazingira kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.
Mratibu wa kongamano hilo, Malulu Igobeko amesema lengo kuu ni kuhamasisha jamii kutambua nafasi muhimu ya nyuki katika uzalishaji wa chakula, uchumi na uhifadhi wa mazingira.
“Nyuki si chanzo cha asali pekee, bali ni uti wa mgongo wa uzalishaji wa mazao mengi yanayotegemea uchavushaji. Tunataka kuonyesha namna Tanzania inavyoweza kuwa kinara wa Afrika Mashariki katika kuchochea uchumi wa uchavushaji unaojali mazingira,” amesema Igobeko ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Sustainable Agricultural and Agribusiness Development Initiatives Tanzania (SAADIT).
Amesema kongamano hilo litakuwa jukwaa la mafunzo, majadiliano na ubadilishanaji wa teknolojia kuhusu mbinu bora za ufugaji nyuki wa kisasa na namna sekta hiyo inavyoweza kuunganishwa na kilimo endelevu.
Kwa upande wake, Mercy Butta kutoka Kurugenzi ya Usalama wa Chakula na Masoko, Wizara ya Kilimo, amesema mchango wa nyuki katika kuongeza uzalishaji wa chakula nchini umekuwa ukipuuzwa kwa muda mrefu, licha ya umuhimu wao mkubwa katika uchavushaji wa mazao.
“Kwa zaidi ya muongo mmoja, Tanzania imekuwa ikizalisha chakula cha kutosha kwa ukanda wa Afrika Mashariki. Mafanikio haya yamechangiwa pia na kazi ya wachavushaji kama nyuki. Hivyo, kulinda nyuki ni kulinda uchumi na usalama wa chakula,” amesema Butta.
Naye Aneth Moshi kutoka Kurugenzi ya Misitu na Ufugaji Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema nyuki wamekuwa chachu katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kijamii.
Hata hivyo, ameonya kuwa wachavushaji hao wako kwenye hatari kutokana na uharibifu wa mazingira, matumizi ya kemikali na mabadiliko ya tabianchi.
“Nyuki wanachangia kudumisha bioanuwai na afya ya mimea ya asili. Tunapaswa kuchukua hatua madhubuti kulinda makazi yao ili kuendeleza maisha endelevu,” amesisitiza.
Kongamano hilo linaratibiwa na SAADIT kwa ushirikiano na wizara na taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Katika hatua nyingine, BEASY 2025 litakuwa jukwaa rasmi la uzinduzi wa mradi wa Hive to Harvest, sehemu ya mpango unaolenga kuunganisha ufugaji nyuki wa kisasa na kilimo kinachotegemea uchavushaji katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Njombe na Iringa.