Maabara tano kupima vifaa vya umeme majumbani

Dar es Salaam. Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) wameanzisha maabara tano za kisasa zitakazopima vifaa vinavyotumia umeme kabla ya kuingia sokoni, kutumika majumbani.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa maabara hizo na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambalo lina jukumu la kuandaa viwango ni kupunguza upotevu wa umeme unaotokana na vifaa ambavyo havina ufanisi katika matumizi yake.

Vifaa vilivyolengwa kwa ajili ya upimaji ni televisheni, feni, mota za umeme, friji, kiyoyozi (AC), Fensi za umeme, majokofu na majiko ya umeme.

Kamishina wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Innocent Luoga, amesema hayo leo Oktoba 15, 2025, katika makao makuu ya (TBS) jijini Dar es Salaam.

Luoga amesisitiza kuwa maabara hizo zitazinduliwa rasmi kesho na kuanza kufanya kazi mara moja.

“Tunapotumia vifaa vyenye ufanisi, itasaidia kupunguza matumizi ya umeme kwenye grid ya Taifa. Vifaa vyenye viwango bora vitasaidia kwenye matumizi bora ya nishati, hivyo itatumiwa kwa ufanisi na kupunguza upotevu,” amesema Luoga.

“Kwa kuanzisha maabara hizi, tunategemea wananchi wataweza kutumia vifaa vya umeme vyenye ufanisi na hivyo kupunguza gharama za matumizi ya umeme majumbani,” amesema Luoga.

Pia, Luoga amefafanua kuwa tangu mwaka 2020, megawati 14 za umeme zimepotea kutokana na matumizi ya vifaa visivyokuwa na ufanisi, na Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi bora ya umeme kuokoa umeme unaopotea.

Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya, Marc Stalmans

Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya, Marc Stalmans, amesema kuwa ongezeko la matumizi ya nishati ya umeme miongoni mwa wananchi wa Tanzania limekuwa moja ya sababu kubwa ya kuanzisha maabara hizo, amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya umeshirikiana na Wizara ya Nishati pamoja na TBS ili kuhakikisha kuwa vifaa vya umeme vinavyokwenda sokoni vimepitia vipimo vya ubora.

“Kila siku, idadi ya watu wanaotumia vifaa vya umeme inaongezeka hapa nchini. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha vifaa hivyo vina ufanisi kabla ya kuingia kwa wananchi,” amesema Stalmans.

Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Metrojia wa Shirika laViwangoTanzania(TBS) Ridhiwani Matenge akizungumza na waandishi wa habari leo Octoba 15, 2025 makao makuu ya Shirika hilo jijini Dar es

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Metolojia kutoka (TBS), Ridhiwani Matenge, ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa kusaidia kuanzisha maabara hizo na UNDP kwa kusaidia kufanikisha mradi huo.

“TBS imeongeza ufanisi wake wa kupima ubora na usalama wa vifaa vya umeme. Maabara hizi zitapima friji, mota za umeme, televisheni, kiyoyozi (AC) na fensi za umeme pamoja ma majiko,” amesema Ridhiwani.

Ridhiwani ameongeza kuwa maabara hizo zimejaa vifaa vya kisasa vitakavyowezesha upimaji wa ufanisi wa vifaa vya umeme kabla ya kutumika.

Naye Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi kutoka UNDP, Gertrude Lyatuu, ameeleza kuwa ni jukumu lao kuhakikisha wananchi wanapata maisha bora kwa kuisaidia Serikali ya Tanzania katika masuala ya maendeleo, ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

“Tumekuwa washirika wakubwa wa Serikali ya Tanzania katika masuala mengi ya maendeleo, na sasa tunashirikiana na Wizara ya Nishati na TBS katika kuhamasisha matumizi ya nishati ya umeme,” amesema Gertrude.

Ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuendelea kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na nafuu ili kufanikisha mabadiliko ya kiuchumi na kijamii nchini.