Mahakama yamtupa nje Mpina, ACT-Wazalendo chatoa mwelekeo

Dar es Salaam. Sasa ni rasmi kwa aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha ACT – Wazalendo, Luhaga Mpina kwamba amekosa sifa ya kugombea nafasi hiyo baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo Dodoma, kukubaliana na hoja za Serikali na kuitupa kesi yake huku chama chake kikisema kitakata rufaa.

Pingamizi la Mpina kugombea nafasi ya urais kupitia ACT – Wazalendo,  liliwekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari na Septemba 15, mwaka huu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ilimuondoa mgombea huyo kwenye mbio za urais, baada ya pingamizi hilo kukubaliwa na mahakama.

Hata hivyo, uongozi wa ACT-Wazalendo ulipinga uamuzi huo wa INEC wa kukata jina la Mpina katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kukimbilia mahakamani.

Leo Oktoba 15, 2025,  ACT – Wazalendo kupitia taarifa yake kwa umma imeeleza kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu) Dodoma, imetoa hukumu kwenye kesi hiyo ya kikatiba nambari 24027 ya mwaka 2025 iliyofunguliwa na Mpina na Bodi ya wadhamini ya ACT – Wazalendo dhidi ya INEC.

“Katika hukumu yake ya leo, Mahakama Kuu imetoa maamuzi kwa kujiegemeza kwenye pingamizi za kisheria zilizowekwa na upande wa Serikali juu ya uwezo (jurisdiction) wa mahakama kusikiliza mashauri yanayohusiana na maamuzi ya INEC.

“Tunasikitika kuwataarifu kuwa Mahakama Kuu imekubaliana na hoja za Serikali na hivyo kuliondoa shauri letu mbele ya mahakama,” taarifa ya ACT – Wazalendo imeeleza.

Chama hicho kimesema hata kama mahakama haikusikiliza maombi yao kwa muktadha wake, bado kitaendelea na juhudi za kuitafuta haki na tunu za demokrasia nchini.

“Chama cha ACT – Wazalendo kitachukua hatua baada ya uamuzi huu wa leo, hatua hizo zitajumuisha njia za kisheria ikiwamo kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu, kuwafikia na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, kuendelea kupigania mabadiliko ya kisheria na kikatiba kwenye uchaguzi wetu,” taarifa hiyo imeeleza.

ACT – Wazalendo kimewashukuru wafuasi na wanachama wao  kwa mshikamano na kujitoa kwao wakati wote wa mashauri hayo.

Kimeendelea kuwaomba wanachama wake kubaki kuwa watulivu, wamoja na kuendelea kujielekeza kwenye uwanda mpana wa mapambano ya demokrasia na haki.