BAADA ya kiungo mkabaji, Baraka Majogoro kurejea nchini na kujiunga na kikosi cha KMC alichowahi kukitumikia hapo awali, nyota huyo amesema haikuwa rahisi kuzikataa ofa mbalimbali za timu kutoka ndani na nje ya nchi zilizokuwa zinamuhitaji.
Nyota huyo aliyejiunga na KMC msimu huu baada ya kuachana na Chippa United ya Afrika ya Kusini, alisema kulikuwa na ofa mbalimbali kutoka ndani ya Tanzania na nje ya nchi, japo uhusiano wake na KMC ndio sababu ya yeye kuamua kurejea kikosini hapo.
“Nilikuwa nina ofa nyingi ambazo menejimenti yangu ilikuwa inazifanyia kazi, kiukweli niliamua kufanya uamuzi wa busara wa kurejea KMC baada ya kuonyesha uhitaji na mimi kwa sababu ya uhusiano mzuri niliokuwa nao mwanzoni,” alisema Majogoro.
Akizungumzia ofa aliyopewa na kikosi cha Namungo FC, Majogoro alisema ni kweli mazungumzo yalikuwapo baada ya kuachana na Chippa, japo aliamini kurejea KMC ni bora zaidi kwake kuliko kwenda timu nyingine msimu huu.
“Malengo yangu ni kufanya vizuri msimu huu na kuendeleza kiwango changu bora ambacho mashabiki na wadau wengi wananijua tangu nikichezea hapa, naamini tutafanikiwa kwa sababu kuna vijana wengi wenye kiu na uchu ya kufikia mafanikio zaidi.”
Nyota huyo wa zamani wa maafande wa Tanzania Prisons, Polisi Tanzania, Ndanda na Mtibwa Sugar, alijiunga rasmi na Chippa United, Agosti 4, 2023, akitokea KMC, ingawa msimu huu amerejea tena ndani ya timu hiyo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.