Dar es Salaam. Mjadala kwa sasa ni iwapo Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) inaweza kuakisi imani ya wadau wa uchaguzi, hasa baada ya mabadiliko yaliyofanyika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kadri kampeni zinavyokaribia ukingoni, macho ya Watanzania na wadau wa siasa yameelekezwa kwa tume hiyo, wakiitazama kwa mizani ya matumaini na mashaka yanayotokana na historia ya chaguzi zilizopita.
Wakati INEC ikiendelea kujitambulisha kwa umma na kutoa wito kwa jamii na wanasiasa kuiamini kuwa itahakikisha uchaguzi wa haki na huru, bado maoni juu yake yamegawanyika kwa namna tofauti.
Baadhi ya wadau wanaona mageuzi yaliyofanyika ni hatua muhimu inayorejesha imani katika demokrasia ya Tanzania, huku wengine wakibaki na mashaka kwamba mizizi ya mfumo wa zamani wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijakatwa kabisa.
Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele amekuwa mstari wa mbele kusisitiza kuwa chombo hicho ni huru na kinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Akiwa kwenye majukwaa mbalimbali, Jaji Mwambegele amekuwa akisisitiza umuhimu wa wanasiasa na wananchi kuiamini tume hiyo.
“Wito wetu ni kwamba sisi ni Tume Huru ya Uchaguzi. Wanasiasa watuamini, tutatenda haki; matokeo yatakayopatikana ndiyo yatakayotangazwa, hakuna mtu atakayeonewa,” amesema mara kadhaa mwenyekiti huyo.
Ameendelea kutoa tahadhari kwa wananchi kuepuka kupotoshwa na taarifa zisizo rasmi, akisisitiza umuhimu wa kupata taarifa sahihi kutoka mamlaka husika.
“Yule atakayechaguliwa ndiye atakayetangazwa. Watanzania waachane na upotoshaji wa watu wasio na nia njema; watafute taarifa kutoka vyanzo rasmi,” anasisitiza Jaji Mwambegele katika moja ya mikutano na wadau.
Mabadiliko kutoka NEC kwenda INEC mwaka 2024, yanatajwa kuwa miongoni mwa mageuzi makubwa zaidi katika historia ya siasa za Tanzania tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa mageuzi mengine makubwa, hatua hii imebeba matumaini makubwa kwa upande mmoja na mashaka makubwa kwa upande mwingine. Wachambuzi wa siasa wanatahadharisha kuwa iwapo INEC itashindwa kusimamia uchaguzi kwa haki na uwazi, inaweza kuathiri upya imani ya wananchi kwa taasisi za uchaguzi nchini.
Kwa sasa, kila kauli ya mgombea wa urais imekuwa kipimo cha namna gani wanasiasa wanavyopokea mfumo huu mpya.
Wapo wanaoona INEC kama ishara ya mwanzo mpya wa demokrasia na wapo wanaoamini bado ni kivuli cha NEC kilichovishwa vazi jipya la uhuru.
Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) ni miongoni mwa wadau wanaoona mwanga mpya ndani ya INEC.
Mwongoza kampeni za mgombea urais wa Chaumma, John Mrema amepongeza mwenendo wa tume hiyo katika uratibu wa kampeni za vyama vya siasa zilizoanza Oktoba 28, 2025.
“Kwenye mwenendo wa kampeni mpaka sasa INEC imeonyesha ushirikiano kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo, hatujaona kasoro kama za chaguzi zilizopita,” amesema Mrema ambaye pia ni Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho.
Amesema INEC imekuwa tayari mara kwa mara kuitisha vikao na kushughulikia hoja mbalimbali zinazowasilishwa na vyama, ikiwamo ya mabadiliko ya ratiba za wagombea wa urais na umakamu wa rais.
Hata hivyo, Mrema ametoa wito kwa tume hiyo kuhakikisha usawa na haki katika hatua zilizosalia za upigaji kura na utangazaji wa matokeo.
“Ni imani yetu kuwa watalisimamia hili kwa mujibu wa sheria na kanuni na wanatakiwa kutenda haki kwa wagombea wote,” amesema.
Amesisitiza pia umuhimu wa kurahisisha taratibu za uapishaji wa mawakala wa vyama vya siasa, akibainisha kuwa baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi wamekuwa wakiomba vielelezo vingi ambavyo havimo kwenye kanuni ya sheria ya uchaguzi.
“Kanuni zinataka barua ya utambulisho wa wakala kutoka chama chake, picha mbili na kitambulisho chochote. Lakini wapo wanaoongeza masharti kama hati ya kusafiria au leseni, jambo lisilo sahihi,” amesema Mrema.
Mrema, ametoa wito kwa INEC kuhakikisha elimu kwa wasimamizi wa uchaguzi inatolewa kwa usahihi ili kuepuka makosa yaliyowahi kutokea kwenye chaguzi zilizopita.
“INEC iwaelimishe wasimamizi wa uchaguzi kuhusu kanuni, ili wasije kuharibu uchaguzi katika hatua za mwisho kama ilivyowahi kutokea huko nyuma,” amesema.
Kwa upande wake Gombo Samandito Gombo, mgombea urais es Chama cha Wananchi (CUF), amesema kwa tahadhari: “INEC itaonekana vizuri itakapofika muda wa kutangaza matokeo.”
Kauli hiyo inaakisi maoni wanasiasa wengi wa upinzani wanaoamini kuwa kipimo cha uhuru wa tume hiyo hakitaonekana katika maandalizi au kauli za mwenyekiti wake, bali katika hatua ya mwisho ya utangazaji wa matokeo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima (AAFP), Rashidi Rai, naye amelitazama suala hilo kwa mtazamo wa kijamii zaidi.
“Kwa upande wetu kama chama hatujaona tatizo kutoka NEC kwenda INEC, lakini wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu mabadiliko haya. Wengi ni wasikilizaji tu, hawajui tofauti zake,” amesema.
Rai ameongeza kuwa, japokuwa mabadiliko ya muundo yanaonekana, watendaji wengi bado ni walewale waliokuwa chini ya NEC, jambo linaloleta changamoto ya kuaminika kwa mabadiliko hayo.
Kinyume na mitazamo hiyo ya tahadhari, mgombea urais wa National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Almas anaona INEC kama mwanzo mpya wa demokrasia ya Tanzania.
“Kuna mabadiliko makubwa sana. Hata jina la ‘Tume Huru’ pekee ni hatua, lakini pia wajumbe wake wanapatikana kwa mfumo tofauti na awali na sheria zimeboreshwa zaidi,” amesema.
Almas amepongeza hatua ya Serikali kutoa magari ya kampeni kwa wagombea wote wa urais, akisema ni dalili ya heshima na usawa wa kisiasa unaojengwa upya nchini.
Hata hivyo, ndani ya CUF bado kuna hisia mseto. Husna Abdullah, mgombea mwenza wa urais kupitia chama hicho, anaamini bado uhuru kamili wa INEC haujajitokeza.
“Karatasi ya kupigia kura imeiweka CCM juu, hii inaashiria kwamba bado tume haijawa huru kikamilifu,” amesema Husna.
Kauli yake inafichua hofu ya muda mrefu miongoni mwa vyama vya upinzani kuhusu usawa wa kisiasa katika mchakato wa uchaguzi nchini.
Kwa upande mwingine, mgombea urais wa National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo ameipongeza INEC kwa kusimamia vyema kampeni, lakini akatahadharisha kuwa mtihani mkubwa upo kwenye upigaji kura na kutangaza matokeo.
“Tume imesimamia vizuri kampeni, lakini sasa mtihani ni kura na matokeo. Wakiharibu hapo, hawataaminika tena na chaguzi zijazo hakuna mtu atakayeshiriki,” amesema Doyo.
Ameongeza uhalali wa uchaguzi haupimwi kwa maandalizi, bali kwa matokeo yatakayotangazwa na kukubalika na pande zote.
“Kama wataharibu katika hatua hiyo muhimu ya mwisho, watapoteza imani kwa wananchi na jumuiya za kimataifa,” amesema Doyo.
Wachambuzi wa siasa nao wameendelea kutoa tathmini zao kuhusu utendaji wa INEC. Dk Richard MbundakutokaChuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema uwajibikaji wa kisiasa unatakiwa ubaki kwa waliounda mfumo wa sasa.
“INEC iliundwa kuondoa malalamiko yaliyokuwepo. Iwapo itashindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, Bunge la 12 na aliyekuwa Spika wake wanapaswa kubeba lawama, kwani walipitisha sheria za tume hiyo,” amesema.
Ameongeza kuwa, ubora wa tume huru utategemea zaidi mazingira ya kisiasa yaliyoiunda kuliko jina au sheria pekee.
Kwa upande wake, Profesa Mohammed MakamewaChuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), ameipongeza Serikali kwa hatua ya kuunda INEC kupitia falsafa ya 4R iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akisema ni matokeo ya maridhiano yaliyolenga kuimarisha mfumo wa demokrasia.
“Kwa kupitia 4R za Rais Samia, iliundwa INEC ambayo inalenga kuondoa changamoto zilizokuwapo awali. Ni hatua muhimu ya kurejesha imani ya wananchi kwa njia ya uchaguzi,” amesema Profesa Makame.
Ameongeza kuwa matarajio ya Watanzania katika uchaguzi huu ni kuona tofauti katika usimamizi wa uchaguzi, hususan kupungua kwa kero zilizokuwa zikilalamikiwa miaka iliyopita.
Kwa ujumla, mitazamo hii inadhihirisha kuwa Tanzania ipo katika kipindi nyeti cha mageuzi ya kisiasa.
INEC inabeba mzigo wa historia ya NEC, matumaini ya kizazi kipya cha wapiga kura na tahadhari ya wanasiasa waliopitia changamoto za uchaguzi wa nyuma.
Ni tume itakayopimwa si kwa maneno, bali kwa matokeo yake yatakayoweka rekodi ya kuimarisha au kudhoofisha imani ya wananchi katika demokrasia ya nchi.