Dar es Salaam. Mgombea urais wa Chama cha Democratic Party, Abdul Mluya leo Jumatano Oktoba 15, 2025, akizungumza katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Vingunguti, jijini Dar es Salaam, ametoa ahadi za mageuzi katika sekta mbalimbali akisema analenga kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi.
Akizungumzia mwelekeo wa uchumi atakaoujenga, Mluya amesema serikali yake itakuwa na msukumo wa kipekee wa kujenga uchumi wa kujitegemea.
Gharama za maiti hospitalini hazitakuwa chanzo cha mapato ya serikali, kikokotoo cha wastaafu kitafutwa mara moja na mikopo ya nje itasitishwa.

“Mungu akijalia mkinichagua nikawa rais, itakuwa ni marufuku kugeuza miili ya marehemu hospitalini kuwa chanzo cha mapato ya serikali,” amesema, huku akisisitiza umuhimu wa kuboresha maisha ya wananchi.
Mluya ameongeza kuwa serikali yake pia itaboresha maisha ya wanawake na wajasiriamali wadogo kwa kuhakikisha huduma za kujifungua zinakuwa bure na wanawake waliojifungua wanapatiwa chakula cha lishe kwa afya yao na watoto.
Aidha, Mluya ameweka mkazo kwenye kuondoa changamoto ya ajira kwa vijana, akisema atafumua mfumo wa elimu kuanzia shule ya awali, kubaini vipaji vya watoto mapema na kuendeleza ujuzi wao ili waweze kujiajiri na kushindana kimataifa.
“Tutakuwa na walimu wanaotambua vipaji vya watoto. Serikali itawalea na kuwaendeleza vipaji hivyo ili vijana wetu waweze kujiajiri na kushindana kimataifa,” amesema.
Kuhusu uchumi wa Taifa, Mluya amesema Tanzania haihitaji mikopo ya nje endapo rasilimali za Taifa zitasimamiwa ipasavyo.
“Serikali yangu itasimamia madini, misitu, bandari na rasilimali nyingine. Tukifanya hivyo, tutasitisha mikopo na kila Mtanzania ataweza kupata posho ya Sh100,000 kila mwezi. Hilo linawezekana kabisa,” amesema.
Akizungumzia sekta ya madini, Mluya amesema serikali yake itafuta mikataba yote ya madini na kuanza upya, huku wawekezaji wote wa kigeni watalazimika kuingia ubia na wazawa ili kupata vibali vya uwekezaji.
“Tutafuta mikataba yote ya madini. Kila kampuni ya nje itatakiwa kuungana na Mtanzania kabla ya kupewa kibali. Huu ndio uzalendo wa kweli,” amesema.
Kuhusu vita dhidi ya ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma, Mluya amesema hatua yake ya kwanza akiwa rais itakuwa kufunga mipaka ya nchi kwa muda, ili kufanya ukaguzi wa mali za viongozi na watumishi wa umma.
“Nikiingia Ikulu nitafunga mipaka ya nchi; hakuna kutoka wala kuingia. Tutakaguana kwanza, mali zilizopatikana kwa ufisadi tutazirejesha,” amesema.

Mgombea mwenza wa chama hicho, Saaduni Abdulrahman Saaduni, amewahimiza wananchi wa Segerea na Dar es Salaam kumpigia kura Mluya kwa sababu wote ni wazaliwa wa eneo hilo na wanazifahamu changamoto za eneo hilo vyema.
“Wanasegerea mnabahati, mgombea urais na mgombea mwenza wote ni wa hapa. Tuchagueni tutatatua matatizo yetu wenyewe,” amesema.
Wagombea ubunge na udiwani wa chama hicho kutoka majimbo mbalimbali ya Dar es Salaam pia wametumia mkutano huo kuomba kura, wakiahidi kuboresha huduma za jamii ikiwemo maji, afya na elimu.
Hamis Maganza, mgombea ubunge wa Kivule, amesema atashughulikia changamoto za barabara za eneo hilo, huku Mwanahawa Hussein Guni wa Kisarawe akiahidi kushirikiana na wananchi kutatua changamoto za jimbo hilo.
Christina Paschal, mgombea udiwani wa Magomeni, amesema atasimamia uboreshaji wa huduma za elimu, afya na maji, wakati Enea Alfred Mwakipesile wa Ubungo akiahidi kushughulikia changamoto za kijamii katika kata hiyo.
Wote kwa pamoja wametoa wito kwa wananchi kumpigia kura Abdul Mluya ili kuunda serikali ya mageuzi itakayoleta Tanzania mpya yenye heshima, usawa na ustawi wa kweli.
“Kwa miaka 61 ya uhuru, bado maisha ya Watanzania yamekuwa magumu. Ni wakati wa mabadiliko ya kweli chini ya DP,” amesema mgombea ubunge Segerea jijini Dar es Salaam, Rehema Madongo.