Mbulu. Zaidi ya wanafunzi 2,000 na wakazi wa eneo la Dongobesh wilayani Mbulu, Mkoa wa Manyara, wameanza kunufaika na huduma ya maji safi kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa kisima chenye thamani ya zaidi yaSh100 milioni.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Dongobesh ndio waliojengewa mradi huo, baada ya kupitia changamoto za kiafya kwa kutumia maji machafu ya kisima kwa kunywa.
Neema hiyo ya maji si tu sasa yatawanufaisha wanafunzi hao bali hao wanafunzi wa shule ya msingi jirani pamoja na wakazi,mradi uliofadhiliwa na Shirika la Bridge of Hope kutoka nchini Ujerumani.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Simendu, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuboresha huduma kwa wananchi, hususan kwenye sekta za elimu na maji.
“Shirika la Bridge Hope limekuwa daraja la matumaini kwa wananchi wetu tangu mwaka 2018. Wametujengea madarasa, mabweni, na sasa wametujengea kisima kikubwa chenye uwezo wa kusukuma maji umbali wa kilomita mbili,” amesema Simendu.
Amesema mradi huo wa kisima hautahudumia tu shule ya sekondari na shule ya msingi zilizo jirani, bali pia wananchi wanaoishi katika maeneo ya karibu, jambo litakalopunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi.
“Tumehakikishiwa ushirikiano wa kudumu na tutaendelea kulinda miradi yote ya maendeleo ili idumu na kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, zaidi ya wanafunzi 2,000 wa Shule ya Msingi Lea Pre & Primary English Medium na Sekondari ya Dongobesh watanufaika na mradi huo, unaotajwa pia kuboresha mazingira ya usafi na afya hasa kwa wanafunzi wa kike wakati wa hedhi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Abubakari Kuuli, amesema kabla ya mradi huo wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji, jambo lililosababisha baadhi ya wanafunzi kukosa masomo.
“Kupitia mradi huu, tumeondoa changamoto ya maji kwa jamii na shule zetu. Hii ni hatua kubwa katika kuinua elimu na afya ya wananchi wetu,” amesema Kuuli.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa Sekondari ya Dongobesh, Nice Mollel, amesema ujio wa kisima hicho utasaidia wanafunzi kupata muda zaidi wa kusoma.
“Tulikuwa tunatumia maji ya mtoni ambayo mara nyingi yalituletea maradhi. Sasa tutatumia maji safi kwa kunywa na hata kumwagilia bustani zetu,” amesema.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Nuruana Kipapai, amesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa, hasa kwa wanafunzi wanaotoka mikoa ya jirani wanaosoma shuleni hapo.
Kwa upande wake, mfadhili wa kisima hicho, Arnd Weil na, kupitia taasisi yake ya Bridge of Hope kutoka Ujerumani, wamesema wameguswa na jitihada za jamii hiyo katika kuboresha maisha yao na maendeleo ya elimu.
“Tuliona changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji kwa watoto na jamii. Ndiyo maana tuliamua kusaidia ili kuwapa matumaini mapya,” amesema Weil.
Mradi huo unatajwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility), inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa Dongobesh na kuibua tumaini jipya kwa vizazi vijavyo.