KATIKA hatua hii, Kamba aliwalaumu sana Watanzania kwa kushindwa kujali muda, hatimaye alikata shauri kutafuta usafiri mwingine.
Ghafla mbele yake ilisimama gari aina ya Toyota IST, alishuka mwanamke aliyekuwa akiingia ndani ya Hoteli ya Lambodin.
Dereva aliyemshusha mwanamke huyo alipokuwa akigeuza gari kuondoka Kamba alimpungia mkono na kumuonesha ishara ya kumsimamisha.
“Ni teksi?” alimuuliza.
“Ndio…” dereva alimjibu na kumfanya Kamba kulisogelea gari hilo.
“Nina mizunguko kidogo, nataka kwenda kununua bidhaa Kariakoo, utanidai kiasi gani?” alisema kwa lafudhi ya Kikongo.
“Usijali, hatutashindwana twende tu…” alisema dereva baada ya kunusa harufu ya pesa na kumfanya Kamba kufungua mlango wa nyuma na kuiweka briefcase yake na kutundika koti juu ya siti ya mbele aliyoingia na kuketi.
“Gari yako ina AC?”
“Bila ya shaka,” alijibu dereva na moja kwa moja akaupeleka mkono wake wa kuume na kukibonyeza kitufe na kuwasha kiyoyozi na hewa kutoka katika kiyoyozi kuenea kwa haraka ndani ya gari.
“Asante maana mji wenu huu unanitesa sana kwa joto.”
“Pole sana.”
“Unaijua vizuri Dar es Salaam?” lilikuwa swali lingine lililotoka kwa Kamba kwenda kwa dereva huku akitoa karatasi aliyokuwa ameandika mitaa ya maduka ya jumla aliyotaka kwenda kununua baadhi ya bidhaa.
“Nimezaliwa Ocean Road, hakuna kichochoro cha mji huu kinachonisumbua,” alijibu dereva kwa kujiamini na kumfanya Kamba kuachia tabasamu la matumaini. Kamba aliamini alikuwa amempata dereva mzoefu na anayelijua jiji. Akatokea kumpenda na kumwamini gafla.
“Tuanze na Mtaa wa Livingstone…” alisema Kamba.
***
Wakati dereva aliyezoeana na Kamba aitwaye Mmaka alipokuwa akipiga simu kumfahamisha ameshafika hotelini, Kamba na dereva wake mpya walishafika Kariakoo na Mkongomani huyo alishanunua bidhaa za kutosha.
Baada ya Kamba kufanya manununuzi katika maduka tofauti, dereva mpya alikuwa amemsoma mteja wake alichokuwa akikifanya kabla ya kushuka ndani ya gari na kwenda dukani kununua bidhaa alizokuwa akizitaka.
Aligundua Kamba alikuwa na kiasi kikubwa cha pesa katika briefcase yake zikiwemo noti za shilingi elfu kumikumi za Kitanzania na Dola miamia za Kimarekani.
Kila alipotaka kununua bidhaa alizokuwa akizihitaji, alichokuwa akikifanya Kamba ni kuchota kiasi cha fedha za Kitanzania kutoka katika briefcase yake na kwenda nacho dukani.
Kamba alifanya hivyo mara kadhaa na dereva alifanikiwa kumchungulia kwa kijicho pembe bila ya Kamba kutambua.
Siku zote Kamba alikuwa amejenga imani na Watanzania akiamini ni watu waaminifu na wakarimu sana. Hakutegemea kama kuna siku angeweza kulizwa.
Ni wakati walipofika Mtaa wa Tandamti, Kamba alimuelekeza dereva duka alilokuwa akitaka kuingia ili kununua baadhi na mahitaji yake. Walipokaribia katika duka husika, Kamba akashuka na kumuacha dereva akiendelea na utaratibu wa kuliegesha gari karibu kabisa na duka hilo.
Bila ya wasiwasi Kamba tayari akiwa ameshachota kiasi cha fedha za Kitanzania alimuacha dereva na kuingia dukani kufanya manunuzi.
Ni wakati Kamba alipokuwa akitoka ndani ya duka huku akiwa amebeba kwa mtindo wa kuzipakata bidhaa zake, ndipo alipopigwa na butwaa.
Kamba hakuliona gari katika eneo ambalo lilipokuwa likiegeshwa kabla hajaingia kuingia dukani. Kwa mshangao aligeuka kila upande kutaka kuthibitisha kile alichokuwa akikiona kama kilikuwa sahihi au la.
Hakuyaamini macho yake, mzigo wa bidhaa alizokuwa amezishika ulikaribia kumdondoka, hapo ndipo alipokaribia kupandwa na mizimu ya Kikongomani.
Kila alipogeuka, hakuliona gari wala mfano wa gari alilokuwa amerikodi, alihisi kuanza kuchanganyikiwa.
Hatimaye Kamba aliamini alikuwa amezidiwa akili, alizifikiria bidhaa alizokuwa ameshazinunua tayari na kiasi chake cha pesa kilichokuwa ndani ya briefcase yake aliyoiacha ndani gari.
Kamba alijutia kitendo chake cha kukodisha gari ya mtu asiyemfahamu na alijilaumu kuendeleza utaratibu wake aliokuwa akiutumia wakati alipokuwa akishuka ndani ya gari kwa ajili ya kuingia dukani kununua bidhaa.
***
Muddy Manyara alizaliwa na kukulia Gerezani, jijini Dar es Salaam wazazi wake walikuwa wakimiliki nyumba katika kitongoji hicho kidogo cha kilichopo Kariakoo.
Alipofikisha umri wa kuanza shule ya msingi, Muddy alipelekwa katika Shule ya Msingi ya Kisarawe iliyokuwa hatua chache kutoka katika nyumba waliyokuwa wakiishi.
Yeye na ndugu zake hawakupata tabu ya kulipa nauli ya daladala wala hawakufuatwa na magari ili kufika shuleni, hatua chache za miguu yao zilitosha kuwafikisha katika shule hiyo.
Baada ya kumaliza elimu yake ya msingi na kutochaguliwa kuendelea na shule ya sekondari ya serikali, wazazi wake walimlipia ada na kujiunga na shule ya Sekondari ya Al Haramain, nayo ilikuwa mjini kabisa maeneo ya Shauri Moyo yaliyoitenganisha vitongoji vya Ilala na Kariakoo.
Bado Muddy, hakuhitaji kutafuta usafiri wa kutoka nyumbani kwao ili kufika shuleni alikuwa akitembea ingawaje mwendo ulioongezeka kidogo kufika shuleni ukilinganisha na alipokuwa akisoma shule ya msingi.
Ilikuwa ni baada ya kumaliza kidato cha nne katika sekondari hiyo ya Al Al Haramain, kwa mara nyingine tena Muddy hakuwa amefanya vizuri katika mitihani yake na wazazi wake walitaka kumfanyia mipango aende akasomee kazi ya uaskari au ualimu kutokana na daraja alilopata katika mitihani wake wa mwisho wa kumaliza kidato cha nne.
Muddy angeweza kupata mafunzo katika Chuo cha CCP Moshi mkoani Kilimanjaro na hatimaye angeajiriwa kulitumikia Jeshi la Polisi la Tanzania (PT) lakini alikataa katakata.
Wazazi wake walimsihi sana akubali kujiunga na jeshi hilo kwa sababu walikuwa na uhakika angeweza kuipata nafasi hiyo kutokana na kufahamiana na baadhi ya wakubwa ambao wangeweza kumsaidia na kupata ajira ya uhakika lakini aliwagomea.
Pia, Muddy alikataa kabisa kwenda kusomea ualimu.
“Mtoto wa Mjini hawezi kufanya kazi ya ualimu wala ile ya uaskari, kuna watu na makabila yanayojivunia kufanya kazi hizo, lakini sio Mtoto wa Mjini,” Muddy aliwajibu wazazi wake ambao walijaribu kumsisitiza akubaliane na mawazo yao lakini alipozidi kushikiria msimamo wake waliamua kumuacha aamini kile alichokuwa akikiamini.
***
Baada ya kumaliza shule hakuwa na cha kufanya zaidi ya kugeuka kuwa kula kulala, akiwategemea wazazi wake kama ilivyokuwa desturi ya watoto wengi wa mjini hususan katika jijini Dar es Salaam.
Muddy naye aliingia kwenye mkumbo huo kama ilivyokuwa kwa ndugu zake ambao wote walikuwa wakiwategemea wazazi wao ambao nao walishastaafu katika majukumu yao ya kufanya kazi za maendeleo.
Maisha ya wazazi wao yalikuwa yakiendeshwa kwa pensheni ndogo waliyokuwa wakiipata kutokana na utendaji wao wa kazi siku za nyuma serikalini.
Mbali na kipato hicho, kiasi kingine kilitokana na kodi ya nyumba ambayo baadhi ya vyumba vya mbele ya nyumba yao walivigeuza kuwa sehemu za biashara zilizokuwa zikiendeshwa na wafanyabiashara wa Kihindi.
Kitu pekee alichokuwa akikifanya Muddy ni kucheza mpira na kushinda masikani akipiga stori za hapa na pale na vijana wanzake waliokuwa hawana shughuli kama yeye.
Hapo ndipo zilipozaliwa ndoto za kutafuta maisha bora ya Ulaya na kuwaingia akilini vijana wengi walioamini wangefanikiwa kimaisha kama wangefika katika mojawapo wa nchi za bara hilo.
“Ulaya kazi ziko nje nje sio kama hapa Bongo… kule unaweza kufanya kazi zaidi ya moja kwa siku na ukaingiza kipato cha kutosha tu,” alisema Ally Baga.
“Tena Wazungu hawataki kuwachosha wafanyakazi, wanawalipa vizuri na wanahakikisha wanakula vizuri na wanapata muda wa kupumzika,” aliongeza Baga.
“Kweli, Wazungu wanajali zaidi zaidi afya za watu na usalama katika kufanya kazi, hawatumikishi kama Waswahili, Waarabu au Wahindi na malipo yao ni mazuri,” aliongeza Hamis Sungajao.
“Ndio maana mtu unaweza kufanya kazi zaidi ya sehemu moja kwa siku,” alisisitiza Baga ambaye alikuwa akisikilizwa kwa umakini na watu wengine akiwamo Muddy.
“Pia, unaweza kupata zari ukapendwa na mwanamke wa Kizungu kazi yako itakuwa ni kula kulala…” aliongeza na kuwafanya Muddy na wenzake kulifurahia sana jambo hilo.
Stori hizo za kijiweni ziliwahamasisha vijana hao kutaka kusafiri na kwenda kuishi Ulaya. Walikubaliana kila mmoja wao kuanza kupanga mikakati ya kusafiri na wakahamasishana kila mmoja ahakikisha anamiliki hati ya kusafiria, passport.
“Kuna njia nyingi za kwenda Ulaya, lakini umuhimu ni kuwa na hati ya kusafiria kwanza,” alishauri Baga ambaye ndiye aliyekuwa mhamasishaji mkuu wa jambo hilo.
Baga hakutaka kuwashauri wenzake kutumia njia za panya za kuvuka mipaka kupitia Mtwara na kuingia Afrika Kusini ambako wangelazimika kuzamia meli ili kwenda Ulaya, bali aliwataka kutafuta pesa kwa njia yoyote ili waweze kufika Ulaya kihalali.
Aliwaambia njia ya kuzamia ni ya hatari na sio ya uhakika sana kuweza kufika Ulaya.
“Hata kama mtu anaweza kuwashawishi wazazi wake wakauza nyumba afanye hivyo,” alisema na kuwahakikishia maisha ya Ulaya yatawalipa kwa kila kitu.
Muddy alikuwa mmoja kati ya vijana walioamini maneno ya Baga na kuyapa kipaombele alitamani kufika Ulaya, bara alilokuwa akilisikia lilikuwa na fursa nyingi za ajira na maisha bora ya kifahari.