Mwaijojele aahidi mageuzi makubwa sekta za kilimo, madini na uvuvi

Moshi. Mgombea Urais kupitia Chama cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele ameahidi kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi endapo Watanzania watampa ridhaa ya kuongoza serikali katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.Akizungumza jana jioni oktoba 14, katika mkutano wa kampeni alioufanya uwanja wa stendi ya mabasi Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro Mwaijojele amesema serikali ya CCK itaweka mkazo katika kuboresha sekta za kilimo, madini na uvuvi, ambazo ni nguzo kuu za uchumi wa taifa.“Tutahakikisha watanzania wananufaika na rasilimali zao. Tutaleta nyenzo za kisasa za kilimo, pembejeo zitauzwa kwa bei nafuu, na tutatumia Tehama kuongeza tija katika kilimo,” amesema.Mwaijojele ameongeza kuwa serikali yake itahakikisha inapatikana mitambo ya kisasa ya kuchimba madini, pamoja na vifaa vya kuchunguza madini ardhini ili kusaidia vijana kujua maeneo yenye utajiri huo na kunufaika nao.Katika sekta ya uvuvi, ameahidi kuwekeza kwenye zana za kisasa za uvuvi wa kina kirefu ili kuongeza uzalishaji na kipato cha wananchi wanaotegemea bahari na maziwa.Vilevile, mgombea huyo ameahidi kuwa serikali ya CCK itatoa mikopo bila riba kwa wananchi wote ili kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo, huku akiahidi kukomesha mikopo ya kausha damu aliyodai kwamba inawatesa  watanzania wengi.“Tutakuwa na kamati za wasomi zitakazosaidia kupanga fedha, kuelimisha wananchi juu ya uwekaji akiba, na kutoa mawazo ya kitaalamu yatakayosaidia kuendesha serikali kwa tija,” ameahidi.Akizungumzia masuala ya kijamii, Mwaijojele ameahidi kuwa serikali yake itahakikisha hakuna vijana watakaohangaika mitaani bila ajira, na kwamba maadili yatadumishwa kwa kuhakikisha vijana wanajiheshimu katika mavazi na mienendo.“Kila kijana atakayehitaji kuoa atasaidiwa kugharamiwa harusi yake. Hatutaki kuona kijana yeyote anaishi bila matumaini au bila hela mfukoni,” amesema kwa msisitizo.Kuhusu wazee, amesema watapewa kipaumbele maalumu kama tunu ya taifa kwa kujengewa nyumba na kupewa huduma bora za afya.Aidha, Mwaijojele ameahidi katiba mpya ndani ya muda mfupi baada ya kuapishwa, pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.“Nimeshangaa kufika Moshi kukuta vumbi katikati ya mji. Nikipewa ridhaa, sitaki kuona vumbi tena hapa Moshi,” amesema.Ameongeza kuwa; “CCK tutabadilisha maisha ya Watanzania. Tutahakikisha kila Mtanzania anapata chakula cha kutosha, anashiba na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo,” amesema Mwaijojele.Kwa upande wake, Mgombea ubunge wa chama hicho Jimbo la Moshi Vijijini, Salome Mbilinyi ameahidi kushughulikia changamoto ya miundombinu ya barabara endapo atachaguliwa.Naye mgombea ubunge wa Rombo kupitia chama hicho, Mercy Sandi ameahidi kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika jimbo hilo endapo atapewa nafasi ya ubunge.