NSSF Yaimarisha Ustawi wa Wanachama Kupitia Nishati Safi Mbeya

*Ni kupitia muendelezo wa Awamu ya Pili wa Kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka rangi

Na MWANDISHI WETU,

Mbeya.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Beno Malisa, amewataka waajiri wa sekta binafsi kuhakikisha wanatimiza takwa la kisheria la kuwasilisha michango ya wanachama wao kwa wakati katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili kuendelea kuboresha ustawi wa wafanyakazi wao na kuimarisha huduma za hifadhi ya jamii nchini.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa majiko ya gesi kwa baadhi ya mama na baba lishe, wanachama wachangiaji wa mpango wa hiari na wastaafu wa Mkoa wa Mbeya, yaliyotolewa na NSSF.

Mhe. Malisa alisema hatua ya kuwasilisha michango kwa wakati ni muhimu kwa ustawi wa wafanyakazi. Alisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kutekeleza wajibu wa kisheria na ni sehemu ya kuwajali wafanyakazi, kama wanavyosema NSSF kwamba “wanapaka rangi ustaa wao” kupitia mafao wanayonufaika nayo.

Aidha, Mhe. Malisa aliwahimiza wananchi waliojiajiri, wakiwemo vijana na wajasiriamali wadogo, kujiunga na kuchangia katika mpango wa hifadhi ya jamii wa NSSF ili kunufaika na mafao mbalimbali yakiwemo mafao mbalimbali yakiwemo ya matibabu, uzazi, uzee na mirathi.

Pamoja na hayo, Mhe. Malisa aliupongeza Mfuko wa NSSF kwa kuunga mkono ajenda ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya matumizi ya nishati safi, akieleza kuwa hatua hiyo ni ushahidi wa dhahiri wa dhamira ya Mfuko kugusa maisha ya wananchi kwa vitendo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema utoaji wa majiko hayo ya gesi ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Mfuko ya kurudisha kwa jamii (CSR), ambayo inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kulinda mazingira, kuboresha afya za wananchi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Bw. Mshomba aliongeza kuwa tukio hilo limeenda sambamba na kampeni ya “NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi”, inayolenga kuhamasisha wananchi, hususan waliojiajiri, kujiunga na mpango wa kuchangia kwa hiari, waajiri kuwasilisha michango ya wanachama wao pamoja na matumizi ya mifuko ya TEHEMA.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Tunda, aliishukuru NSSF kwa mchango wake mkubwa katika kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa makundi mbalimbali ya wananchi, hasa wajasiriamali wadogo.

Awali, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. Omary Mziya, alisema Mfuko utaendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujiunga na kuchangia, ili kuhakikisha kila Mtanzania “anapaka rangi ustaa wake” kupitia NSSF.