Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman ameeleza namna alivyojipanga kutengeneza ajira kwa vijana ikiwemo kupitia katika miradi yote inayotekelezwa na Serikali.
Othman amesema sura ya 18 ya ilani ya uchaguzi ya chama hicho, upande wa Zanzibar, imefafanua maeneo tisa ya hatua watakazozichukua za kutengeneza ajira, endapo wakifanikiwa kuingia madarakani.
Ameeleza hayo leo Jumatano Oktoba 15,2025 wakati wa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Wingwi Mapofu wilayani Micheweni kisiwani Pemba katika mwendelezo wa kusaka kura.

Katika ufafanuzi wake, Othman amesema ajira zitatengenezwa kutokana na uwekezaji wa Serikali, ikiwemo uwanja wa ndege bandari na hospitali, lakini vijana wa Zanzibar hawajanufaika.
“Sisi tunasema miradi ambayo Serikali imewekeza itakuwa ya kutengeneza ajira kwa ajili ya watoto, wetu, ndugu zetu Wazanzibari.
“Sera yetu ACT Wazalendo inasema popote Serikali itakapowekeza kama kazi ya kufanya kampuni basi itakuwa kampuni ya wazawa. Kitakachofanyika kutafuta wabia wenye maarifa ili kushirikiana kuifanya kazi hiyo,” amesema.
Othman amesema masharti ya mchakato itakuwa vijana wa Zanzibar kuajiriwa, akisema hali itakuwa hivyohivyo katika mradi wa ujenzi wa bandari na hospitali unaondelea hivi sasa.
“Tutakwenda kuondoa hii mikataba ya kuleta kampuni binafsi kuendesha hospitali zetu, hii jambo la mwanzo nitakalokwenda kudili nalo. Nitaifuta na kurejesha watalaamu wetu kuendesha sekta ya afya.”
“Kwenye miradi yote iliyowekeza itakuwa eneo la kutengeneza ajira kwa vijana wetu, leo kuna sababu gani watoto wetu kukosa ajira,” amesema Othman.

Katika hatua nyingine, Othman amesema chini ya Serikali atakayoiunda mwekezaji yeyote awe wa kudumu au wa muda ikiwemo wa wajenzi wa barabara, sharti la kwanza litakuwa kiwango cha chini cha mtu kulipwa.
“Haiwezakani uwe kwenu upo kwenu ukalipwa ujira wa Sh120,000 ukiangalia bei walizoziweka za kuwalipa mafundi, wafanyakazi au vibarua na mara ya tano wanazowalipa wanaowaajiri.
“Ukipiga mahesabu mishahara iliyowekwa zabuni ni mara tano wanazolipa,zinazobakia zinaishia mifuko, sasa ujinga ujinga sasa basi tutakwenda kuukomesha,” amedai Othman.
Othman amesema chini ya uongozi wake, mkarandarasi yeyote atakayepata zabuni Zanzibar atatakiwa kumuajiri mtu ambaye amepitia katika mfumo maalumu wa soko la ajira la Zanzibar utakaowekwa na Serikali ya ACT Wazalendo.
“Huwezi kutuletea mtu unayemtaka, huyu unayemuajiri tutaweka kiwango cha kulipwa si kwa matakwa ya mtu fulani. Hakuna anayeshindwa na kazi, bali wanashindwa na malipo madogo ya mishahara.
“Ndugu zangu hili nakwenda kulikomesha, ili tupate ajira,” amesema Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT – Wazalendo, Zanzibar, Omari Ali Shehe amesema mikutano ya kufunga kampeni za chama hicho, itafanyika Oktoba 25 uwanja wa Tibirizi Pemba kisha Oktoba 26 watafanya Kibanda Maiti.