Raila Odinga; historia ya Kenya, kielelezo cha demokrasia Afrika

Dar es Salaam. Kijana mwenye umri wa miaka 17, mwenye asili ya Nyanza, Kaunti ya Siaya, nchini Kenya, aliwasili Dar es Salaam, Tanzania.

Alikuwa amezuiwa kuendelea na masomo ya sekondari alipokuwa akisoma Shule ya Juu ya Maranda, iliyopo Siaya. Zilikuwa zama za ukoloni. Dola ya Uingereza (UK) ilikuwa imeiatamia Kenya.

Jamii ya Luo ndiyo asili ya kijana huyo. Kukataliwa kuendelea na masomo Kenya kulikuwa malipo ya gharama ya harakati za baba yake, aliyekuwa mstari wa mbele kupambana kuiondoa dola ya kikoloni Kenya.

Hii ni simulizi yenye umri wa miaka 63. Ilitokea mwaka 1962. Kijana anayebeba uhusika jina lake ni Raila Amolo Odinga, mwana wa Mary Juma Odinga na Jaramogi Oginga Odinga.

Ni zama ambazo hakukuwa na nchi iliyoitwa Tanzania, bali Tanganyika. Uhuru wa Tanganyika ulikuwa bado mbichi na haikuwa Jamhuri, isipokuwa dola chini ya Katiba ya Kifalme.

Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, hakuwa Rais, alikuwa Waziri Mkuu akifanya kazi chini ya Malkia Elizabeth wa Uingereza.

Kupitia kitabu cha maisha yake The Flame of Freedom, Raila anasimulia walivyosafiri kwa gari kutoka Siaya akiwa na wenzake wawili, Oudia Okello na Mirullo Okello. Walipofika Tanzania, walipewa hati za kusafiria za Tanganyika, wakasafiri hadi Cairo, Misri kwa ndege ya Shirika la Ufaransa, kisha Ujerumani Mashariki.

Alipofika Ujerumani Mashariki, alijiunga na Taasisi ya Herder, alikomalizia elimu ya sekondari, kisha alisoma na kuhitimu Shahada ya Uhandisi wa Mitambo, Chuo Kikuu cha Magdeburg kilichopo Magdeburg, Ujerumani.

Aliishi Ujerumani miaka minane, kuanzia mwaka 1962 hadi 1970, kisha alirejea Kenya akiwa ametimiza lengo la msako wa elimu.

Wakati wowote ukisikia Raila anatajwa kuwa raia wa Tanganyika au Tanzania, jibu ni kwamba katika nyakati za ukoloni, ilibidi aazime uraia wa Tanganyika kwa kibali cha Mwalimu Nyerere ili apate hati ya kusafiria ya Tanganyika, akasafiri hadi masomoni Ujerumani akitambulika kama Mtanganyika.

Jumatano, Oktoba 15, 2025, siku moja baada ya kumbukumbu ya miaka 26 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Raila alipata shambulio la moyo akiwa anafanya matembezi mepesi na kufariki dunia. Raila alikuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Koothattukulam, iliyopo Kerala, India, ambako ndiko alikokutwa na mauti.

Mwaka 1970, Raila alirejea Kenya baada ya kumaliza masomo yake Ujerumani, na mwaka 1974 aliteuliwa kuwa Meneja Mkuu wa Shirika la Viwango Kenya (KBS).

Mwaka 1978 alipanda cheo kuwa Naibu Mkurugenzi hadi mwaka 1982 alipojikuta matatani baada ya jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Daniel Arap Moi, lililofanywa na kundi la askari wa Jeshi la Anga likiongozwa na Hezekiah Ochuka.

Baada ya jaribio hilo kushindikana, Raila alikamatwa akihusishwa na kupanga uasi huo na kufungwa kwa takribani miaka 10 katika vipindi tofauti vya jela, kizuizini na mahabusu. Mateso hayo yakawa mwanzo wa mwelekeo mpya katika maisha yake ya kisiasa.

Alipotoka gerezani, Raila hakujiona kama mhalifu bali kama shujaa wa demokrasia aliyedhamiria kupigania mfumo wa vyama vingi na haki za wananchi. Tangu wakati huo alijipambanua kama kiongozi jasiri na nguzo ya siasa za ushindani nchini Kenya.

Kifo chake kimeacha kumbukumbu ya mwanasiasa aliyejitoa kwa ujasiri, ambaye licha ya kutofanikiwa kushinda urais, alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha misingi ya demokrasia nchini humo.

Mwaka 1994, Raila alipojiunga na Chama cha Maendeleo ya Kitaifa (NDP) kutoka Ford Kenya, ilizaliwa kaulimbiu ya Tinga, kifupi cha Tingatinga.

Awali, Tinga ilikuwa kaulimbiu ya chama, lakini baadaye ikajitengeneza zaidi kama jina la utani la Raila.

Tingatinga huchonga barabara, lakini ikishawekwa lami, huwa haliruhusiwi kupita juu yake maana litaharibu. Kama ilivyo sifa ya jina Tinga, ndivyo ilivyo kwa Raila, amechonga barabara ya siasa Kenya. Amekuwa chemchemi ya demokrasia na ujio wa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Ndani ya miaka 25, aligombea urais mara tano bila kufanikiwa.

Mwaka 1997 lilikuwa jaribio lake la kwanza, na 2022 lilikuwa la tano. Kwa miaka 43 iliyotimia, Raila ni mwanasiasa aliyefanikisha mengi bila kuchoka. Kenya ni bora leo kwa sababu ya huduma alizotoa.

Mwandishi gwiji wa Kenya na Afrika, Profesa Ngugi wa Thiong’o, aliwahi kuandika kuhusu Raila juu ya ujasiri aliouonesha kwa kuvumilia mateso jela kwa ajili ya kupigania mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Ngugi aliandika kuhusu mateso ambayo Raila alipata akiwa gerezani. Alimpoteza mama yake mzazi akiwa nyuma ya nondo na wala hakutetereka.

Mtaalamu huyo wa fasihi andishi duniani aliandika kuwa Raila alipotoka jela hakwenda nyumbani kwake, alimfuata na kumshawishi kuungana naye ili kuendeleza harakati za kupigania mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Ngugi alisema harakati hizo ndizo zilizochochea mabadiliko na Kenya kuupokea mfumo wa vyama vingi vya siasa. Madhumuni ya Ngugi yalikuwa kutaka watu wafahamu kwamba Raila si mtu mwoga, bali mpambanaji.

Kenya ilipofanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza uliohusisha vyama vingi vya siasa mwaka 1992, aliuendea uchaguzi huo kwa tabasamu. Alikuwa mshindi, alifanikisha malengo. Alichonga barabara ya demokrasia inayovutia Afrika na duniani.

Oktoba 1991, Raila alikimbia nchi na kwenda mafichoni Norway baada ya kunusurika kuuawa mara kadhaa.

Alisema Serikali ya Kenya chini ya Moi ilikusudia kumuua ili kumnyamazisha asiendelee kukosoa.

Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika mwaka 1992, Raila hakugombea urais. Alirejea Kenya kutoka uhamishoni Norway na kuungana na baba yake, Jaramogi Odinga, aliyekuwa wa tatu nyuma ya Moi na Kenneth Matiba.

Raila aligombea ubunge Jimbo la Lang’ata na kushinda. Aliliongoza jimbo hilo kwa miaka 20 na hakuwahi kushindwa uchaguzi wa ubunge mara zote alipogombea.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1997, aliposhindwa kiti cha urais, alifanya mapatano na Moi, kisha chama chake cha NDP kikaungana na chama tawala cha Kenya African National Union (Kanu). Baada ya kuungana na Moi, alipanda ngazi mpaka kuwa Katibu Mkuu wa Kanu.

Raila kuwa Katibu Mkuu wa Kanu ulikuwa ushindi mwingine, ulikuwa ushahidi wa nguvu zake kiasi cha kumlazimu Rais Moi kufanya naye mazungumzo na hata kumpokea kuwa Katibu Mkuu wa Kanu, kisha akamfanya kuwa Waziri wa Nishati.

Kwa wananchi wa Nyanza, eneo analotokea Raila, kwa miaka mingi lilikuwa halina maendeleo na kukosa huduma za msingi kutoka serikalini kutokana na siasa za upinzani za Jaramogi (baba yake) na Raila mwenyewe.

Nyanza iliwakumbatia Jaramogi na Raila, na kwa kitendo hicho pamoja na siasa za ukabila Kenya, Moi akaamua kulitenga eneo hilo. Baada ya Raila kuungana na Moi, Nyanza ilianza kupata maendeleo na huduma nyingi kutoka serikalini.

Uchaguzi Mkuu wa 2002, wengi walidhani Moi angempigia chapuo Raila kuwa mrithi wake, lakini kinyume chake alimchagua Uhuru Kenyatta.

Raila aliungana na wanasiasa wengine wakubwa wa Kanu kumsusia Moi na Uhuru wake. Wakaanzisha ushirika wa kisiasa wa National Rainbow Coalition (NARC).

NARC walimteua Mwai Kibaki kuwa mgombea urais. Raila aliibeba tiketi ya Kibaki na kuzunguka Kenya nzima akiomba achaguliwe dhidi ya Uhuru.

Alifika Mlima Kenya, nyumbani kwa Uhuru na Kibaki, akawaeleza kwa nini Kibaki na si Uhuru.  Wananchi waliitikia, Kibaki alishinda. Si hivyo tu, Kanu iliondoka kwenye uongozi wa siasa za nchi na kikageuka kuwa chama cha upinzani.

Kitendo cha kuiangusha Kanu na Moi, kisha kumwingiza madarakani Kibaki, kilitafsiriwa kama ushindi mkubwa kwa Raila.

Makubaliano yaliyounda NARC mwaka 2002 yalijengwa juu ya sharti kuwa kama Kibaki angeshinda urais, angemteua Raila kuwa Waziri Mkuu.

Kibaki hakutekeleza hilo, alimfanya Raila kuwa Waziri wa Barabara, Ujenzi wa Umma na Nyumba.

Raila aliihudumia wizara hiyo kwa miaka miwili na miezi 10. Baada ya hapo alisimama kama mpinzani halisi, chanzo kikiwa mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2005.

Raila aliona mabadiliko hayo hayakuwa na tija kwa Kenya.

Ndani ya Bunge la Katiba, alishiriki kuzaliwa kwa vuguvugu la Orange Democratic Movement (ODM) lililopinga rasimu hiyo.

Serikali ya Rais Mwai Kibaki iliongoza kampeni ya “Ndiyo,” huku Raila na ODM wakipigia debe “Hapana.”

Kura ya maoni ya Novemba 21, 2005 ilimalizika kwa asilimia 58.35 ya Wakenya kupinga, hivyo rasimu hiyo haikupitishwa.

Baada ya kushindwa kwa mabadiliko hayo, ODM ilisajiliwa kama chama cha siasa na Raila akawa kiongozi wake. Kutokana na tofauti na Kibaki, aliondoka Baraza la Mawaziri na kuongoza upinzani.

Uchaguzi Mkuu wa 2007 uliokuwa na ushindani mkali kati ya Kibaki na Raila uliishia katika vurugu na vifo baada ya kila upande kudai ushindi.

Hali hiyo ilisababisha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuingilia kati chini ya usuluhishi wa Rais Jakaya Kikwete.

Matokeo yake, Kibaki aliendelea kuwa Rais na Raila akawa Waziri Mkuu wa kwanza katika historia ya Kenya.

Machafuko ya 2007/2008 yaliweka msingi wa Katiba mpya ya mwaka 2010 iliyoongeza uwajibikaji na uhuru wa taasisi.

Raila alihusishwa na mafanikio hayo kama mpigania demokrasia. Katiba hiyo iliruhusu Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2017, kesi iliyowasilishwa na Raila kupinga ushindi wa Uhuru Kenyatta.

Katika maisha yake ya kisiasa, Raila alifanya maridhiano na marais wote, Moi, Kibaki, Uhuru na Ruto akiweka alama ya umoja na upatanisho.

Wakenya wanamuita “Baba” au “Tinga,” majina yanayoakisi heshima kwake.

Mwaka 2024 alijaribu kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika bila mafanikio.