Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasiasa mashuhuri na kinara wa upinzani na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga aliyefariki dunia leo Jumatano Oktoba 15, 2025.
Odinga maarufu ‘Baba’, amefariki akiwa na umri wa miaka 80 katika Hospitali ya Macho ya Sreedhareeyam Ayurvedic huko Kerala nchini India, baada ya kupata shambulio la moyo.
Odinga alipatwa na mshtuko wa moyo wakati akifanya mazoezi ya kutembea asubuhi kwenye viunga vya hospitali hiyo alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kupitia mitandao ya kijamii ya Rais Samia amesema; “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga. Tumempoteza kiongozi mahiri, Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Msiba huu si wa Kenya pekee, bali wetu sote.

“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatuma salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Dk William Samoei Ruto, Mama Ida Odinga, watoto, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Kenya kwa msiba huu.
“Tunaungana kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajaalie subira, faraja na imani katika kipindi hiki na ailaze roho ya mpendwa wetu, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, mahali pema peponi,” ameandika Rais Samia.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amesema: “Nimehuzunishwa sana na kifo cha rafiki yangu mpendwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Mheshimiwa Odinga. Alikuwa mwanasiasa hodari na rafiki mpendwa wa India. Nilikuwa na pendeleo la kumjua kwa karibu tangu siku zangu nikiwa Waziri Mkuu wa Gujarat na ushirika wetu uliendelea kwa miaka mingi.

“Alikuwa na mapenzi maalumu kwa India, utamaduni wetu, maadili na hekima ya kweli. Hii ilionekana katika juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa India na Kenya. Alipendezwa sana na Ayurveda na mifumo ya dawa za jadi za India, baada ya kushuhudia athari zake chanya kwa afya ya binti yake. Natuma rambirambi zangu kwa familia yake, marafiki na watu wa Kenya katika saa hii ya majonzi.”
Kiongozi mwingine wa Kenya, Righathi Gachagua amesema; Baba Raila Odinga, upumzike vyema. Kwa familia, mwenzi wako Mama Ida Odinga na watoto wako, familia yangu na mimi tunaungana nanyi katika maombi katika wakati huu mgumu. Pole zangu nyingi kwako na kwa watu wa Jamhuri ya Kenya.

“Alijitolea maisha yake katika huduma ya ubinadamu: kama mwanaharakati wa kisiasa, mtumishi wa umma, mhadhiri wa chuo kikuu, mbunge, kiongozi wa chama, waziri wa baraza la mawaziri, waziri mkuu na nyanja nyingine nyingi. Juu ya haya yote, njia yako ya mafanikio na athari inabaki kuwa isiyofutika.”
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema ameandika kuwa amesikitishwa na kifo cha Odinga. “Tunatuma rambirambi zetu kwa watu wa Kenya, familia ya Odinga, Rais, William Ruto na wote walioguswa na mtetezi huyu mkuu wa demokrasia. Urithi wake utadumu. Apumzike kwa amani ya milele.”

Kiongozi wa upinzani wa Uganda, Bobi Wine ameandika pia kwenye akaunti yake ya mtandao wa X kuwa; “Tumepokea taarifa za kifo cha Raila Odinga kwa masikitiko makubwa. Alisimama kidete kwa ajili ya uhuru na heshima. Ndani yake, tumempoteza mwanasiasa mkubwa, jitu la Kiafrika, ambaye alifanya bora yake kwa ubinadamu katikati ya shida kubwa. Rambirambi nyingi kwa watu wakuu wa Kenya na vikosi vyote vya demokrasia kote ulimwenguni. Roho yake ipumzike kwa amani.”