Kagera. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi akipewa ridhaa ya kuongoza nchi kwa kipindi kijacho, Serikali itaimarisha huduma za jamii mkoani Kagera, sambamba na kuboresha usafiri wa majini, huduma za afya, maji na sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji.
Ahadi hizo amezitoa leo Jumatano, Oktoba 15, 2025 na mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan alipokuwa mkoani Kagera baada ya kumaliza kampeni mkoani Geita.
Amesema Serikali itakayoundwa na CCM itaweka mkazo katika kuinua huduma za kijamii hususan wilayani Muleba kwa kununua boti tano, mbili kwa ajili ya kubeba wagonjwa na tatu kwa ajili ya doria za usalama na kudhibiti uvuvi haramu unaochangia kupungua kwa samaki Ziwa Victoria.
“Miongoni mwa ahadi zetu, mkitupa ridhaa hapa Muleba, ni kuleta boti mbili zitakazotumika kusafirisha wagonjwa kutoka kata za Goziba na Bumbire, pamoja na kujenga gati mbili katika vijiji husika ili kurahisisha upakiaji na upakuaji wa abiria na mizigo,” amesema Samia.
Ameongeza kuwa, boti tatu za doria zitaimarisha ulinzi na kudhibiti uvuvi haramu, huku Serikali ikiwekeza zaidi katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili vijana wapate ajira na kuongeza uzalishaji wa mazao ya samaki.

Kuhusu huduma ya umeme, Samia amesema Serikali itakamilisha mradi wa kituo cha kupokea umeme eneo la Ilemela ambao umefikia asilimia 85 ya utekelezaji.
“Ujenzi wa kituo hicho utasaidia kuondoa tatizo la upungufu wa umeme katika baadhi ya visiwa na vitongoji vya mkoa huo,” amesema mgombea huyo.
Pia, amegusia changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama, hasa wilayani Muleba, ambako wananchi wanategemea mito na visima visivyo na uhakika wakati wa kiangazi.
Samia amesema Serikali imeshakamilisha usanifu na upembuzi yakinifu wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria utakaogharimu Sh39.3 bilioni na kuwanufaisha wanufaisha wakazi wa Muleba na wilaya jirani.
“Nina furaha kuwajulisha kuwa wizara ya maji ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi huu, ambao utamaliza kabisa tatizo la maji katika maeneo haya,” amesema Samia.
“Mungu ametupa maziwa haya makubwa ni jukumu letu kuhakikisha wananchi wananufaika kwa kupata maj safi na salama.”
Katika sekta ya kilimo, mgombea huyo amesema Serikali ya awamu iliyopita ilianzisha mashamba ya migomba na kahawa likiwamo la ekari 300, ambalo vijana 300 kupitia Programu ya Boresha Kesho Yako (BBT), wanaendeleza uzalishaji.
Aidha, amesema Serikali ilitoa zaidi ya Sh3 bilioni kujenga soko la mazao ya uvuvi na iwapo CCM itapewa ridhaa kuendelea kuongoza, itapanua mpango huo kwa kuanzisha viwanda vya usindikaji wa mazao ya uvuvi ili kuongeza thamani ya mazao na kipato kwa wavuvi.
“Tunataka kuona wavuvi wanapata manufaa zaidi kupitia usindikaji na kuuza mazao yao kwa bei bora. Pia tutaongeza boti za kisasa za uvuvi zitakazotolewa kwa mikopo nafuu,” amesema.
Kwa upande wa kahawa, Samia ameahidi Serikali itaendelea kuongeza uzalishaji wa miche bora, kuwawezesha wakulima kupata trekta na kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Amesisitiza kuwa, CCM itatekeleza kwa vitendo ilani yake ya mwaka 2025/30, ikilenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwekeza katika sekta zinazogusa moja kwa moja ustawi wao.

“Kagera mnafahamika kwa uchapazi kazi wenu, hususan katika kilimo cha kahawa, migomba, uvuvi na ufugaji. Ndiyo maana miaka mitano iliyopita tulielekeza jitihada zetu katika kuzikuza sekta hizo za uzalishaji, bila kusahau ujenzi wa miundombinu na huduma za jamii,” amesema Samia.
Amesema CCM kwa ujasiri mkubwa imerejea mkoani humo kuomba ridhaa ya wananchi kuendelea kuongoza nchi, ikiahidi kusimamia maendeleo yaliyofikiwa pamoja na kuendeleza miradi iliyotekelezwa katika awamu iliyopita.
“Tumerejea kwenu kwa ujasiri mkubwa kuomba ridhaa ya kuendesha Serikali, kusimamia nchi hii na kuendeleza tuliyofanya miaka mitano iliyopita, ikiwamo kumaliza mgogoro kati ya wakulima na wafugaji katika vitalu viwili uliodumu kwa miaka 17,” amesema Samia.
Aidha, ameahidi kuboresha kitalu kimoja kikubwa cha halmashauri kupitia programu ya BBT kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe ili vijana waendelee kunufaika kiuchumi.
Pia, ameeleza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali iliboresha mfumo wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri na hadi sasa, vikundi 152 vimenufaika na mikopo yenye thamani ya Sh2.2 bilioni, hatua iliyosaidia kuongeza kipato kwa wananchi.
Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema Kagera ni mkoa wa tisa kuambatana na mgombea huyo wa CCM katika kampeni, na kwamba mapokezi makubwa wanayoyapata kila wanapopita ni uthibitisho wa imani na matumaini makubwa waliyonayo Watanzania kwa mgombea huyo.
“Samia ni kiongozi ambaye akiahidi anatekeleza. Mfano ni maendeleo ya Mkoa wa Kagera unaounganishwa na mikoa ya kanda ya ziwa kupitia miradi mikubwa kama Daraja la Kigongo–Busisi, ambalo kukamilika kwake kunachochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huu,” alisema Dk. Bashiru.
Aliongeza kuwa kufikia mwaka 2030, Kagera itakuwa miongoni mwa vituo vikuu vya uwekezaji, biashara na uzalishaji nchini, kutokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayoendelea.
Dk Bashiru pia amebainisha kuwa awali, Kagera na mikoa ya mipakani ilikuwa inakabiliwa na changamoto za kiusalama, lakini sasa hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.
“Miaka ya nyuma, haikuwa rahisi kusafiri usiku katika maeneo haya bila ulinzi wa askari. Leo Kagera na mipaka yake ni salama, ujirani mwema tunaendeleza na tunapochagua CCM tunajua tunachagua amani na usalama wa kudumu,” amesema.
Ameongeza kuwa, sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji zinaendelea kukua, huku bei ya kahawa iliyokuwa imeshuka miaka michache iliyopita sasa ikiimarika, hali inayowahamasisha wakulima wengi kurejea kulima kwa wingi.
Awali, Ezekiah Wenje aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho ambaye hivi karibuni amejiunga na CCM, amesema kiongozi bora ni yule anayewapa watu matumaini.
“Nilichojifunza duniani ni kuwa wajibu mkubwa wa kiongozi ni kuwapa matumaini watu anaowaongoza. Mambo yaliyosemwa hapa leo yanawapa Watanzania na wananchi wa Kagera matumaini kwamba kesho yao ni bora kuliko leo,” amesema Wenje.
Amefafanua kuwa tangu Samia aingie madarakani, amekuwa kiongozi anayesikiliza, akiwakumbatia wote wakiwamo waliokuwa wapinzani, kwa kuwa aliwahi kuwaita mezani kujadiliana masuala ya kitaifa, ikiwamo kuwaruhusu waliokuwa wamekimbia nchi kurejea bila masharti, pamoja na kuachiliwa kwa waliokamatwa baada ya uchaguzi wa 2020.
“Tuliomba mikutano ya hadhara ifunguliwe, jambo ambalo lilitimizwa. Kwa bahati mbaya, baadhi yetu tukaanza kukutukana badala ya kushukuru. Tulipendekeza pia marekebisho ya sheria za uchaguzi na suala la wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi na marekebisho hayo sasa yamefanyika. Huu ni ushahidi kuwa Samia akiahidi, anatekeleza,” amesema Wenje.
Ameongeza kuwa, ni hatari kuongozwa na viongozi wasiokuwa na ujasiri, akisisitiza, “Mungu hafanyi kazi na waoga na kwamba, uongozi wa kweli unahitaji uthubutu na imani, si maneno ya kujitapa bila vitendo.
“Ni hatari kuwa na viongozi wanaosema wako tayari kufa, wakati hata Yesu aliomba kama inawezekana kikombe cha kifo kimuepuke. Kiongozi jasiri ni yule anayechagua uhai, matumaini na maendeleo ya watu wake,” amesema Wenje.