Karagwe. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendeleza mapinduzi ya maendeleo katika Wilaya ya Karagwe kupitia maeneo manne ambayo ni huduma za kijamii, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, ukuaji wa sekta za uzalishaji, na uboreshaji wa miundombinu.
Akihutubia maelfu ya wananchi wa Karagwe, leo Jumatano Oktoba 15,2025, Samia amesema Serikali yake imejipanga kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote bila kubagua, huku akisisitiza kuwa safari ya maendeleo ni hatua endelevu.
Samia amesema katika sekta ya afya, Serikali imepiga hatua kubwa kwa kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati, huku ikihakikisha dawa muhimu zinapatikana kwa kiwango cha juu.

“Kitaifa, upatikanaji wa dawa muhimu upo asilimia 86. Hatujafika asilimia 100, lakini tulipofikia si haba. Tutaendelea kuboresha huduma za afya hadi kila Mtanzania awe na uhakika wa matibabu bora karibu yake,” amesema.
Kuhusu elimu, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kujenga miundombinu ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ufundi ili vijana wapate ujuzi na ajira.
Samia ameongeza kuwa Serikali inapanua mfuko wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ili vijana wote wanaomaliza kidato cha sita wapate nafasi ya kuendelea na masomo bila kujali hali ya kiuchumi ya wazazi wao.
Kuhusu maji, amesema Serikali imetenga mabilioni ya fedha kupeleka maji safi na salama kwa wananchi, huku ikijenga skimu za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara.
“Sasa maji si kwa matumizi ya nyumbani pekee, bali pia kwa kilimo. Tunataka wakulima wazalishe mara mbili kwa mwaka, tuwe na chakula cha kutosha na kukuza kilimo biashara,” amesisitiza.
Kwenye nishati, Rais Samia amesema lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata umeme unaotokana na vyanzo safi.
“Tumepeleka umeme vijijini hadi vitongojini. Lengo letu ni kila Mtanzania atumie nishati safi ya umeme. Hii ni huduma muhimu, ni usalama, ni biashara, ni maendeleo,” amesema huku akipigiwa makofi na wananchi.
Samia ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutoa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo ili kupunguza gharama kwa wakulima.
“Bila ruzuku, wakulima wasingenunua mbolea nyingi, mavuno yangekuwa kidogo. Sasa tunawatoza nusu ya bei, wanapata mbolea nyingi, wanavuna zaidi na kuuza zaidi. Hii ndiyo maana halisi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi,” amesema.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kutoa mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, Tasaf na mifuko mingine ya uwezeshaji wananchi.
“Tunajenga stendi na masoko kwa sababu huko kuna fursa za biashara. Mtu akipata mtaji wa kufanya biashara, tunakuwa tumemwezesha kiuchumi,” amesema Rais Samia.
Ametaja pia hatua za Serikali za kuwasaidia wafugaji kwa kutoa chanjo kwa bei nafuu na kuku bure, huku wakulima wa kahawa wakinufaika na kuondolewa kwa tozo zilizokuwa zikiwapunguzia kipato.
“Sasa mkulima wa kahawa anapokea malipo yote mfukoni bila makato. Tutaendelea kuangalia maeneo yote tunapoweza kutoa ruzuku zaidi,” ameahidi.
Mgombea huyo amesema Serikali inaendelea kujenga uchumi imara unaotegemea sekta za kilimo, viwanda, na miundombinu.
“Barabara, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa maji ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Tunajenga barabara za lami, tunaboresha bandari ya Kemondo na Bukoba ili kukuza biashara na usafirishaji,” amesema.
Kuhusu viwanda, Samia amesisitiza kuwa ilani ya CCM inaelekeza kujenga kongani za viwanda kila wilaya ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na wavuvi.
“Tunasaidia wavuvi kwa mikopo ya vizimba na boti. Tunataka samaki wazalishwe zaidi, wachakatwe hapa nchini na kuuzwa nje kupitia ndege za mizigo za ATCL,” amesema.
Aidha, aliahidi kufufua viwanda vya kuchakata kahawa ili kuongeza thamani ya zao hilo kabla ya kuuzwa nje.
“Tusiuze kahawa ghafi. Tuitengeneze, tuiuze ikiwa imeongezwa thamani. Hapo ndipo kipato cha mkulima kitaongezeka,” amesisitiza.
Samia amesema Serikali itashughulikia maombi yaliyotolewa na wananchi wa Karagwe, ikiwemo ujenzi wa stendi na masoko mapya, pamoja na ujenzi wa vyumba vya baridi (cold rooms) kwa ajili ya kuhifadhi mazao kama parachichi.
“Tumeweka mpango wa kujenga vyumba vya baridi nchi nzima, hasa kwenye mikoa ya kati kunakolimwa parachichi, ili mazao yasiharibike,” amesema.
Samia aliwaomba wananchi wa Karagwe kuendelea kuiamini CCM ili iweze kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne iliyopita.
“Tumefanya vizuri. Tukipewa ridhaa tena, tutaendelea kufanya vizuri zaidi,” amesema huku umati wa wananchi ukishangilia.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Ngara mkoani Kagera,Dotto Bahemu akiomba kura leo Jumatano Oktoba 15,2025 wilayani Karagwe mkoani Kagera kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa chama hicho,Samia Suluhu Hassan.
Awali mgombea ubunge wa jimbo la Ngara, Dotto Bahemu amesema katika sekta ya afya wakati Samia anaingia madarakani jimbo hilo lilikuwa na hospitali moja ya wilaya ambapo wananchi wengine walikuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 100 kufuata huduma ya afya, ila Samia akiwa Rais amepeleka Sh2 bilioni kwa ajili ya hospitali nyingine ya wilaya ambayo inaendelea na ujenzi ,huku baadhi ya huduma zikiwa zimeanza.
“Aidha umetupa vituo vitatu vya afya ambapo zaidi ya Sh3 bilioni zilitumika na zahanati zikiongezeka kutoka 45 wakati unaingia madarakani sasa ina zahanati 50.Jimbo lilikuwa na shule za sekondari 25 sasa hivi ziko 31 ambapo zaidi ya Sh7.9 bilioni zimetumika na shule za msingi zimeongezeka pia,”
“Sisi watu wa Ngara tunajitambua hatuko tayari kushikiwa akili na mtu yoyote kwa ajili ya kutuambia tuende tukafanye nini tunachotaka kukiamua sisi tunakijua wenyewe aina ya kiongozi tunayemtaka ni ambaye ametuthibitishia pasi na shaka katika kipindi kilichopita kwa yale ambayo ametufanyia, pamoja na ahadi zinazoleta matumaini kwa miaka mingine mitano ijayo.
“Na siyo mwingine ni Samia kwa hiyo hatuko tayari kufanya uamuzi mwingine zaidi ya kumchagua Samia ,tunatuma salamu kwenda pande zote za dunia kwamba aina ya kiongozi tunayemtaka ni Samia ambaye ndani ya kipindi cha miaka minne akiwa madarakani amekuta jimbo la Ngara tukiwa na shida mbalimbali ametupa Sh81 bilioni kutekeleza miradi ya maendeleo,”amehitimisha Bahemu.