Selemani Kidunda Apata Cheti cha Ukocha wa Ngumi ya Kimataifa – Global Publishers



Bondia maarufu wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania, Selemani Kidunda, ameongeza hadhi nyingine katika taaluma yake ya michezo baada ya kuhitimu rasmi kozi ya ukocha wa mchezo wa ngumi.

Kidunda sasa ni kocha wa kimataifa wa ngumi mwenye hadhi ya daraja la nyota moja (One Star International Coach), cheo kinachomtambua kama kocha mwenye sifa za kufundisha ngumi katika mataifa yote duniani.

Kozi hiyo ilifanyika kwa njia ya mtandao (online) chini ya uratibu wa Shirikisho la Kimataifa la Ngumi (IBA) kuanzia Julai 28 hadi Agosti 6, mwaka huu (2025).

Katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa wahitimu wa kozi hiyo, iliyoratibiwa na Shirikisho la Ngumi la Taifa (BFT) kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kidunda alipokea cheti chake rasmi kama ishara ya kukamilisha mafunzo hayo kwa mafanikio.

Selemani Kidunda ni miongoni mwa wanamasumbwi waliowahi kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa, ikiwemo Michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012, kabla ya kuingia kwenye ngumi za kulipwa.