Serikali yaanza kufukua Mto Morogoro

Morogoro. Shangwe, furaha na vifijo vimetawala katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Mambi baada ya Serikali kununua skaveta mpya yenye thamani ya Sh360 milioni, ambayo itaanza kazi ya kufukua mto Morogoro ulioacha njia yake ya asili kwa zaidi ya miaka minane.

Mto huo umekuwa ukisababisha mafuriko, kuharibu nyumba na kuathiri maisha ya wakazi wa maeneo jirani kipindi cha mvua.

Akizungumza leo Oktoba 15, 2025 mjini hapa, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema Serikali imesikia kilio cha wananchi na kuamua kununua skaveta hiyo mpya ambayo imekabidhiwa rasmi Bodi ya Bonde la Wami-Ruvu.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Mambi kuhusu suluhisho la mto Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

“Serikali imenunua mtambo mpya (skaveta) kwa thamani ya Sh360 milioni na imekabidhiwa rasmi kwa Bodi ya Bonde la Wami-Ruvu. Tunalenga kutatua changamoto za mito ya Ngerengere, Wami, Mgeta na Ruvu pale zinapobadilisha njia zao asili na kuleta mafuriko katika makazi ya wananchi,” amesema Kilakala.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mambi, Hamad Salum Hamad, amesema tatizo la mto Morogoro kuacha njia yake ya asili lilianza kuonekana mwaka 2017 na kuwa mbaya zaidi mwishoni mwa mwaka jana ambapo maji yaliingia kwenye nyumba zaidi ya 100 na watoto kushindwa kwenda shule.

“Tumeonyesha shangwe na tumepiga vigeregere kwa sababu Serikali imesikia kilio chetu. Sasa tuna imani mto utarejea katika njia yake ya asili na tutalala salama,” amesema Silon Wahindi mkazi wa mtaa huo.

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Mambi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya katika mkutano wa kutatua changamoto za mto Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

Mhandisi wa Maji kutoka Bodi ya Bonde la Wami-Ruvu, Nangu Makula, amesema bodi inahakikisha maji yanapita katika mito bila kuathiri makazi ya wananchi.

“Mto Morogoro unamwaga maji katika Mto Ngerengere na kuingia Mto Ruvu. Leo tumeanza kuurejesha kipande chote cha mtaa wa Mafisa ili wananchi wakae kwa amani na utulivu,” amesema Makula.