Shauri la Polepole mapya yaibuka, Ofisa wa Polisi atajwa mahakamani

Dar es Salaam. Mambo mapya yameibuka katika shauri la kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, baada ya mawakili wake kuiomba Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam iridhie kupokea ushahidi wa mdomo wa Christina Polepole, ambaye ni dada wa Humphrey.

Maombi hayo yametolewa leo Oktoba 15, 2025 na Peter Kibatala, kiongozi wa jopo la mawakili wa Polepole wakati shauri lilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.

Shauri hilo la maombi namba 24514/2025 linalosikilizwa na Jaji Mfawidhi, Salma Maghimbi, lilifunguliwa na wakili Kibatala kwa niaba ya Polepole, Oktoba 7, 2025, chini ya hati ya dharura, dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na wenzake.

Wajibu maombi wengine kwa mfuatano ni  Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polis Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC).

Wakati shauri lilipotajwa, Kibatala akishirikiana na mawakili Faraji Mangula na Gloria Ulomi, ameieleza mahakama kuwa leo asubuhi amepata taarifa kutoka kwa Christina, dada wa Polepole ambazo ni muhimu mahakama kuzifanyia kazi.

Amesema Christina amemweleza kuwa Julai 17, 2025 aliwekwa chini ya ulinzi na maofisa wa Polisi nyumbani kwake Bahari Beach, Dar es Salaam, wakiongozwa na Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam (DZCO), George Byagemu (Bagyemu).

Amesema Christina amemweleza alipigwa na maofisa hao wa Polisi wakiongozwa na Byagemu na walimuhoji kuhusu alipo Balozi Polepole.

“Maoni yetu ni kwamba taarifa hiyo ina value (thamani) katika kutoa uamuzi wa maombi yaliyoko mbele ya mahakama, hasa kwa kuzingatia taarifa zilizotajwa katika viapo kuhusu wapi alipo na nani wanaomshikilia,” amesema Kibatala.

Amesema kifungu cha 413(2) cha CPA kinaipa mahakama mamlaka ya kuratibu mwenendo wake katika mashauri kama hayo ili kufikia haki na kwamba, kifungu cha 416(1) kinaipa mahakama mamlaka ya kupokea maombi kwa mdomo au kwa maandishi. Amesema wao wanatoa maombi hayo kwa mdomo.

Wakili Kibatala amesema kwa kuwa hakuna ubishi kuwa kiapo ni ushahidi na kwa kuwa tayari kuna ushahidi kwenye kumbukumbu, mahakama ina mamlaka ya kupokea ushahidi wa ziada.

Kibatala amesema kwa kuwa shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura wanaomba mahakama iridhie kupokea ushahidi wa mdomo wa Christina, kuhusu eneo hilo chini ya kiapo, kwa kuwa litasaidia kupata ukweli.

Akijibu ombi hilo, Wakili wa Serikali, Ayoub Sanga amesema wanapinga maombi hayo kwa kuwa yaliyoko mahakama yamewasilishwa chini ya hati ya dharura na  kuonyesha udharura wenyewe mahakama imelipa uzito suala hilo.

Amedai Oktoba 9, 2025 wakili wa mwombaji aliomba kuwasilisha kiapo cha ziada na hawakupinga kwa sababu alieleza kuna taarifa ambazo familia wanapaswa kumpa.

Sanga amedai leo Oktoba 15, wakili wa mwombaji baada ya kusoma viapo vyao kinzani vilivyowasilishwa mahakamani ndipo anakuja na maombi kuwa kuna taarifa anataka aiongeze, ambayo alikuwa nayo miezi mitatu nyuma.

“Kwa hiyo, kwa upande wetu tunaona kuna nia ya wazi ya wenzetu kutaka kuchelewesha shauri hili kwa kuwa walipaswa kuwasilisha taarifa zote kwenye kiapo cha ziada,” amesema.

Amesema ingawa wanatambua na kukubali kuwa kifungu cha 413(2) kinaipa mahakama mamlaka ya kuratibu mwenendo wa shahidi kadri inavyoona inafaa na kwamba, chini ya kifungu cha 416(1) (b) ina mamlaka kupokea ushahidi wa mdomo.

Hata hivyo, amesema wanaomba mahakama isitumie mamlaka hayo kwa sababu: Kwanza, ombi lililoletwa halihusiani na shauri na pili, mahakama ili iweze kutumia vifungu hivyo lazima ihakikishe hakuna ukiukwaji haki.

Amesema kama mahakama itamruhusu anayetaka kuleta ushahidi akitoa tuhuma dhidi ya DZCO George Byagemu, yeye hataweza kupata fursa ya kujitetea ili kukinzana na shahidi huyo.

Amesema katika hali hiyo kutakuwa na ukiukwaji haki kwa kuwa kuna mtu hatapata haki ya kusikilizwa kuhusu tuhuma hizo.

Vilevile, amesema Kanuni ya 2 ya Kanuni za Mashauri hayo Tangazo la Serikali (GN) Namba 150 la mwaka 1930, baada ya kuwasilisha kiapo kinachofuata ni kiapo kinzani na kwamba, kama kuna taarifa za ziada zinaongezwa kwa kuwasilisha kiapo cha ziada.

Amedai kama kwenye kiapo kinzani kuna hoja za kujibu, basi upande kinzani unawasilisha kiapo kujibu kiapo kinzani na si utaratibu wa shahidi kutoa ushahidi kwa mdomo.

“Kwa hiyo, tunachokiona mwenzetu baada ya kusoma viapo kinzani vyetu ameona kuna vitu anataka kuviongeza bila kufuata utaratibu,” amedai.

Kwa upande wake, wakili Nguka amedai mahakama inaendeshwa na kanuni na moja ya kanuni hizo ni kila shauri lazima lifikie mwisho.

Amedai maombi yaliyowasilishwa yanafungua milango ya shauri kutokufika mwisho.

“Tunaomba mahakama yako tukufu isiingie kwenye mtego wa kuchelewesha shauri hilo ambalo wamelifungua kwa hati ya dharura. Sisi wajibu maombi tunaogopa mtego huo na tunaomba mahakama yako iendelee na usikilizwaji wa shauri,” amesema na kuongeza:

“Kama wakili anaona bado kuna mambo yanayoendelea anaweza kuliondoa shauri na kwenda kufanya utafiti, akiridhika ndipo arudi kuendelea na shauri.”

Amesema kama mahakama itaona kuna umuhimu wa kupokea ushahidi wa Christina, basi waulete kwa maandishi kupitia kiapo ili nao wapate kukijibu baada ya kukutana na DZCO ili kujiridhisha iwapo Julai 17, 2025 (miezi mitatu) alimuweka chini ya ulinzi.

Amesema haki ya kusikilizwa ni ya msingi ambayo hata Mwenyezi Mungu mwenyewe aliifanya kwa Adamu, japo alijua kuwa ametenda kosa na amejificha bado alimuuliza kuwa yuko wapi na anafanya nini.

“Hivyo, tunaomba maombi haya yatupiliwe mbali ili tuendelee na usikilizwaji wa shauri hili leo ili kuwatendea haki waleta maombi,” amesema.

Wakili Kibatala akijibu hoja kuhusu kiapo cha ziada walichowasilisha awali amesema alikiwekea msingi kuwa taarifa alikuwa amezipata siku hiyo.

Hata hivyo, amesema mashauri hayo yanalenga kupata taarifa kujua mtu yuko wapi na nani anamshikilia na kama yuko hai au la. Amesema hiyo si kesi ya mikataba bali ni suala la uhai na kifo, hivyo hata taarifa zinapokuja kwa wakili zinakuja kwa muktadha huo.

Kibatala amesema mahakama si chuma bali inaendeshwa na wanadamu ambao wanajua pia kuwa kuna suala la woga.

“Hoja kwamba nilikuwa nazifahamu taarifa hizo tangu Julai 17 sijui wenzetu wamezitoa wapi. Lakini pia anayeombewa kutoa ushahidi si mimi bali nimesema toka mwanzo kuwa ushahidi huo utaongeza thamani,” amesema.

Amesisitiza kuwa mahakama inahitaji ushahidi ili kufikia haki na kwamba, utaratibu wa kutoa ushahidi kizimbani kwa kiapo ndiyo unaokoa muda.

Kibatala amesema Bunge liliona kuwa mashauri hayo ni muhimu, kwani yanahusu uhai wa mtu ndiyo maana likatunga sheria kuwa mahakama inaweza kuratibu mwenendo wake jambo ambalo ameeleza hajaliona katika mashauri mengine.

Amesisitiza kuwa, taarifa hiyo ni muhimu katika kujua Polepole yuko wapi au ni nani wanaomshikilia.

Amedai madai ya mawakili wa wajibu maombi kuwa maombi ya ushahidi huo yamekuja baada ya kusoma viapo vyao kinzani si ya kweli, kwani kwenye viapo vyao hawajamtaja DZCO Byagemu.

Amesema shahidi huyo akipanda kizimbani ataweza kuhojiwa na kwa kuwa kuna wakili amepata kiapo na kwa niaba ya ofisi ya ZCO.

Amesema hakuna haki itakayovunjwa kwani mawakili walioapa kwa niaba yake watamwakilisha kwani watamhoji shahidi, akieleza kuwa haki inayozungumziwa si kumnyang’anya Byagemu shamba lake.

Kibatala amesisitiza kuwa kupokea ushahidi kwa mdomo badala ya kiapo si jambo jipya, akiielekeza mahakama katika shauri la Halima Mdee na wenzake dhidi ya Chadema.

Vilevile, amesema hakuna mtego mbaya kwenye shauri kama hilo linalomhusu mtu maarufu.

Kibatala amehitimisha hoja akisisitiza kuwa mahakama ina mamlaka kutoa maelezo yoyote ambayo yanakidhi mazingira ya shauri hilo.

Jaji Maghimbi baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha shauri hilo mpaka saa nane mchana huu kwa ajili ya uamuzi.