NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Uzinduzi wa maabara hizo utafanyika kesho, Oktoba 15, 2025, katika Makao Makuu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Jijini Dar es Salaam.
Maabara hizo zinalenga kuhakikisha vifaa vinavyotumika majumbani na viwandani vinakuwa na viwango bora vya matumizi ya umeme, hatua itakayosaidia kupunguza upotevu wa nishati na gharama za matumizi kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishina wa Umeme na Nishati Jadifu kutoka Wizara ya Nishati, Innocent Luoga, amesema matumizi ya vifaa vyenye ufanisi ni muhimu katika kupunguza mzigo wa matumizi ya umeme kwenye gridi ya taifa.
“Vifaa vyenye viwango bora vitasaidia kwenye matumizi bora ya nishati, hivyo umeme utatumiwa kwa ufanisi na kupunguza upotevu. Tukitumia vifaa vyenye ufanisi, tutapunguza gharama za matumizi ya umeme majumbani,” amesema Luoga.
Ameeleza kuwa vifaa visivyo na ubora huongeza upotevu wa nishati na kuathiri ustawi wa matumizi ya umeme majumbani na kitaifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya, Marc Stalmans, amesema ongezeko la matumizi ya umeme nchini limechochea umuhimu wa kuanzishwa kwa maabara hizo, ili kuhakikisha vifaa vyote vinavyokwenda sokoni vinakuwa na ubora na ufanisi unaotakiwa.
“Idadi ya watu wanaotumia vifaa vya umeme inaongezeka kila siku, hivyo ni muhimu kuhakikisha vina ufanisi kabla ya kufikishwa kwa wananchi,” amesema Stalmans.

Naye Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Metolojia kutoka TBS, Ridhiwani Matange, amesema maabara hizo zimewekewa vifaa vya kisasa vitakavyowezesha upimaji wa viwango vya ufanisi na usalama wa vifaa vya umeme.
“TBS imejipanga kuhakikisha vifaa vinavyopimwa vinakuwa na ubora wa hali ya juu ili kupunguza gharama za umeme kwa wananchi,” amesema Matange.
Ameongeza kuwa wananchi wanaotumia vifaa vilivyonunuliwa kabla ya maabara hizo kuanza kazi hawapaswi kuwa na hofu, kwani TBS itaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vifaa hivyo.
“Tumeendelea kushirikiana na Wizara ya Nishati na TBS katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za nishati ya umeme. Serikali inapaswa kuendelea kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na nafuu ili kufanikisha mabadiliko ya kiuchumi na kijamii nchini,” alisema Lyatuu.
Uzinduzi wa maabara hizo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kudhibiti ubora wa vifaa vya umeme nchini, na kuchangia katika juhudi za serikali za kuhakikisha matumizi bora ya nishati na kulinda mazingira.