TFF yaufungia Sokoine, Liti, timu nne kutafuta makazi mapya

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limevifungia viwanja viwili kutumika kwa mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Championship kutokana na kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

Viwanja vilivyofungiwa ni Liti uliopo Singida na Sokoine unaopatikana jijini Mbeya, huku ikielezwa vitafunguliwa endapo vitafanyiwa maboresho na kukaguliwa na Shirikisho hilo.

Katika taarifa ya awali iliyotolewa na TFF leo Oktoba 15, 2025, kuhusu kufungiwa uwanja wa Liti, imesema: “Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungia Uwanja wa Liti, Singida kutumika kwa michezo ya Ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

“Miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya Kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu.

“Kufuatia uamuzi huo, timu zinazotumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia uwanja mwingine kama Kanuni inavyoelekeza mpaka uwanja wao utakapofunguliwa, baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF.

“TFF inazikumbusha Klabu zote kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja.”

Taarifa ya kufungiwa uwanja wa Liti ambao Singida Black Stars inautumia kwa mechi zake za nyumbani, ilifuatia na ile ya kufungiwa Uwanja wa Sokoine unaotumiwa na timu za Mbeya City na Tanzania Prisons zinazoshiriki Ligi Kuu Bara sambamba na KenGold ya Championship.

Kufuatia kufungiwa kwa viwanja hivyo, kunazifanya timu tatu za Ligi Kuu ambazo ni Mbeya City, Tanzania Prisons na Singida Black Stars, kutafuta viwanja vingine kwa ajili ya mechi za nyumbani sambamba na KenGold upande wa Ligi ya Championship.

Kesho Oktoba 16, 2025, KenGold inatarajia kuwa mwenyeji wa Gunners kutoka jijini Dodoma katika mechi ya Ligi ya Championship ambapo timu hiyo imepanga kuutumia Uwanja wa Chunya ulipo Mbeya.